HOJA NNE ZINAZOTIKISA BUNGE LA KATIBA!!




MAHAKAMA ya Kadhi, Uraia pacha, kiongozi wa umma kumiliki akaunti ya benki nje ya nchi na nafasi tatu za Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni hoja nne zinazotikisa mjadala wa Bunge Maalum la Katiba, uliyoanza jana.

Hoja hizo ambazo ziliibua msuguano mkali kuanzia kwenye Kamati za Bunge na hatimaye kukataliwa na maoni ya walio wengi, zimeonekana kuibua mgawanyiko wa wazi baina ya wajumbe.

Wakati Waislamu wakitaka Mahakama ya Kadhi itambulike kikatiba ili uamuzi unaotolewa na mahakama hiyo kuhusu migogoro ya ndoa na mirathi usikatiwe rufaa katika mahakama za serikali, wajumbe Wakristo wanakataa wakisema kufanya hivyo ni kukiuka misingi ya katiba inayotambua kuwa nchi haifungamani na dini yoyote.

Kuhusu uhuru wa imani ya dini, ibara ya 32.-(1) ya rasimu ya Katiba inapendekeza kuwa; kila mtu anao uhuru wa mawazo, imani na uchaguzi katika mambo ya imani ya dini na anao uhuru pia wa kubadili dini, imani yake au kutokuwa na imani na dini. Kifungu kidogo (3) ndicho kinabishaniwa, kwani pendekezo la rasimu ni kwamba; shuguli ya uendeshaji wa jumuiya za dini itakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya serikali.

Msuguano katika hoja hiyo ni kwamba, Waislamu wanataka mahakama itambulike kikatiba lakini uendeshaji wake watagharamia wao ila Wakristo wanaamini kuwa ikiwa jumuiya hizo zitagharamia uendeshaji wake, basi suala hilo halipaswi kuingizwa kwenye katiba.

Hoja ya uraia pacha nayo imetikisa Bunge kwa kiwango kikubwa, ambapo upande unaotaka uraia pacha unajenga hoja kwamba itakuwa ni fursa nzuri ya Watanzania waliyoko nje kurejea na kuwekeza katika kukuza uchumi.

Wanahoji kwamba kama raia wa kigeni wanapewa uraia wa Tanzania baada ya kuishi nchini kwa miaka kadhaa, iweje Watanzania waliozaliwa hapa wanyang’anywe uraia baada ya kwenda nje kusoma au kujikwamua kiuchumi halafu wakabadili uraia.

Hata hivyo, wajumbe wanaopinga hoja hiyo ya uraia pacha, wanawaona Watanzania waliokana uraia wa Tanzania na kuchukua wa nchi nyingine ni wasaliti, kwamba kuendelea kuwavumilia kama raia halali wa Tanzania wakati walishaukana ni kuwavunja moyo wale wazalendo.

Mapendekezo ya rasimu kuhusu uraia wa kuzaliwa, ibara ya 57.-(1) kila mtu aliyezaliwa Tanganyika au Zanzibar atakuwa raia wa kuzaliwa wa Jamhuri ya Muungano iwapo, wakati wa kuzaliwa, mama au baba yake alikuwa raia wa Jamhuri ya Muungano.

Ibara ya 59, mtu yeyote mwenye asili au nasaba ya Tanzania na ambaye ameacha kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano kwa kupata uraia wa nchi nyingine, atakapokuwa katika Jamhuri ya Muungano, atakuwa na hadhi kama itakavyoainishwa katika sheria za nchi.

Hoja nyingine iliyochangiwa na wajumbe wengi ni kuhusu ibara ya 16 (a) inayozuia kiongozi wa umma kutofungua au kumiliki akaunti ya benki nje ya Jamhuri ya Muungano isipokuwa tu kwa namna ambayo sheria za nchi zinaruhusu.

Baadhi ya wajumbe waliopata nafasi ya kuchangia jana, waligawanyika katika makundi mawili ambapo moja linaunga mkono pendekezo hilo la rasimu huku lingine likitaka waruhusiwe kuwa nazo ispokuwa waeleze fedha hizo walizipataje.

Ibara ya 90 (1) ambayo inatambua kuwepo kwa Makamu wa Rais ambaye atakuwa ndiye msaidizi mkuu wa Rais kuhusu mambo yote ya Jamhuri ya Muungano, nayo imeibua utata mkubwa kutokana na muundo wa muungano wa serikali mbili unaopendekezwa na walio wengi kukinzana na rasimu ya katiba.

Katika mapendekezo ya wajumbe walio wengi, inapendekezwa kuwepo kwa makamu wa rais watatu ambapo mgombea mwenza wa Rais ndiye atakuwa makamu wake wa kwanza, wa pili atakuwa Rais wa Zanzibar na Waziri Mkuu atakuwa makamu wa tatu wa Rais.

Hata hivyo, utata wa makamu hawa unajitokeza katika kukaimu nafasi ya Rais endapo yeye na makamu wake wa kwanza watakuwa hawapo, kwani Rais wa Zanzibar na Waziri Mkuu itakuwa vigumu kukaimu nafasi hiyo kwa sababu hawajachaguliwa na wananchi wa pande mbili za muungano.

Wanaotaka muundo huo wa serikali mbili, wanajenga hoja kwamba makamu wa kwanza wa Rais kutokuwa mgombea mwenza, inaweza kuleta mgongano iwapo Rais wa Jamhuri ya Muungano atatoka chama kingine, Rais wa Zanzibar pia akatoka chama kingine na Waziri mkuu akatoka chama tofauti.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment