
Wakati ikisubiriwa ripoti ya uchunguzi wa
Tume Maalumu iliyoundwa kwa Azimio la Bunge kuchunguza kashfa ya vigogo
walioficha Sh323.4 bilioni katika benki nchini Uswisi, Shirika la
Kimataifa la Mtandao wa Ulaya wa Madeni na Maendeleo (Eurodad), leo
linaanza kuwachunguza walioficha mabilioni hayo ya fedha nchini humo.
Kazi hiyo ya uchunguzi inaanza leo hadi
Novemba 5, mwaka huu, ambapo pamoja na mambo mengine watafanya ziara ya
uchunguzi kuhusu masuala ya uwazi katika kodi katika nchi za Ulaya.
Uchunguzi huo utafanywa na jopo la
wataalamu waliobobea katika masuala ya kodi na maendeleo na wataongozwa
na Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe ambaye
pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema.
Sakata la kashfa hiyo liliibuliwa bungeni
kwa hoja binafsi ya Zitto, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini,
mwishoni mwa mwaka 2012.
Zitto alisema kwamba kiasi cha fedha kilichofichwa nchini Uswisi ni kikubwa zaidi ya hicho kilichotajwa.
Kufuatia hoja hiyo, Bunge chini ya Spika
Anne Makinda liliipa Serikali kipindi cha mwaka mmoja ambacho kinaishia
Oktoba mwaka huu, iwe imekamilisha uchunguzi na kuwasilisha ripoti hiyo
bungeni.
Ripoti ya Tume hiyo iliyoundwa na
Serikali kwa Azimio la Bunge ilitolewa mwishoni mwa mwaka jana,
ikiongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema,
mpaka sasa tayari imewahoji vigogo 200 wakiwamo wabunge, wanasiasa na
wafanyabiashara.
Muda wa tume hiyo kufanya uchunguzi
unakamilika mwezi huu na inatarajiwa katika mkutano ujao wa Bunge
unaoanza Oktoba 29 mjini Dodoma, itawasilisha ripoti hiyo.
Taarifa zilizolifikia Mwananchi Jumapili
na kuthibitishwa na Zitto jana jioni zilieleza kuwa Eurodad ambao ni
mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali 48 kutoka nchi 19 za Ulaya,
yanayojihusisha na masuala ya kufuatilia madeni ya nchi zinazoendelea,
kwa muda sasa umekuwa ukipambana na watu wanaokwepa kulipa kodi.
"Mashirika haya yamekuwa kwenye kampeni
ya kupinga utoroshwaji wa fedha kupitia ukwepaji kodi unaofanywa na
mashirika ya kimataifa kwa nchi zinazoendelea," ilieleza sehemu ya
taarifa hiyo.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa kesho Zitto
atakutana na Waziri wa Fedha wa Uswisi na maofisa wa benki mbalimbali na
asasi za kiserikali zilizopo katika mji mkuu wa nchi hiyo, Geneva.
"Zitto pia atahudhuria mkutano wa Kamati
ya Kodi ya Umoja wa Mataifa katika kampeni ya kubadili mfumo wa kodi za
kimataifa ili kuzuia unyonywaji wa nchi za Kiafrika unaofanywa na
kampuni kubwa za kimataifa," inaeleza taarifa hiyo.Juzi 21 mwaka huu,
Werema alizungumza na Mwananchi Jumapili na kuthibitisha kuhojiwa kwa
vigogo hao 200, lakini akasita kuwataja kwa majina kwa maelezo kuwa
asingeweza kuwataja kwa kuwa uchunguzi bado ulikuwa unaendelea.
"Uchunguzi huo unaendelea," alisema
Werema huku akisita kueleza kwa undani juu ya kazi hiyo kwa kile
alichosema kuwa hana sababu ya kufanya hivyo kwa sasa.
"Subiri uchunguzi bado unafanywa," alisema Werema na alipotakiwa kueleza utamalizika lini alisema: "Utamalizika tu."
Uchunguzi wa walioficha mabilioni ya
Uswisi uliibuka baada ya Benki ya Taifa ya Uswisi (SNB) kutoa taarifa
Juni, 2012 kuhusu raia wa kigeni wanaomiliki akaunti za benki nchini
humo.
Orodha hiyo iliorodhesha pia baadhi ya
Watanzania wenye akaunti zenye fedha zinazofikia Dola196 milioni ambazo
ni sawa na Sh323.4 bilioni.
Jarida la kimataifa la uchunguzi la 'The
Indian Ocean Newsletter' toleo la hivi karibuni, lilimnukuu Werema
akisema uchunguzi huo kwa sasa unatia matumaini.
Mbali na Werema, tume hiyo inaundwa na
viongozi kadhaa wa taasisi nyeti kama vile Mkurugenzi wa Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hosea, Mkurugenzi wa
Usalama wa Taifa, Rashid Othman na Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa
Benno Ndulu.
Tume hiyo inawahusisha pia Mkuu wa Sheria
wa BoT, Mustapha Ismail na maofisa kutoka idara ya upelelezi na Ofisi
ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali.
Kwa mujibu wa jarida hilo la kimataifa,
miongoni mwa watuhumiwa hao ni wanasiasa na majenerali wastaafu
wanaotuhumiwa kutorosha zaidi ya Dola133 milioni mwaka 2005, kupitia
Mfuko wa Ulipaji Madeni ya Nje (EPA)
Baadhi ya watu wanaodaiwa kuhusika
wamehojiwa kutokana na taaluma zao, familia zao, akaunti zao za benki
zilizoko nchini na nje ya nchi pamoja na nchi walizotembelea mara kwa
mara kwa miaka mitatu iliyopita.
Lengo la kuwahoji inaelezwa ni kutaka
kujua iwapo walifuata njia zinazotakiwa katika kufungua akaunti hizo nje
ya nchi na iwapo fedha zilizohifadhiwa huko zilipatikana kihalali.
Akiwa mkoani Tabora wiki moja iliyopita
katika mikutano ya kuimarisha chama, Zitto alisema tayari amemwandikia
barua Katibu wa Bunge kutaka taarifa ya uchunguzi huo itolewe katika
mkutano ujao.
CHANZO MWANANCHI.
POSTED BY:www.info@dirayetu.blogspot.com
0 comments:
Post a Comment