MKUTANO KUHUSU ADHABU MBADALA YA KIFUNGO GEREZANI KUFUNGULIWA NOVEMBA, 2013

JAJI MKUU MOHAMED CHANDE OTHMANJaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman anatarajiwa kufungua mkutano kuhusu masuala ya adhabu mbadala wa kifungo gerezani, utakaoanza kesho (6 Novemba, 2013)  jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo umeandaliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Idara ya Huduma kwa Jamii, kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa linalojishughulisha na Maboresho ya Sheria za Adhabu la Penal Reform International, na utafanyika katika Hoteli ya Holiday Inn, Dar es Salaam.
Lengo la Mkutano huo ni kujadili masuala mbalimbali kuhusu kuboresha adhabu mbadala wa kifungo gerezani na pia kupitia maazimio kuhusu  matumizi ya adhabu mbadala yaliyofikiwa katika Mkutano kama huu uliofanyika nchini Uganda na kuzindua Mtandao unaohusu Adhabu Mbadala wa Kifungo kwa nchi za Afrika, unaojulikana kama ‘African Alternative to Imprisonnment Network’.
Mkutano huu wa kesho utakaoendelea hadi keshokutwa, utawashirikisha Wakuu wa Vyombo vinavyosimamia adhabu mbadala wa kifungo kutoka nchi 10 za Afrika.  Nchi hizo ni  Ethiopia, Kenya, Malawi, Rwanda, Afrika Kusini, Sudani ya Kusini, Uganda, Zambia, Zimbabwe na wenyeji Tanzania.
Mkutano huu ambao unajulikana kama Mkutano wa Uzinduzi wa Mtandao unaohusu Adhabu Mbadala wa Kifungo kwa nchi za Afrika (Africa Alternatives to Imprisonment Network Inaugural Meeting) utafuatiwa na Mkutano mwingine wa Adhabu Mbadala kwa nchi za Afrika Mashariki (East Africa Alternantives to Imprisonment Conference) utaofanyika tarehe 7 hadi 8 Novemba, 2013.
Mkutano huo, mahsusi kwa nchi za Afrika Mashariki, utawashirikisha wawakilishi wa Idara zinazoshughulika na Adhabu Mbadala wa Kifungo (Probation and  CommunityService) na Mashirika ya Kijamii kutoka nchi za Kenya, Uganda na wenyeji Tanzania. Wafadhili na Mashirika mbalimbali ya Kimataifa na washiriki wa Mkutano wa Afrika pia wamealikwa kuhudhuria mkutano huo.
Lengo la mkutano huo wa nchi za Afrika Mashariki ni kubadilishana uzoefu katika kusimamia utekelezaji wa Adhabu Mbadala wa Kifungo na kuweka mikakati ya kuboresha utekelezaji wake kwa nchi za Afrika Mashariki.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
05 NOVEMBA, 2013
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment