CHAMA
cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kimekuwa na
utaratibu wa kila mwaka kutoa tuzo.
kwa wanamichezo wanaofanya vizuri na
sherehe za utoaji wa tuzo hizo zimekuwa zikifanyika kati ya miezi ya Mei
na Juni.
Hata hivyo mwaka huu tuzo hizo zimechelewa kufanyika kutokana na
sababu mbalimbali, ambazo zipo nje ya uwezo wa Kamati ya Tuzo, Kamati
ya Utendaji ya TASWA, wanachama wa TASWA, wanamichezo husika na
wwandishi wa habari za michezo kwa ujumla wao.
Ndugu zangu ninyi ni mashahidi wa tuzo za miaka miwili iliyopita, zilivyofana na zikabaki kupigiwa mfano kwa ubora wake.
Lakini mwaka huu, mambo kidogo yalikuwa magumu kutokana na
kampuni ambayo sitaitaja jina, ambayo awali ilituhakikishia ingedhamini
kwa asilimia 100 lakini ilipata matatizo ya kiuchumi wiki tatu kabla ya
tarehe tuliyokuwa tumepanga kufanya tuzo, hivyo wakatuomba tusogeze
mbele huenda mambo yangeimarika.
Kuanzia hapo kila mara wakawa wanatuhakikishia mambo yatakuwa
mazuri, lakini mwezi Agosti mwishoni wakatupa taarifa rasmi kuwa
hawatamudu kudhamini tuzo zetu, hali ambayo ilituchanganya kwa kiasi
kikubwa kwani ingekuwa vigumu sana kupata wadhamini wa ghafla kwa wakati
huo.
Hata hivyo kutokana na heshima ambayo TASWA imejijengea na
kuaminika mbele ya jamii kwa kushirikiana na Kamati ya Tuzo, tukaanza
mazungumzo na kampuni mbalimbali na tayari tumepata kampuni mbili za
kutusaidia, huku tukiendelea na juhudi zetu za kupata wadhamini wa
kutosha kulingana na bajeti yetu.
Leo ninayo furaha kuwatangazia kuwa Desemba 20 mwaka huu,
tutafanya Tuzo ya Wanamichezo Bora wa mwaka 2012 katika ukumbi ambao
tutautangaza hivi karibuni na maandalizi yamefikia hatua nzuri sana.
Tumefanya vikao kadhaa cha mwisho kikiwa jana kati ya Kamati ya
Utendaji ya TASWA na Kamati ya Tuzo, tumetafakari athari za kuchelewa
kufanya na zile za kuacha kufanya, tukajiridhisha ni bora tufanye ingawa
tumechelewa, lakini lazima tuwaenzi wanamichezo waliofanya vizuri mwaka
uliopita.
Tunaomba radhi wanamichezo wanaowania tuzo hizo, vyama
mbalimbali vya michezo na wote ambao kwa namna moja au nyingine
kuchelewa kwetu kuliwakwaza, lakini hatukuwa na jinsi yote ni katika
kuhakikisha tuzo zetu zinakuwa bora kama miaka iliyopita.
Tayari majina ya awali ya wanaowania tuzo kwa michezo mbalimbali
tulishayatangaza, ni jukumu sasa la Kamati ya Tuzo kuendelea na
mchakato ili kuhakikisha zinakuwa nzuri zaidi.
Haji Manara
Mwenyekiti Kamati ya Tuzo
3/10/2013
0 comments:
Post a Comment