‘Daladala’ ya Mv Dar es Salaam kuzinduliwa!!

Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli (kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo wakitoka katika Kivuko cha MV Dar es Salaam baada ya kuwasili katika Gati ya Mbegani wilayani Bagamoyo mkoani Pwani jana.
Waziri wa Ujenzi Dk John Magufuli amekagua safari ya kivuko cha Mv Dar es Salaam kwa mara ya kwanza hadi Bagomoyo, huku kukiwa na changamoto kadhaa miezi michache kabla ya uzinduzi rasmi wa huduma hiyo.
 
Huduma za kivuko hicho, kilichowasili nchini mwishoni mwaka jana, zinatarajiwa kuzinduliwa muda wowote na Rais Jakaya Kikwete na kurahisisha usafiri kwa wakazi wanaokaa pembezoni mwa pwani hiyo.
Dk Magufuli aliwambia watu waliofika kushuhudia ukaguzi huo jana kuwa kivuko hicho kitasaidia kupunguza foleni na kukuza utalii.
Alibainisha kuwa kuchelewa kwa huduma ya kivuko hicho kunatokana na kuendelea kwa ujenzi wa sehemu za kupakia abiria ambazo ni za kisasa zaidi.
Alisema, kwa sasa Kikosi cha Maji cha Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kimejenga sehemu za kupandia za dharura na kwamba wanatarajia kumaliza kazi kuu ndani ya siku 10 hadi 15 zijazo.
“Hiki kivuko ni cha aina yake hata maegesho yake ni tofauti. Niwapongeze wenzetu wa jeshi na nina uhakika wataifanya kazi ya kujenga kwa haraka,” alisema Dk Magufuli.
Alisema, Kivuko hicho chenye uwezo wa kubeba abiria 300, kitakuwa kikifanya safari zake katika vituo saba na nauli zake zitakuwa nafuu.
“Kulikuwa na maneno mengi kuwa kivuko hakipo… na wale waliokuwa hawaamini kimekuja, wakitaka wakiguse,” alisema Dk Magufuli na kushangiliwa na umati uliokuwa feri kabla ya kuanza ukaguzi.
Mv Dar es Salaam chenye huduma za kisasa ndani zikiwamo televisheni, kaunta ya vinywaji na vitafunwa, kilitumia saa tatu kamili kutoka Dar es Salaam hadi Mbegani, Bagamoyo kikiwa na watu takriban 300.
Tofauti na vile vya Mv Magogoni na Mv Kigamboni, Kivuko cha Mv Dar es Salaam kimejengwa kwa ustadi wa hali ya juu na huduma nzuri za kukaa kama meli ya kitalii.
Katika safari hiyo, baadhi ya wananchi walishindwa kujizuia na kuanza kutapika pale kivuko kilipopatwa na dhoruba ya mawimbi. Hali hiyo iliwafanya wahudumu wa kivuko hicho kupita na kugawa mifuko ya rambo mara kwa mara kuzuia kuchafua chombo hicho.
Hata wakati Watanzania wengi wakisubiri kuanza rasmi kwa safari hizo, ujenzi wa vituo vilivyopo katikati ya pwani hiyo unakabiliwa na changamoto ya mapingamizi ya Mahakama.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mhandisi Mussa Iyombe alisema kuna baadhi ya maeneo ambayo yaliyopangwa kujengwa vituo kama Jangwani yemewekewa pingamizi mahakamani na watu wanaodai ni wamiliki wa viwanja hivyo licha ya umiliki wao kuondolewa.
Maeneo yatakayojengwa vituo vya kivuko hicho ni Kawe, Jangwani, Magogoni, Rungwe Oceanic, Mbweni, Kaole na Mbegani.
Wananchi hao, alisema wanadai fidia kubwa na kwamba wamekuwa wakifuatilia kwa kina kuhakikisha wanatatua tatizo hilo kwa wakati.
“Tunajitahidi kwa hali na mali kuhakikisha tunapoanza kutoa huduma yale maeneo ya kati yawe yanafanya kazi. Hatuwezi kufanya safari za Dar es Salaam hadi Bagamoyo bila vituo hivyo muhimu vyenye wakazi wengi,” alisisitiza Iyombe.
Mara baada ya kupata maeneo hayo watajenga vituo imara, bora, kwa muda mfupi na kwa gharama nafuu kwa kuwa njia zake siyo kubwa.
Aliongeza kuwa mpaka sasa kuna Makandarasi tofauti wanaoendelea kujenga baadhi ya vituo visivyo na mapingamizi na kwamba iwapo kesi hizo hazitawasumbua sana, haizidi miezi sita safari zitaanza.
“Nimewaagiza Jangwani waendelee kujenga hata kama Mahakama itakuja kutusimamisha itafahamika mbele kwa mbele ila tayari tulishawaomba wenye viwanja tuzungumze na watueleze kama wao ndio wamiliki halali,” alidokeza.
Hata hivyo, haraka aliabainisha kuwa uamuzi wowote utakaotolewa na Mahakama watauheshimu wakati wanaangalia namna gani mradi uendelee pasina kuathirika.
Kuhusu suala la nauli, Iyombe alisema watakaa chini kupiga hesabu za gharama za uendeshaji na masuala mengine ya uchakavu ili kubaini kiwango ambacho abiria anatakiwa kukitoa.
Zoezi hilo, alibainisha litatoa picha halisi kama nauli itakua ya kiwango cha huduma au biashara.
“Lengo letu ni kukifanya kivuko kama huduma sasa ikitokea nauli imefikia kiwango cha biashara itabidi Serikali itoe ruzuku. Ni lazima tuhakikishe nauli haizidi sana ile ya basi,” alisema Iyombe.
Ili huduma katika pwani hiyo ziwe na ufanisi, alisema inatakiwa viwepo vivuko viwili vinavyopishana na kutaka sekta binafsi kununua vivuko vyao kuongeza huduma na kujenga maegesho na hoteli katika maeneo ya vituo.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) Marcellin Magesa alisema kivuko hicho kilitengenezwa na Mkandarasi kutoka Denmark Johs Gram-Hassen A/S kwa takriban Sh8 bilioni.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo alisema anashukuru kuanzishwa kwa huduma hizo huku akitoa maombi kwa wizara kuwa iangalie utaratibu wa kupanua barabara kutoka Bagamoyo hadi Mbegani.
Ndikilo alishauri barabara hizo ziwe chini ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na yajengwe maegesho ya kisasa kwa ajili ya wasafiri watakaokuwa wakiacha magari yao.
“Lakini wananchi nao watakuwa wanaumia ukikosekana usafiri wa moja kwa moja kutoka Bagamoyo hadi Mbegani. Kama wengi watakuwa wakishuka Nzinga kuja Mbegani wakitokea Bagamoyo hawataona umuhimu wa Kivuko bora watumie barabara,” alisema.
Katika safari hiyo ya ukaguzi, maofisa wa wizara na idara zilizopo chini ya Wizara ya Ujenzi walipata fursa ya kujionea mandhari nzuri iliyopo katika ukanda wa pwani kati ya Bagamoyo na Dar es Salaam.
Ndani ya kivuko hicho chenye ghorofa moja, kuna viti vya kisasa na kifahari vya rangi ya udongo vilivyopangwa kiustadi, televisheni mbili juu na chini, sehemu za kuchajia simu na feni.
“Huu ni usafiri mzuri na wa starehe sana japo tumetumia muda mwingi kidogo. Kuanzishwa kwa huduma kunatupatia fursa sisi ambao hatujawi kutumia usafiri wa aina hii kwenda Bagamoyo,” anasema Abdul Ali, mmoja wa biria aliyejumuika katika safari hiyo.
Alisema kinachotakiwa ni Temesa kuwaelimisha watu juu ya masuala mbalimbali ya usalama wawapo katika kivuko hicho ili yakitokea maafa iwe rahisi kujiokoa.
“Hizi skrini mbili ningependa ikianza kufanya kazi zionyeshe namna gani mtu ajiokoe akiwa ndani. Hii itatusaidia sana sisi wageni wa usafiri huu wa majini,” alieleza Ali huku akisifia uundaji wa kivuko hicho.
Meneja Mradi wa kampuni iliyounda kivuko hicho Andreas Gottrup alisema kivuko hicho kina kasi inayozidi nautical mile 20 na kimejengwa kwa Aluminiam ili kiwe chepesi zaidi kikiwa majini.
“Tumekijenga kwa ustadi mkubwa kwa usimamizi makini wa Temesa na Wahandisi wa Wizara. Hakuna haja ya kuwa na wasiwasi,” alisema Gottrup.
Kivuko hicho iwapo kikiwa kinafanyiwa matengenezo ya mara kwa mara alisema kinaweza kukaa muda mrefu zaidi ya miaka 30 hadi hata 100.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment