CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya maandamano ya kupinga vikao vya Bunge Maalamu la Katiba vinavyoendelea mjini Dodoma.
Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CC) kumuagiza Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, kurudi katika meza ya mazungumzo na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kunusuru mchakato wa Katiba mpya.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa Chadema, John Mnyika, alisema pamoja na CC kumtaka Kinana arudi katika meza ya mazungumzo na Ukawa wao wataendelea na maandalizi ya maandamano kwa kuwa bado vikao vya Bunge Maalumu vinaendelea.
Alisema Kamati Kuu ya CCM ilimaliza vikao vyake na imeeleza uamuzi waliofikia lakini haikutoa agizo la kutaka kusimamishwa Bunge Maalumu huku wajumbe waliopo bungeni ambao wengi ni wa chama hicho wakiendelea kuchukua posho.
“Kikao kile kiliongozwa na Rais Jakaya Kikwete ambaye ni mwenyekiti wao, sisi tulitegemea angeingilia kati na kutoa tamko la kutaka Spika Samweli Sitta kusimamisha Bunge hilo lakini wao wamemtuma Kinana kwenye mazungumzo huku Bunge likiendelea,”alisema
Alisema Rais Kikwete anayo mamlaka ya kuweza kusimamisha posho za wajumbe kwa kuzuia fedha kutoka Hazina hali itakayowanya wasiendelea na vikao hivyo.
“Mazungumzo yanaendelea nyuma ya pazia na mwafaka bado haujapatikana, lakini wakati mazungumzo hayo yanaendelea bado Bunge maalumu linaendelea kupitia kamati zake,
“Hivyo na sisi kwa upande wetu tunaendelea na mchakamchaka wa maandalizi ya maandamano nyuma ya pazia na tunawaambia watu wetu kujiandaa na kuwa tayari,” alisema na kuongeza:
“Haiwezekani sisi watuambie tutulie, tusubiri matokeo ya mazungumzo halafu wao wanaendelea na vikao, sasa kama wao wanaendelea na vikao vya kula posho sisi tunaendelea na maandalizi ya mchakamchaka wa maandamano na tayari tumeshatunga wimbo wa kuhamasisha katika maandamano hayo na tutawapa wanachama wetu.
“Sisi tunajiandaa na tuna imani na vyama vingine vinajiandaa ili endapo maridhiano hayo hayatapatikana tunaingia katika maandamano ambayo tarehe itatangaza muda ukifika.”
0 comments:
Post a Comment