SERIKALI KUANZISHA CHOMBO MAALUM CHAKUSIMAMIA AJIRA NA MASLAHI YA WAALIMU!! Unknown 11:13 Edit Serikali imeridhia kuanzisha chombo maalumu kitakachoshughulikia nidhamu na ajira za walimu, lengo likiwa ni kuondoa kero za muda mrefu zinazowakabili walimu nchini. Akizungumza katika Kipindi cha Maswali ya Papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu bungeni jana, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema Baraza la Mawaziri limeshatoa baraka zote za kuanzishwa kwa chombo hicho ambacho kitasimamia walimu tu, huku watumishi wengine wa Serikali wakiendelea kusimamiwa na Tume ya Utumishi wa Umma. “Sasa ni faraja kwa walimu maana juzi, tulikaa katika Baraza la Mawaziri na tumekubali kuanzisha chombo maalumu kitakachoshughulika na nidhamu na ajira za walimu, tunaamini masuala yao yote yatapatiwa ufumbuzi,” alisema Pinda. Waziri Pinda alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Igunga (CCM), Dk Dalali Kafumu aliyetaka kujua kero za walimu zitamalizwa lini, hasa kutokulipwa mishahara yao kwa wakati pamoja na madai yao mbalimbali. Mbunge huyo alitolea mfano tukio la hivi karibuni lililotokea katika Halmashauri ya Igunga ambako zaidi ya walimu 100 walimfungia ofisini Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Sisti Kessy kwa saa nne, wakishinikiza kulipwa mishahara yao ya Aprili na Mei mwaka huu. “Mpaka sasa walimu hawa hawajalipwa, ni lini Serikali itamaliza kero zinazowakabili walimu nchi nzima, wakiwemo wa wilayani Igunga,” alisema Dk Kafumu. Akijibu Pinda alisema: “Walimu ni asilimia zaidi ya 50 ya watumishi wote wa umma. Kwa muda mrefu wabunge wamekuwa wakilipigia kelele suala la walimu. Tumeanza taratibu za kuanzisha chombo hiki kitakachosimamia masuala ya walimu.” Alisema moja ya jambo linalosababisha walimu kuchelewa kulipwa stahiki zao mara tu wanapoajiriwa ni kukwepa kwenda katika maeneo ya kazi waliyopangiwa, badala yake wanakwenda kufundisha maeneo ambayo hawakupangiwa. Akizungumzia kuundwa kwa chombo hicho, Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Waalimu Tanzania (CWT), Ezekiel Oluoch alisema ikiwa Baraza la Mawaziri limeridhia hivyo itakuwa ni msaada mkubwa kwa walimu. “Sisi tulichokuwa tunakitaka ni Tume ya Utumishi wa Walimu ambayo itashughulikia masuala yote ya walimu, kama chombo alichosema Waziri Mkuu ndicho hicho basi tutashukuru,” alisema Oluoch. Hata hivyo, alitoa angalizo akieleza kuwa kama chombo hicho kitakuwa chini ya chombo kilichoelezwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa wakati wa bajeti yake ambacho ni Mamlaka ya Kudhibiti Masuala yote ya Shule za Msingi, hakitakuwa na msaada kwa walimu. Oluoch alisema watashukuru chombo hicho kikiwa ni Tume ya Utumishi wa Walimu ili kiweze kusimamia kazi tano ambazo ni kuajiri, kulipa mishahara, kuangalia mahitaji ya walimu, kufukuza walimu na kuwapandisha madaraja. “Kikiwa na uwezo huo wa kushughulikia pia uhamisho, likizo na mengine kitakuwa na manufaa mazuri kwa walimu,” alisema Oluoch. Share on Facebook Share on Twitter Share on Google Plus About Unknown This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel. RELATED POSTS
0 comments:
Post a Comment