Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ameunda kamati mbili maalumu kwa
ajili ya kutathmini muundo wa ligi na kupendekeza namna ya kuboresha,
na kutathmini muundo wa Bodi ya Ligi na kupendekeza namna ya kuuboresha
ikiwemo kuunda kampuni.
Kamati ya Kutathmini Muundo wa Ligi
inaongozwa na Kocha wa zamani wa Taifa Stars, Dk. Mshindo Msolla wakati
Katibu ni Ofisa Mashindano wa TFF, Idd Mshangama. Wajumbe ni Rahim
Kangezi, Amri Said, Sunday Manara, Salim Bawazir na Lucas Kisasa.
David Nchimbi kutoka Delloitte ndiye
anayeongoza Kamati ya Muundo wa Bodi ya Ligi wakati wajumbe ni Edwin
Kidifu (Mwanasheria wa SUMATRA), Jones Paul (Mkurugenzi wa
Sunderland/Symbion Academy), Evans Aveva, John Jambele, Masoud Sanani na
Pelegrinius Rutahyuga.
Wakati huo huo, Rais Malinzi amemteua
Pelegrinius Rutahyuga kuwa Mshauri wa Rais (Ufundi). Mshauri wa Rais
(Utawala) atateuliwa baadaye.
TIKETI 260 KOMBE LA DUNIA BRAZIL ZATOLEWA NCHINI
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa
Miguu (FIFA) limeipa Tanzania mgawo wa tiketi 260 za Fainali za Kombe la
Dunia nchini Brazil.
Watanzania wanaohitaji tiketi hizo
wanatakiwa kutuma maombi TFF kwa maandishi wakielezea aina ya tiketi na
mechi wanazotaka kushuhudia. Hakuna tiketi zitakazoombwa FIFA bila
kuwepo maombi kwa maandishi.
Tiketi zilizopo kwa Tanzania ni
ifuatavyo; kwa hatua ya makundi (ukiondoa mechi ya ufunguzi), raundi ya
16 bora, robo fainali na mechi ya kutafuta mshindi wa tatu ni 250.
Kwa mechi ya ufunguzi, nusu fainali
mbili na fainali (mechi namba 1, 61, 52 na 64) ni tiketi kumi tu ndizo
zitakazopatikana. Bei za tiketi ziko katika viwango vitatu tofauti.
Mechi ya ufunguzi tiketi zake ni dola za
Marekani 495, 330 na 220. Hatua ya makundi (mechi namba 2-48) ni dola
175, 135 na 90. Hatua ya 16 bora (mechi namba 49-56) ni dola 220, 165 na
110.
Robo fainali (mechi namba 57-60) ni dola
330, 220 na 165 wakati nusu fainali (mechi namba 61 na 62) ni dola 660,
440 na 275. Mechi ya mshindi wa tatu ni dola 330, 220 na 165. Kiingilio
kwa fainali kitakuwa dola 990, 660 na 440.
TFF itawasilisha maombi ya tiketi hizo
FIFA kuanzia Desemba 8 mwaka huu hadi Februari 7 mwakani. Idadi ambayo
itaombwa FIFA itatokana na Watanzania waliowasilisha maombi TFF kwa vile
zinaweza zisipatikane tiketi zote hizo zilitengwa kwa Tanzania.
Hivyo tunasisitiza maombi ya tiketi yatakayofanyiwa kazi ni yale ambayo yamewasilishwa TFF kwa maandishi tu.
AFRIKA KUSINI KUTUA KWA SOUTH AFRICA AIRWAYS
Kikosi cha Afrika Kusini (Basetsana) kwa
ajili ya mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kwa wasichana wenye umri
chini ya miaka 20 dhidi ya Tanzania (Tanzanite) kinatua nchini kesho
(Desemba 5 mwaka huu).
Afrika Kusini itatua Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) itatua saa 8 kamili mchana kwa ndege
ya South Africa Airways.
Wanaounda Basetsana ni makipa Kaylin
Swart, Regirl Ngobeni na Juliet Sethole. Mabeki ni Abongile Dlani, Caryn
van Reyneveld, Chamelle Wiltshire, Meagan Newman, Nomonde Nomthseke,
Tiisetso Makhubela na Vuyo Mkhabela.
Viungo wapo Amanda November, Amogelang
Motau, Gabriella Salgado, Koketso Mamabolo, Nomvula Kgoale na Thembi
Kgatlane. Washambuliaji ni Mosili Makhoali, obyn Moodaly, Sduduzo
Dlamini na Shiwe Nogwanya.
Viingilio katika mechi hiyo
itakayochezwa Jumamosi (Desemba 7 mwaka huu) ni sh. 1,000 kwa viti vya
rangi ya kijani, bluu na orange, sh. 2,000 kwa VIP C, sh. 5,000 kwa VIP B
wakati VIP A watalipa sh. 10,000.
JOPO LA WATAALAMU KUPANGA MKAKATI WA AFCON 2015
Jopo la wataalamu 20 walioteuliwa na
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi
linakutana kupanga mkakati wa kuonesha jinsi Tanzania inavyoweza
kushiriki Fainali za Afrika (AFCON) zitakazofanyika mwaka 2015 nchini
Morocco.
Kikao hicho maalumu (retreat)
kitafanyika mjini Zanzibar kuanzia Desemba 6-8 mwaka huu. Jopo hilo
litaongozwa na Mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT),
Kanali mstaafu Idd Omari Kipingu.
Wengine wanaounda jopo hilo
linalohusisha pia makocha ni Dk. Mshindo Msolla, Peter Mhina, Ayoub
Nyenzi, Abdallah Kibaden, Pelegrinius Rutahyuga, Kidao Wilfred, Salum
Madadi, Juma Mwambusi, Ken Mwaisabula, Boniface Mkwasa, Fred Minziro,
Meja Abdul Mingange, Ally Mayay, Boniface Mkwasa na Dan Korosso.
Wajumbe wengine wa jopo hilo wanatoka Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA).
Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
POSTED BY:www.info@dirayetu.blogspot.com
0 comments:
Post a Comment