Mwenyekiti wa Bunge maalum la Katiba Mh.Samweli Sitta |
Wakati Bunge Maalumu la Katiba
likiazimia kuzifanyia marekebisho kanuni zake ili kuwabana wajumbe wa Bunge
hilo ambao ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), viongozi wa
kundi hilo wamesema hawatishwi na uamuzi huo na kwamba wataendelea kususia
vikao hivyo.
Kikao kilichokuwa kiwe cha mashauriano kilichoitishwa juzi na
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta kiliazimia kuzifanya marekebisho
baadhi kanuni za uendeshaji kwa lengo la kusimamia nidhamu wajumbe wake, hatua
inayotafsiriwa kwamba inawalenga Ukawa.
Jana Sitta akizungumza na Mwananchi Jumamosi alisema mabadiliko
yanayokusudiwa kufanywa yatahusisha masuala ya nidhamu, yakiwamo fujo na utoro,
mambo ambayo hivi sasa hayawezi kudhibitiwa moja kwa moja na mwenyekiti wa
Bunge hilo.
Sitta alikuwa akitoa ufafanuzi wa taarifa iliyotolewa na ofisi
yake jana na kusomwa mbele ya waandishi wa habari na Katibu wa Bunge Maalumu,
Yahya Khamis Hamad, ikieleza maazimio ya kikao ya usuluhishi alichokuwa
amekiitisha kwa ajili ya kutanzua mzozo unaotishia kukwama kwa mchakato wa
Katiba Mpya.
Hata hivyo, Ukawa unaoundwa na wajumbe wa Bunge Maalumu kutoka
Vyama vya Chadema, NCCR Mageuzi, CUF na baadhi ya wajumbe kutoka Kundi la 201
walioteuliwa na Rais, walisusia kikao hicho na kusababisha uamuzi uliofikiwa
kuwa wa upande mmoja.
Hata hivyo, wakizungumza na chanzo hiki jana kwa nyakati
tofauti, viongozi wa Ukawa ambao ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na
yule CUF, Profesa Ibrahim Lipumba walisema hawatishwi na mabadiliko ya kanuni
yanayokusudiwa kufanywa na kwamba wataendelea kususia vikao hivyo hadi hoja zao
zitakapozingatiwa.
Ukawa walitoka bungeni siku chache kabla ya kuahirishwa kwa
awamu ya kwanza ya Bunge Maalumu mwezi Aprili mwaka huu, kwa madai kwamba Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kinatumia wingi wa wajumbe wake kutaka kufutwa kwa baadhi
ya mapendekezo ya wananchi yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba.
Kauli ya Sitta
Sitta aliliambia gazeti hili kuwa moja ya kasoro katika
uendeshaji wa Bunge ni pale makundi kama Ukawa na Tanzania Kwanza
yanapotambuliwa kama makundi rasmi ya Bunge Maalumu, wakati makundi rasmi ni
wabunge, wawakilishi na Kundi la Wajumbe 201 wa kuteuliwa na Rais.
“Bunge hili lina uhuru wa ajabu ambao ni mkubwa kuliko Bunge
jingine lolote, Bunge ambalo hata uongozi wake hauwezi kumchukulia mtu hatua
kwa utovu wa nidhamu eti mpaka umuone mtu anafanya makosa, umpeleke kwenye
Kamati ya Kanuni na hivyo ndiyo inakuwa imekwisha maana kama ana watetezi wake
wanamtetea,” alisema Sitta na kuongeza:
“Matokeo yake wananchi wanalalamika kwamba hakuna nidhamu
bungeni na kwamba kiti kimeshindwa kuchukua hatua, sasa unachukuaje hatua
wakati kanuni zetu ndivyo zilivyo?”
Aliendelea: “Yako mambo mengi yanapaswa kufanyika na tuna siku
63 tu za kukamilisha kazi tuliyopewa sasa hatuwezi kutumia fedha za umma na
watu wengine wanafanya mzaha, leo huyu anachukua posho, mara anaondoka, haya
mambo lazima yatafutiwe dawa.”
Source:Mwananchi.
0 comments:
Post a Comment