Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye. |
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, licha ya kutoeleza
ajenda za kikao hicho, ilisema kitafanyika jijini Dar es Salaam na
kuongozwa na mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete kuanzia saa 4 asubuhi.
Kikao hicho kinafanyika wakati upepo wa kisiasa
ndani ya chama hicho ukiwa haujatulia huku kukiwapo masuala mazito ya
kitaifa yanayotikisa medani za kisiasa, likiwamo suala la uandikishaji
wapiga kura, maandalizi ya kura ya maoni za kupitisha Katiba
Inayopendekezwa na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, ambayo
yameelezwa na wachambuzi wa siasa kuwa hayawezi kukwepeka katika kikao
hicho.
Itakumbukwa kuwa kikao hicho kitafanyika ikiwa ni
siku 10 baada ya kukamilika tarehe ya mwisho ya adhabu kwa makada sita
wa CCM, waliokuwa wakitumikia adhabu ya miezi 12 kwa ukiukwaji wa
maadili kwenye mchakato wa kutaka kuteuliwa na CCM kugombea urais.
Kikao kilichopita cha CCM kilichoketi Januari 13,
mwaka huu kilibainisha kuwa baada ya muda wa adhabu zao kuisha, Kamati
Kuu ingefanya tathimini kuona iwapo wagombea hao walizingatia masharti
ya adhabu zao na endapo kungekuwa na ambao hawakuzingatia masharti
adhabu zao zingeongezwa.
Wiki iliyopita, Nnauye alithibitisha kuwa muda wa
adhabu hiyo ulikuwa ukingoni na kuwa viongozi hao wangefanyiwa tathmini
na kamati ndogo ya maadili ili kubaini iwapo adhabu hiyo ilitekelezwa
ipasavyo.
Makada waliokuwa wakitumikia adhabu hiyo ni Waziri
Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
Wengine ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba, Waziri wa Kilimo na Ushirika, Stephen
Wasira na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Kikao hicho huenda pia kikazungumzia mwenendo wa
uandikishaji wa wapiga kura katika Daftari la Kudumu kwa kutumia
teknolojia ya alama za vidole (BVR), iliyozinduliwa jana na Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda.
CCM, ni miongoni mwa vyama vya siasa nchini
vinavyoungana na vyama vinavyounda Umoja ya Katiba ya Wananchi (Ukawa),
kuhoji mara kwa mara ufanisi wa mfumo wa BVR katika kuandikisha
wapigakura kutokana na historia yake isiyoridhisha.
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini, Dk Benson Bana wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, alisema anaamini CCM itajadili pamoja na mambo
mengine, matokeo ya Kamati ya ndogo ya maadili inayoongozwa na Makamu
Mwenyekiti wa Chama hicho, Philip Mangula, iliyojadili suala la wagombea
na kashfa ya Tegeta Escrow.
Dk Bana alitolea mfano suala la kashfa ya ufisadi
katika Akaunti ya Escrow kuwa ni suala mbalo CCM wanaweza wakaamua
kulibeba kama hoja na kuyapeleka kwa ajili ya kujadiliwa na kikao hicho
kikubwa cha chama.
“Hili suala la ufisadi wa Tegeta Escrow ni
‘critical issue’, ni muhimu kwa chama chao kulijadili na kuja na majibu
ya maswali yanayowasumbua wananchi wengi, hasa ukizingatia kuwa suala
hilo lilikitikisa sana chama hicho,” alisema Dk Bana.
Alisema jambo lingine linaloweza kuchukuliwa kama
ajenda katika kikao hicho na kuamua kulijadili ni wale wanachama wake
waliojitangaza kugombea urais na ambao waliopewa adhabu ya mwaka mmoja
ambapo anasema wanaweza kutaka kufanya mapitio, kama walitekeleza
maagizo
“Vile vile wanaweza kuangalia kalenda ya uchaguzi
ya chama chao na wajadili na kupendekeza utaratibu wa jinsi ya kuwapata
wagombea wao…vile vile lipo suala la hali ya siasa nchini, hali
imebadilika, upepo hauvumi kuelekea CCM,” alisema.
Aliongeza kuwa masuala mengine wanayoweza kujadili
ni matukio ya kutisha na yasiyo ya kawaida yanayojitokeza nchini kama
vile matukio ya kutekwa kwa watu na kuteswa, kuibuka kwa panya road na
mengine yanayofanana na hayo ambayo anasema ni ukweli ulio wazi kuwa
matukio hayo yanaashiria kuvurugika kwa amani na utulivu wa nchi.
“Matukio mengi yasiyo ya kawaida yameibuka hivi
karibuni, mfano suala la vijana wa JKT nao wanaandamana wanataka ajira,
lakini kila mtu anajua kuwa wale vijana wanajulikana wanafundishwa
kujenga nidhamu, sasa wanaandamana, kunaonekana lipo tatizo nchini. Yote
haya hayaleti mwelekeo mwema kwa jamii,” alisema.
Aliongeza kuwa, “tuhuma nzito zinazowakabili
wanachama wake wanajua madhara yake na wanajaribu kutaka kuyarekebisha
ili kurejesha ushindi ambao kwa kweli unaonekana kuwaendea vibaya. Haya
yote yanaweza kuwasukuma kuitisha vikao nyeti kama hivi na kujadili
mustakabali wa chama chao ili waendelee kupata ushindi wa kishindo.
Alisema kitu kingine muhimu ambacho hawawezi
kukikwepa kukijadili ni pigo walilolipata katika chaguzi za serikali za
mitaa, ambapo chama hicho kilionekana kupata anguko kubwa kuliko
matarajio.
Mengine aliyosema yanawezwa yakawa ajenda katika
kikao hicho ni pamoja na kura ya maoni ya Katiba iliyopangwa kufanyika
Aprili 30, mwaka huu, muda anaosema hata wana CCM wenyewe wanajua kuwa
hautoshi.
Mhadhiri mwingine wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
Richard Mbunda alisema kubwa ambalo CCM linalowahangaisha na ambalo kwa
namna yoyote huenda likawa miongoni mwa ajenda katika kikao chao ni
kuleta utulivu wa ndani ya chama na kumjua mwanaCCM atakayepeperusha
bendera yao.
“Nadhani hata wale wanachama wake sita waliopewa
adhabu bado hawajaelezewa kama adhabu zao zimekwisha. Ingawa muda wa
adhabu umekwisha, lakini hawajaelezwa hatma yao, kwa hiyo hili ni jambo
muhimu ambalo hawawezi kuliacha.
Mbunda alisema jambo lingine muhimu kabisa ambalo huenda itapewa
uzito ni hili la kumpata mgombea anayekubalika katika jamii na ambaye
ataweza kupeperusha vyema bendera ya chama na kukubalika na makundi
yote.
“CCM waliozoea kuwa hakuna sababu ya kuangalia ni
mgombea gani anayekubalika na jamii kwa imani kuwa wakisimamisha yeyote
atapita, hali ya sasa kwa namna yoyote lazima waweke mtu anayekubalika
katika jamii na hii ni ajenda kubwa inayohitaji mjadala mpana.
“Na ile tabia ya kutengeneza mazingira fulani awepo na huyu asiyepo, lazima waichukulie kwa uangalifu,” alisema Mbunda.
Mbunda alisema jambo lingine ni suala la kura ya
maoni ya Katiba, ambalo pia ni suala nyeti na muhimu kwa CCM na kuwa
wanapaswa wajipange vyema endapo wanataka Katiba waliyoipendekeza ipite.
0 comments:
Post a Comment