Wabunge jana waliwaweka kitimoto mawaziri wanne wakiwataka watoe maelezo ya kukwama kwa baadhi ya mambo katika wizara zao na kusababisha matatizo kwa wananchi na Serikali kukosa fedha.
Mawaziri hao ni wa Maliasili na Utalii, Lazaro
Nyalandu; Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; William Lukuvi, Waziri
wa Maji; Profesa Jumanne Maghembe na Waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika, Stephen Wasira.
Wakichangia taarifa ya utekelezaji wa shughuli za
Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji na ile ya Ardhi, Maliasili na
Mazingira, wabunge hao walionekana kukerwa na ahadi zisizotekelezeka za
mawaziri hao kiasi cha wao kukata tamaa.
Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola akichangia
taarifa hizo aliwashukia mawaziri watatu kwa wakati mmoja akieleza
kuhusika kwao kukwamisha baadhi ya mambo.
Alisema migogoro ya ardhi nchini haitakwisha kama
viongozi ndiyo wanaohusika kulinda baadhi ya watu. “Wako viongozi
wanahodhi ardhi na kusababisha matatizo, mwekezaji wa Oysterbay Villa,
Lukuvi ndiye alimsaidia kupata eneo alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam,” alisema Lugola na kuongeza:
“Sasa leo amekuwa Waziri wa Ardhi, itakuwaje? Mimi
nitaichoma moto mbeleko inayombebea huyu mwekezaji kitendo kinachozuia
Kinondoni kupata Sh3 bilioni. Huyu mwekezaji ana kiburi alizuia hata
kamati kutaka kuingia kwenye eneo hilo lakini nikatumia ubaunsa wangu
tukaingia.”
Hata hivyo, hoja ya Lugola kuhusu Lukuvi na
mwekezaji huyo ilipingwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto
Kabwe ambaye alisema waziri huyo alisaidia hata kubadilisha mkataba wa
umiliki wa Oystebay Villa, hivyo amwache.
Lugola akiendelea kuchangia alimshukia Waziri
Maghembe kwamba anapeleka maji katika eneo lake tu wakati wananchi wa
jimbo la Mwibara na Bunda wakiteseka kwa mradi wao wa maji
kutokukamilika.
“Waziri alisema uongo hapa kwamba mradi
umekamilika kumbe ni uongo, niliwahi kuomba Rais atoe hawa mawaziri
mizigo na nimefurahi amefanya mabadiliko hivyo naomba yawe ya tija,”
alisema na kuongeza: “CCM isipigiwe kura hata mimi wasinipigie kama
mradi wa maji hautakamilika.”
Kuhusu Kilimo alieleza kuwa wanailinda Bodi ya Pamba na ndiyo maana kuna uchakachuaji mkubwa wa mbegu za pamba.
Alimtaka Nyalandu kwenda Mwibara kufanya mkutano na mamba na viboko ambao wanakula wapigakura wake huku akikaa kimya.
“Lazaro Nyalandu uende ukawazuie mamba na viboko
na kama unataka kwenda Ikulu halafu umeshindwa kuzuia mamba je, ukiwa
Ikulu utaweza kweli? alihoji Lugola.
Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa Kwela (CCM), Ignas Malocha
aliwashukia Nyalandu na Profesa Maghembe kwa kutoa ahadi ambazo
wameshindwa kutekelezeka.
Alisema ameshalalamikia suala la mamba katika jimbo lake lakini waziri amedanganya zaidi ya mara tatu bungeni.
“Nimeshazungumza hili suala la mamba hadi
nimechoka, waziri anadanganya zaidi ya mara tatu na ameshindwa kutatua
tatizo la mamba,” alisema Malocha huku akisema haiwezekani waziri akawa
anasema uongo.
Alimgeukia Profesa Maghembe akieleza kuwa ni
lazima aseme ni lini mradi wa maji katika Jimbo la Kwela na Sumbawanga
kwa ujumla utakamilika...“Utuambie suala la maji mmefikia wapi mbona
mnatudanganya?”
Kwa upande wake, Zitto alimweka Nyalandu kwenye
wakati mgumu pale alipomwambia kuwa kama hatatoa tangazo la Serikali
kuhusu kuanza kutumika kwa tozo mpya za Tanapa katika hoteli zilizopo
katika hifadhi zake, basi awasilishe barua ya kujiuzulu kwa Rais kwa
kuwa ameisababishia Serikali hasara ya Sh80 bilioni.
Taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira
ilieleza kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii haijatekeleza hukumu
iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha iliyotaka wizara kutoa
tangazo la kuanza kutumika kwa tozo mpya.
Taarifa hiyo iliyosomwa na Mwenyekiti wa kamati
hiyo, James Lembeli imeeleza kuwa ni miezi minne sasa tangu hukumu hiyo
itolewe lakini wizara haijatekeleza na kusababisha kupotea kwa Sh2
bilioni kila siku.
Akizungumzia taarifa hiyo, Zitto alisema
anashangazwa kuwa waziri yupo halafu anashindwa kutekeleza agizo na
akalitaka Bunge lichukue hatua.
Zitto alishangazwa pia na taarifa ya kamati kutokutoa maagizo ya kufanya bali kushauri tu, jambo ambalo alisema lina walakini huku akihusisha jambo hilo na ushirikiano wa pacha watatu yaani Nyalandu, Lembeli na Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa ambaye ni Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii.
Zitto alishangazwa pia na taarifa ya kamati kutokutoa maagizo ya kufanya bali kushauri tu, jambo ambalo alisema lina walakini huku akihusisha jambo hilo na ushirikiano wa pacha watatu yaani Nyalandu, Lembeli na Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa ambaye ni Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii.
“Haiwezekani hapa kuna mapacha watatu, waziri,
mwenyekiti na waziri kivuli. Itakapofika jioni kama hajatoa tangazo
tusimuone humu bungeni, upeleke barua ya kujiuzulu kwa Rais,” alisema
Zitto.
Akijibu hoja zilizotolewa na wabunge, Waziri
Lukuvi alisema atapambana na tatizo la migogoro ya ardhi nchini na
kusisitiza kuwa Serikali itachukua mashamba yote makubwa ambayo
hayaendelezwi.
Pia, alijibu hoja ya mwekezaji wa Oysterbay Villa akisema katika
siku 10 alizokaa katika wizara hiyo, ametatua mgogoro huo
hajausababisha kama Lugola alivyodai.
“Hati ilikuwa inaonyesha ni miaka 99 hivyo mimi
nikaishusha hadi miaka 47 hivyo Kinondoni wameruhusiwa kukagua
appartiments zao,” alisema.
Kwa upande wake, Waziri Nyalandu alitumia muda
wake kuelezea tatizo la tozo ambalo wabunge wamelimlaumu akieleza kuwa
kiasi cha Sh80 bilioni ambacho kinalalamikiwa ni cha miaka minane ambayo
kesi ilikuwa mahakamani.
Alisema hata mahakama iliyotoa hukumu iliwashangaa
wanasheria wa Tanapa kwa kushindwa kuishauri Serikali kutoa tangazo
hilo. Baada ya kubanwa baadaye, Nyalandu alisema tangazo hilo litakuwa
limetolewa ifikapo Februari 15.
Akijibu hoja za Wizara ya Kilimo, Wasira alisema anayafahamu matatizo kilimo hivyo atayashughulikia.
Akijibu hoja ya Lugola alisema anayajua matatizo
ya wakulima wa pamba hivyo ataitisha kikao cha wabunge wote wanaotoka
maeneo yanayolimwa pamba ili kupanga mikakati ya kushughulikia matatizo
yaliyopo.
Profesa Maghembe alimshangaa Lugola kwa kutoa
shutuma dhidi ya wizara yake wakati katika Jimbo la Mwibara limepatiwa
miradi minne ya maji iliyokamilika na mitano inakaribia kumalizika ikiwa
juu ya asilimia 50.
“Kama Lugola hayaoni haya basi naomba Spika mumsaidie apelekwe hospitali akapimwe,” alisema Profesa Maghembe.
0 comments:
Post a Comment