Katika matokeo hayo, Shule ya Sekondari ya
Kaizirege ya mkoani Kagera, iliyoanzishwa mwaka 2010, ndiyo imekuwa
kinara ikiwa ni mwendelezo wa mafanikio baada ya mwaka jana kushika
nafasi hiyo lakini kwa upande wa shule zenye watahiniwa chini ya 40.
Shule iliyoshika mkia ni Manolo iliyopo Tanga, mkoa ambao umetoa shule
tano miongoni mwa shule zilizoshika nafasi 10 za mwisho.
Matokeo hayo ni ya kwanza tangu kuanza kutumika
kwa mfumo mpya wa upangaji wa Wastani kwa Kutumia Pointi (GPA) ambao
unaonyesha shule zote 10 za kwanza ni za binafsi.
Akitangaza matokeo hayo jana jijini Dar es Salaam,
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Dk Charles
Msonde alisema waliofaulu mtihani huo ni wanafunzi 196,805 sawa na
asilimia 68.33 ya watahiniwa 288,247 waliofanya mtihani huo,
ikilinganishwa na 235,227, sawa na asilimia 58.25 ya waliofaulu mwaka
2013.
Dk Msonde alisema wavulana waliofaulu ni 106,960 sawa na asilimia 69.85 na wasichana ni 89,845 sawa na asilimia 66.61.
Kwa mujibu wa maelekezo ya BRN, ufaulu wa upande wa sekta ya elimu, ambayo ilipangiwa malengo tisa, ulipaswa uwe asilimia 70.
Hata hivyo, pamoja na kuwa chini kidogo ( asilimia
1.7) kufikia wastani wa ufaulu kitaifa, Msonde alisema: “Tumejitahidi
kwani ni asilimia kama moja na ushee ilibaki, walimu walifanya kazi
nzuri na nina imani tutaifikia.”
Alisema watahiniwa 297,365 waliandikishwa kufanya
mtihani huo wakiwamo wasichana 139,400 sawa na asilimia 46.88 na
wavulana 157965 sawa na asilimia 53.12. Watahiniwa wa shule walikuwa
244,902 ikilinganishwa na watahiniwa 367,163 walioandikishwa kufanya
mtihani huo mwaka 2013.
“Idadi ya watahiniwa wa shule walioandikishwa
kufanya mtihani huo ilipungua kwa asilimia 33.3 ikilinganishwa na
watahiniwa walioandikishwa mwaka 2013.”
“Mwaka 2012 kati ya watahiniwa 386,355 waliofanya
mtihani wa kidato cha pili, watahiniwa 136,243 walirudia kidato cha pili
na watahiniwa 250,112 waliendelea na kidato cha tatu ambao ndiyo
waliosajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2014,” alisema na
kuongeza:
“Kati ya watahiniwa 297,365 waliosajiliwa kufanya
mtihani wa kidato cha nne 2014, watahiniwa 288,247 sawa na asilimia
96.93 walifanya mtihani na watahiniwa 9,118 sawa na asilimia 3.07
hawakufanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali.”
Alisema watahiniwa wa shule, kati ya watahiniwa
244,902 waliosajiliwa watahiniwa 244,410 sawa na asilimia 98.17
walifanya mtihani ambao wasichana walikuwa ni 110,603 sawa na asilimia
98.13 na wavulana ni 129,807 sawa na asilimia 98.19. Watahiniwa 4,492
sawa na asilimia 1.83 hawakufanya mtihani.
Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea, alisema kati ya
watahiniwa 52,463 waliosajiliwa, 47,837 ambao ni sawa na asilimia 91.18,
walifanya mtihani na ambao hawakufanya ni 4,626 sawa na asilimia 8.82.
Ufaulu wa masomo
Dk Msonde alisema ufaulu wa watahiniwa wa shule
katika masomo ya msingi umepanda kati ya asilimia 1.28 na 11.22
ikilinganishwa na mwaka 2013.
“Ufaulu wa juu kabisa ni ule wa somo la Kiswahili
na asilimia 69.66 ya watahiniwa wote wa shule waliofanya somo hili
wamefaulu na ufaulu wa chini kabisa ni ule wa somo la hisabati ambalo
asilimia 19.58 ya watahiniwa wote waliofanya somo hili wamefaulu.”
“Ufaulu katika masomo ya sayansi yaani fizikia,
kemia na baiolojia umeendelea kuimarika kidogo kwa kulingana na ufaulu
wa masomo hayo mwaka 2013,” alisema.
Katika matokeo hayo, ufaulu wa kila somo na
asilimia katika mabano ni Kiswahili (69.66), kemia (56.73), Kiingereza
(55.10), baiolojia (48.30), fizikia (46.71), jiografia (37.96), uraia
(37.70), historia (37.41), biashara (34.29), uhasibu (42.20) na hisabati
(19.58).
Matokeo yaliyozuiwa, kufutwa
Dk Msonde alisema baraza limefuta matokeo ya
watahiniwa 184 waliobainika kufanya udanganyifu. Kati ya watahiniwa
waliobainika kufanya udanganyifu, 128 ni wa kujitegemea na 56 ni
watahiniwa wa shule.
Alisema kati ya watahiniwa hao, 128 wanatoka vituo
viwili vya Kisesa mkoani Mwanza na Ubago visiwani Zanzibar, huku
wengine 56 wakitoka shule mbalimbali.
“Tumeagiza mamlaka husika kuwachukulia hatua za
kinidhamu waliohusika katika vituo hivyo vya Kisesa na Ubago kwani
udanganyifu uliofanyika ni karatasi moja ya kujibia mtihani imeandikwa
na watu watatu tofauti jambo ambalo linaonyesha hakukuwa na umakini,”
alisema.
Shule kongwe na za vipaji hoi
Shule za vipaji kama Ilboru, Mzumbe, Msalato,
Kilakala, Tabora Boys, Kibaha na Tabora Girls na Shule kongwe
zinazomilikiwa na Serikali kama Pugu, Zanaki, Bwiru Boys, Minaki, Azania
na Jangwani, kwa mara nyingine zimeshindwa kufua dafu kwa shule za
binafsi.
Katika orodha ya shule 10 bora shule binafsi zilizotamba katika
matokeo hayo ni Kaizirege (Kagera), Mwanza Alliance (Mwanza), Marian
Boys (Pwani), St. Francis Girls (Mbeya), Abbey (Mtwara), Feza Girls (Dar
es Salaam), Canossa (Dar es Salaam), Bethel Sabs Girls (Iringa), Marian
Girls (Pwani) na Feza Boys (Dar es Salaam).
Shule 10 za mwisho ni Manolo (Tanga), Chokocho
(Pemba), Kwaluguru (Tanga), Relini (Dar es Salaam), Mashindei (Tanga),
Njelekela Islamic Seminari (Kigoma), Vudee (Kilimanjaro), Mnazi (Tanga),
Ruhembe (Morogoro) na Magoma (Tanga).
Watahiniwa 10 bora kitaifa
Dk Msonde aliwataja wanafunzi 10 bora kitaifa kuwa
ni Nyakaho Marungu (Baobab), Elton Jacob (Feza Boys), Samwel Adam
(Marian Boys), Fainess Mwakisimba (St. Francis Girls), Mugisha Lukambuzi
(Bendel Memorial), Paul Jijimya (Marian Boys), Angel Mcharo (St.
Francis Girls), Atuganile Jimmy (Canossa), Jenifa Mcharo (St. Francis
Girls) na Mahmoud Bakili (Feza Boys).
Wasichana 10 bora kitaifa
Katika matokeo hayo mwanafunzi bora kwa wasichana
ni Nyakaho Marungu (Baobab), aliyefuatiwa na Fainess Mwakisisimba (St.
Francis Girls), Angel Mcharo (St. Francis Girls), Atuganile Jimmy
(Canossa), Jenifa Mcharo (St. Francis Girls), Levina Ndamugoba
(Msalato), Veronica Wambura (Canossa), Sifaely Mtaita (St Maris Mazinde
Juu), Catherine Ritte (St. Francis Girls) na Anastazia Kabelinde
(Kaizerege).
Wavulana 10 bora
Dk Msonde alimtangaza kinara kwa wavulana kuwa ni
Elton Jacob (Feza Boys) akifuatiwa na Samwel Adam (Marian Boys), Mugisha
Lukambuzi (Bendel Memorial), Paul Jijimya (Marian Boys), Mahmoud Bakili
(Feza Boys), Amani Andrea (Moshi Technical), Mahmoud Msangi, Elias
Kalembo, Haji Gonga na Kelvin Sessan wote kutoka Feza Boys.
0 comments:
Post a Comment