IMEELEZWA kuwa maswala mengi
yanayohusu ukatili wa Kijinsia yamekuwa yakifumbiwa macho na Serikali kwa
kushindwa kuwachukuliwa hatua wahusika pindi wanapobainika kutenda makosa hayo
hususani Jeshi la Polisi.
Hayo yalibainishwa mwishoni mwa
Wiki katika Mafunzo ya waandishi wa habari juu ya kuandika habari za
unyanyasaji wa kijinsia kwa Wanahabari wa Mikoa ya Rukwa na Katavi
yaliyoandaliwa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania(TAMWA) yaliyofanyika
katika ukumbi wa Hoteli ya Hollanda iliyopo mjini hapa.
Washiriki wa mafunzo hayo
walisema pamoja na kazi ya Wanahabari kufanya kazi kama TAMWA inavyotaka ya
kuibua matatizo ya ukatili wa kijinsia yanayofanyika vijijini lakini bado
taasisi zinazotakiwa kuchukua hatua zaidi hazifanyi hivyo jambo linalokwamisha
juhudi za waandishi wa habari.
Washiriki hao walitolea mfano
wa kesi nyingi zinazoripotiwa na vyombo vya habari na jeshi kuwakamata wahusika
na kuwaachia bila kutoa taarifa juu ya hatua zilizochukuliwa dhidi ya mhusika
na badala yake mtuhumiwa kuendelea kutamba mitaani akijidai kushindwa kwa
waliomshitaki.
Kwa upande wao wakufunzi wa
Semina hiyo, Jamilah Kilahama na Ibrahimu Bakari kutoka TAMWA Dar Es Salaam,
walisema moja ya sababu zinazofanya wahusika wa maswala ya unyanyasaji wa
kijinsia kushindwa kuchukuliwa hatua ni pamoja na kujuana baina ya watenda
makosa na Jeshi la polisi.
Waliongeza kuwa rushwa ni moja
ya sababu ya kushindwa kukomeshwa kwa ukatili wa kijinsia kutokana na wahusika
kutoa rushwa kwa vyombo vya dola pindi wanapo bainika kuhusika na uvunjifu wa
haki za binadamu hasa kumtendea ndivyo sivyo mtoto na Mwanamke kwa kuwa ndiyo
waathirika wakubwa wa unyanyasaji wa kijinsia.
Mbali na hilo walisema uoga
uliojengeka ndani ya jamii ya kushindwa kuwashtaki watu wanaowabaini kuwatendea
unyama watu wengine kwa kuhofia uhai wao kutoka kwa wahusika pamoja na kutengwa
katika jamii ni moja ya sababu zinazochangia kutokukomeshwa kwa ukatili wa
kijinsia.
Aidha washiriki wengi
walilitupia lawama jeshi la polisi kwa kuendelea kuyafumbia macho maswala ya
ukatili wa kijinsia ikiwa ni pamoja na wao kuendeleza ukatili huo kwa
kuwatendea ndivyo sivyo baadhi ya watuhumiwa wanaofikishwa katika Vituo vyao
wakitolea mfano Askari wa kiume kumpekua mtuhumiwa wa kike kuwa ni kinyume cha
Sheria na haki za binadamu.
Wawezeshaji wa Semina hiyo
walisema ni vema jamii ikaelewa Aina mbalimbali za ukatili wa Kijinsia kama
ulivyoainishwa katika Miongozo ya TAMWA ili iweze kuyaepuka na kuyatolea ufumbuzi
wa haraka pindi yanapotokea katika jamii zao.
Walizitaja aina hizo kuwa ni
pamoja na ukatili wa kihisia na kisaikolojia, Mila na Desturi potofu, Ukatili
wa Kimwili, Ukatili wa Kingono na ukatili wa kiuchumi ambao asilimia kubwa
humwathiri mtoto na Mwanamke ambapo takwimu zinaonesha katika kila wanawake
watano mmoja amepatwa na unyanyasaji na anatarajiwa kupata unyanyasaji wa
kijinsia.
Hata hivyo Chama cha Wanahabari
Wanawake Tanzania (TAMWA) kimejiwekea mpango mkakati wake wa miaka mitano
2000-2014, pamoja na mambo mengine kimepanga kufanya shughuli ambazo
zitaimarisha elimu kwa mtoto wa kike kwa kupunguza vitendo vya ukatili wa
kijinsia hasa vile vinavyoathiri wanawake na watoto. Vitendo hivyo ni pamoja na
ubakaji, kulazimisha watoto wa kike kukatisha masomo na kuolewa, ukeketaji na
familia kutelekeza watoto ambavyo kwa pamoja vinamnyima mtoto wa kike haki yake
ya msingi ya kupata elimu.
0 comments:
Post a Comment