TUME ya
Uchaguzi nchini (NEC) inadaiwa kuingia katika mchakato wa mwisho wa
kuzipa zabuni ya kuandaa vifaa vya Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 kampuni za
M/S Jazzmatrix Cooperation na M/S Invu IT Solution zinazodaiwa kuwa na
rekodi mbaya ya utendaji.
Tanzania
Daima limedokezwa kuwa mkakati huo unahusishwa na njama za kutaka
kukibeba Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi huo kwa kuchakachua
matokeo ya kukibakiza madarakani.
Kampuni hizo
ambazo katika zabuni ya Tume ya Uchaguzi zimetajwa kushirikiana na
Kampuni ya Kitanzania ya M/S SCI Tanzania Limited, mbali ya kutojulikana
zinapotoka, pia ndizo zimekuwa na gharama kubwa kuliko kampuni nyingine
zilizoomba kazi hiyo.
Kiwango
ambacho kampuni hizo zilitaja na kukubaliwa na NEC kwa ajili ya kuandaa
vifaa vya kielektroniki vya kusajili wapiga kura (Biometric Voters
Registration) ni zaidi ya euro milioni 60, sawa na sh bilioni 126.3,
wakati kampuni zinazofuata zikihitaji kuanzia euro milioni 40.
Naibu Katibu
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe, ni
mmoja wa viongozi waliofichua mkakati huo, akidai unafanywa na serikali
ya CCM ili kuhakikisha wanajiandaa kudhibiti kila eneo ili waweze kubaki
madarakani.
Alisema
lengo ni kuhakikisha mchakato wa vitambulisho vya kupigia kura vya
kielektroniki vina kuwa na faida kwa CCM na kukiingizia fedha chama
hicho za kutumia kwenye uchaguzi huo kupitia mfumo huo dhaifu wa
vitambulisho hivyo.
Zitto alisema kutokana na hali hiyo, amemwandikia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) barua ya kutaka
ukaguzi wa zabuni hiyo ufanyike kwa kushirikisha Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru) na vyombo vingine vya usalama kwa ajili
ya kujiridhisha.
“Wenzetu CCM wanafanya mikakati ya kujiandaa na Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa kuhakikisha wanapata fedha za kutoshana hata
mazingira mabaya ya vifaa vitakavyotumika katika upigaji kura na sasa
wameshaingia hata katika Tume ya Uchaguzi kwa ajili ya kutengeneza
mazingira,” alisema Zitto.
Aliongeza
kuwa kiasi kilichotolewa ni kodi ya Watanzania na kwamba ni vema taifa
likajiridhisha kuwa matatizo yaliyotokea Kenya na Ghana hayatajirudia
Tanzania, hasa wakati wa upigaji kura.
Gazeti hili
limeona barua hiyo ya Zitto kwenda kwa CAG, ya Novemba 7, 2013, yenye
kichwa cha habari; ‘Zabuni ya Biometric Voters Registration (BRV KITS)
No. IE/018/2012-13/HQ/G/19 yenye thamani ya sh bilioni 126.3.’
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini anasema kuwa NEC imekuwa katika mchakato wa zabuni tajwa hapo juu.
“Zabuni hiyo
sasa imeanza kuleta malalamiko miongoni mwa wananchi kutokana na
kinachosemekana kuwa kampuni iliyopewa zabuni hiyo haina uwezo
kiteknolojia, pia bei zao ni kubwa.
“Katika
mafunzo ya hivi karibuni ya SADCOPAC jijini Nairobi tuliazimia kuwa ni
vema kwenye zabuni nyeti kama za namna hii, SAIs wawe na uwezo wa
kufanya ukaguzi kabla ya zabuni kutolewa na kuanza kutekelezwa,”
alisema.
Kwa mujibu
wa nyaraka za NEC ambazo Tanzania Daima linazo, kampuni zilizopewa tenda
ya pamoja yenye kugharimu kiasi cha dola 78, 987,636.00, sawa na sh
126,291,375,455 ni M/S Jazzmatrix Cooperation na M/S Invu IT Solution
ambazo hazijulikani nchi zinapotoka zikiwa zinashirikiana na M/S SCI
Tanzania Limited.
Katika
nyaraka hizo kampuni zilizokosa tenda na ambazo zimelalamika kwa
Mkurugenzi wa NEC namna mchakato wa kutoa zabuni hiyo ulivyoendeshwa
zimeainishwa kuwa ni M/S Zetes SA ya nchini Ubalgiji, M/S IRIS
Corporation Technology ya Malaysia, M/S Lithotech Exports ya Afrika
Kusini, M/S Safran Morpho ya Ufaransa na M/S Avante International
Technology, Inc ya Marerkani.
Kampuni hizo
zinahoji njia na sababu zilizowafanya wakose tenda hiyo licha ya kuwa
na uzoefu, vifaa bora pamoja na kuwa na kiwango kidogo cha gharama
tofauti na kampuni iliyopewa kazi.
Katika moja
ya malalamiko yao, Kampuni ya M/S Morpho, inalalamika kutofahamishwa
namna walivyokosa vigezo vya kupata kazi hiyo licha ya kuwa na sifa za
kimataifa za kufanya kazi huku ikiwa imetoa bei nafuu kuliko kampuni
iliyopata kazi.
“Tulikuwa
miongoni mwa washindani muhimu kwa kuwa kiwango chetu kilikuwa ni sh
bilioni 97.8 ambazo ni sawa na euro 44,939,912 + sh 3,843,736,140.
“Ujuzi,
vigezo na uzoefu wetu havilingani, duniani kote tumefanya kazi katika
maeneo mengine kwa ufanisi na tunashindwa kuelewa kivipi walishinda hao
ambao wamepata kazi kwa kiwango cha zaidi ya sh bilioni 27.8
ikilinganishwa na yetu,” ilisomeka sehemu ya barua.
Alipotafutwa
Mkurugenzi wa NEC, Julius Mallaba, alisema hawezi kuliongelea suala
hilo katika simu na kuomba mwandishi awasiliane na Kaimu Mkurugenzi wa
NEC, Dk. Sist Cariah, ambaye alisema mchakato wa kupata kampuni
ulifuatwa kisheria.
Dk. Cariah
alisema si kweli kwamba kampuni iliyopewa kazi haina uwezo bali
malalamiko yanatoka kwa watu walioshindwa kupata kazi hiyo.
Alipoulizwa
juu ya uzoefu wa kampuni hiyo na wapi ilifanya kazi, Dk. Cariah alisema
kwa maelezo waliyonayo ni kwamba kampuni hiyo ina uzoefu wa miaka 35 wa
kufanya kazi, huku akishindwa kuainisha sehemu ilizowahi kufanya kazi.
Kuhusu wapi
zimetoka kampuni hizo, Dk. Cariah alisema suala la kutoainishwa
kimaandishi ni makosa ya kawaida, huku akitaja kuwa zinatoka katika nchi
ya India na Australia.
Kuhusu
gharama, Dk. Cariah alisema licha ya makampuni mengine kutaja gharama za
chini, zingeweza kuwa na gharama kubwa zaidi wakati wa kukamilisha kazi
hiyo kutokana na kuwa na gharama zilizojificha.
POSTED BY:www.info@dirayetu.blogspot.com
0 comments:
Post a Comment