KIKWETE AWAJIA JUU VIONGOZI WILAYA YA KINONDONI!!

Rais Jakaya Kikwete akitazama maji yaliyofurika kwenye makazi wa watu eneo la Tegeta, alipofanya ziara ya kuangalia maeneo yaliyoathirika kwa mvua wilayani Kinondoni, jana 
Rais Jakaya Kikwete amewashukia watendaji wa Wilaya ya Kinondoni kwa kushindwa kuondoa maji yaliyozingira makazi ya watu eneo la Tegeta Basihaya, Dar es Salaam.
 
Akiwa katika ziara iliyochukua saa moja na nusu katika eneo la Tegeta na Mkwajuni wilayani Kinondoni jana, Rais Kikwete aliwakemea watendaji wa halmashauri hiyo kwa kushindwa kuchukua hatua za haraka kuyaondoa maji kwenye nyumba hizo.
“Ninawataka viongozi na watendaji wa Manispaa ya Kinondoni kuyaondoa maji ya mafuriko yaliyozingira nyumba zaidi ya 200… kuyaacha maji hayo hadi sasa ni uzembe.
“Maisha lazima yaendelee kwa wakazi hawa, mafuriko yamewakumba wananchi wetu lakini tangu mvua ianze wiki mbili zilizopita watendaji na wahandisi hamjachukua hatua ya kuyaondoa maji haya ili watu waendelee kuishi,” alisema.
Kwa wiki mbili, mvua zinazoendelea kunyesha, watu 12 wameripotiwa kufa kutokana na mafuriko huku mamia wakiyahama makazi yao.
Akizungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, Meya wa Manispaa Yusuph Mwenda, watendaji na wakazi wa eneo hilo, Rais Kikwete alisema: “Kuanzia sasa naagiza maji haya yaondolewe ili wananchi warudi kwenye makazi yao. Wahandisi mnafahamu namna ya kuyaondoa, tumieni elimu yenu ya uhandisi kuyaondoa.”
Baada ya kuwasili Tegeta Basihaya saa 6.00 mchana, Rais Kikwete alionyeshwa na Makonda nyumba zilizozingirwa na maji huku akimweleza kuwa wana mpango wa kuweka mifereji itakayoondoa maji hayo na kwamba Sh3 bilioni zinahitajika kwa kazi hiyo.
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema: “Nguvu kubwa ielekezeni kuyaondoa maji hayo baada ya hapo mtakaa kupanga namna ya kuweka mifereji ili kuzuia mafuriko hapo baadaye, hakuna sababu za kuanza kujadili bajeti hapa.”
Alisema ili mafuriko katika eneo hilo yasiweze kurudia tena katika miaka ijayo, ni lazima baadhi ya nyumba zibomolewe ili kupisha maeneo ya kuweka mifereji hiyo.
“Mimi si mhandisi lakini hapa ni lazima baadhi ya nyumba zibomolewe ili mtengeneze miundombinu ya kupitisha maji vinginevyo kila mwaka kutakuwa na mafuriko.”
Akiwa katika Bonde la Mkwajuni, Rais Kikwete alisema Serikali itatoa viwanja kwa wakazi wa mabondeni watakaoamua kuhama ili kujiepusha na maafa ambayo yamekuwa yakitokea kila mwaka... “Serikali itawapa viwanja watakaohama mabondeni, nawashauri mhame, haya maisha ya kuishi kwa wasiwasi kila mwaka si mazuri.”
Alisema wananchi hao wanajirudisha nyuma kiuchumi kwa sababu wamekuwa wakipoteza vifaa vyao kwenye mafuriko hayo...
 “Mwaka huu unanunua vifaa vyako lakini vinakuja kuchukuliwa na mafuriko, maisha gani haya ya shida kila mwaka.”

Mkazi wa Tegeta Pwani, Halima Athumani alilia mbele ya Kikwete akitaka awaondoe matajiri waliojenga nyumba na kuziba mifereji ya kupitisha maji.
“Baba tusaidie huku kuna matajiri ambao wanajenga majengo makubwa bila kuzingatia maisha ya wengine, kama mafuriko haya yangetokea usiku tungekuwa tumekufa, wanajenga na kuziba mikondo ya maji,” alisema.
Rais Kikwete alimsikiliza na kusema viongozi wa manispaa hiyo wamemsikia na akaagiza ufanyike mkutano ili kutatua kero hiyo.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment