UTOROSHAJI MADINI: SERIKALI YAOKOA mil. 73/-!!


 

SERIKALI imepata sh. milioni 73 zilizotokana na mnada wa kwanza wa madini yaliyokamatwa yakiwa yanasafirishwa nje ya nchi kinyume cha utaratibu kupitia viwanja vikubwa vya ndege uliofanyika jijini Arusha, Novemba 2014.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), Dominic Rwekaza, aliyasema hayo kwenye kikao kati ya Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga, watendaji wa Wizara hiyo na Taasisi zinazosimamia Sekta ya madini nchini kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

Alisema kabla ya kupiga mnada madini hayo, wahusika walifikishwa mahakamani na kuhukumiwa ambapo madini hayo yalitaifishwa kwa mujibu wa sheria ya madini ya mwaka 2010.

Baadhi ya madini yaliyokamatwa yalipelekwa kwenye Maonesho ya Vito ya Kimataifa ya Arusha yaliyofanyika Novemba 2014 na kunadiwa kwa wadau.

"Hadi Desemba,2014, ukaguzi uliofanyika kupitia madawati yaliyopo katika viwanja vikubwa vya ndege vya Julius Nyerere, Kilimanjaro na Mwanza ambao umewezesha kukamatwa kwa watoroshaji wa madini katika matukio 64 tofauti.

"Matukio hayo ni yale yaliyoripotiwa katika viwanja hivyo tangu kuanzishwa kwa madawati hayo Julai 2012...matukio hayo yalihusisha madini yenye thamani ya sh. bilioni 15.9," alisema.

Rwekaza aliongeza kuwa, Wakala huo pia umekuwa ukikagua gharama za uwekezaji na uendeshaji wa migodi mikubwa na ya kati ili kukusanya taarifa sahihi za kodi na kuziwasilisha kwa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) na mamlaka nyingine.

Alisema kutokana na ukaguzi huo, baadhi ya migodi mikubwa imeendelea kulipa kodi ya mapato ambapo hadi kufikia Desemba 2014, sh. bilioni 551.73 zimelipwa kwa Serikali kama kodi ya mapato na migodi ya Geita, Golden Pride na Tulawaka.

"Ukaguzi uliofanywa na Wakala umewezesha sh. bilioni 18.16 kulipwa serikalini na baadhi ya wamiliki wa migodi mikubwa na ya kati baada ya kubainika kutolipwa hapo awali.

"Kiasi hiki kinahusisha malipo ya mrabaha, kodi ya zuio, kodi zitokanazo na mishahara ya wafanyakazi na kodi nyingine," alisema Rwekaza na kuongeza kuwa, kutokana na kaguzi zinazofanywa na Wakala, halmashauri mbalimbali zenye migodi zimeendelea kulipwa ushuru wa huduma kwa mujibu wa sheria zilizopo.

Kikao hicho kati ya Kitwanga, watendaji wa Wizara na Taasisi zinazosimamia sekta ya madini nchini, kilikuwa cha kwanza baada ya Naibu Waziri huyo kuanza kuisimamia sekta ya madini.

Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment