CCM YAWAPA ONYO WANAOJITANGAZIA URAIS KABLA YA WAKATI


Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye akionesha kitabu cha maadili yanayotakiwa kufuatwa na wanaCCM alipokuwa akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Dar es Salaam leo,
 kuhusu onyo walilopewa makada wa CCM wanaodaiwa kutangaza nia ya kuwania urais kabla ya muda kuwadia. Makada hao waliohojiwa na Kamati Ndogo ya Maadili ya chama hicho ni; Mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa,  Frederick Sumaye, Naibu Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano, Januari Makamba, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Mbunge wa Sengerema, Wiliiam Ngeleja  na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira. Makada hao watakuwa chini ya uangalizi kwa miezi 12.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kati ya tarehe 13/02/2014  na tarehe 18/02/2014 kumekuwa na mfululizo wa vikao kadhaa vya Chama kitaifa vilivyoshughulikia suala la maadili ndani ya Chama.
Vikao hivyo ni pamoja na Kamati Ndogo ya Udhibiti tarehe 13-14/02/2014, Tume ya Udhibiti na Nidhamu 18/02/2014 na Kamati Kuu tarehe 18/02/2013.
Waliohojiwa katika mfululizo wa vikao hivi ni wafuatao:-

1. Ndg. Frederick Sumaye
2. Ndugu Edward Lowasa
3. Ndugu Bernard Membe
4. Ndugu Stephen Wassira
5. Ndugu January Makamba
6. Ndugu William Ngeleja

Baada ya kuwahoji ilithibitika kuwa baadhi ya tuhuma dhidi yao ni za kweli na hivyo kupendekeza adhabu.  Mapendekezo hayo yalipelekwa kwenye Tume ya Udhibiti na Nidhamu na hatimaye Kamati Kuu ya CCM ambayo ilitoa adhabu kwa wahusika.
Kwa ujumla waliohojiwa wamethibitika kuwa na makosa yafuatayo:-
1. Walithibitika kuanza kampeni za kutafuta kuteuliwa kugombea Urais kabla ya wakati kinyume na Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM Toleo la Februari 2010, Ibara 6(7)(i).
2. Wamethibitika kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya Chama na baadhi yao kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya jamii.  Kosa hili nalo ni kwa mujibu wa Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM Toleo la Februari 2010, Ibara kadhaa za kanuni hizo.


Kamati Kuu baada ya kuthibitisha makosa hayo imewapa watu wote sita waliohojiwa adhabu ya ONYO KALI na kuwataka wajiepushe na vitendo vinavyokiuka maadili na iwapo wataendelea na vitendo hivyo Chama kitawachukulia hatua kali zaidi.
Tafsiri ya adhabu ya ONYO KALI kwa mujibu wa Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM Toleo la Februari 2010, Ibara ya 8(ii) (b) ni:-
“Mwanachama aliyepewa adhabu ya ONYO KALI atakuwa katika hali ya kuchunguzwa kwa muda usiopungua miezi 12, ili kumsaidia katika jitihada zake za kujirekebisha.”
Kamati Kuu imeitaka pia Kamati Ndogo ya Udhibiti kuwachunguza na kuchukua hatua kwa wote waliohusika kwa namna moja au nyingine (mawakala na wapambe) kufanyika kwa vitendo hivyo vilivyovunja Kanuni za Chama.
Aidha, Kamati Kuu imewaonya vikali Viongozi na Watendaji wa Chama na kuwataka kujiepusha kujihusisha na matendo ya wanawania Urais yanayovunja na kukiuka maadili ya Chama, wametakiwa kuzingatia Kanuni na taratibu za Chama.

Imetolewa na:-

Nape Moses Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA,
ITIKADI NA UENEZI,
18/02/2014
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment