Na Benedict Liwenga, Maelezo-Dodoma.
Katiba ni
‘Sheria Mama’ inayolinda haki za raia wote wakiwemo wanawake, wanaume na
watoto nchini na kuainisha mfumo wa kuendesha nchi na wajibu wa
viongozi wanaopewa dhamana ya kuongoza.
Hivyo, ni
vema Sheria hii Mama ikaheshimika na kila raia hasa pale inapokuwa
ikiandaliwa ama kutungwa ili kuweza kupata Katiba rafiki yenye kumjali
kila mwananchi kwa lengo la kudumisha maendeleo yenye tija katika taifa
letu.
Hivi
karibuni tumeshuhudia makundi mbalimbali yakiwasilisha nyongeza ya
mapendekezo yao ya ziada katika Bunge Maalum la Katiba si kweli kama
inavyodaiwa baadhi ya watu na vyombo vya habari, kuwa makundi hayo
yalikuyanawasilisha hoja mpya, bali makundi haya yamekuwa yakidai kuwa
baadhi ya mambo muhimu yalikuwa yamesahaulika au kutotiliwa mkazo wakati
wa kukusanya maoni.
Kazi
ambayo ilikuwa ikifanywa na Tume ya Marekebisho ya Katiba pindi
walipowasilisha hoja zao hapo awali, ndipo wanapotumia wasaa huo
kuwasilisha nyongeza ya mapendekezo hayo katika Bunge hilo.
Bila shaka
kwa kitendo hiko wafanyacho waungwana hawa toka makundi mbalimbali ya
wananchi si dhambi kwani wana nia nzuri ya kutaka kupata Katiba
iliyorafiki na yenye mrengo wa kijinsia ili iweze kuwalinda na kuwaletea
maendeleo katika taifa lao yaani Tanzania.
Mwenyekiti
wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samuel Sitta amekuwa akisisitiza juu ya
kazi yake anayoifanya katika Bunge hilo kuwa si kupokea hoja mpya na
sio kufanya kazi ya iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na ukweli huu
unajidhihirisha pale alipofanya mikutano na baadhi ya makundi
mbalimbali yaliyowahi kufika Bungeni hapo yakiwemo makundi ya Wasanii,
Wafugaji, Wavuvi, Walemavu pamoja na Umoja wa Azaki za Vijana ambayo
yaliwasilisha taarifa ya mapendekezo yao ikiwa ni nyongeza ya yale
waliyokwisha wahi kuyawasilisha hapo awali ili yapate kuongezewa katika
mchakato wa kusaka Katiba mpya.
Mwenyekiti
wa Bunge hilo, Mhe. Sitta wakati alipokutana na kundi la Shirikisho la
Vyama vya Watu wenye Ulemavu (SHIVYAWATA) alipata kutoa msisitizo wake
kuhusiana na kazi ya Bunge hilo, huku akisisitiza kuwa kazi wanayoifanya
ya kuyapokea makundi mbalimbali Bungeni hapo haina lengo la kuja na
hoja mpya na kuziwasilisha katika Bunge hilo, bali ni mawasiliano ya
kawaida yanayohusu safari kutoka Rasimu Mpya ya Katiba mpaka kufikia
katika Katiba Mpya inayopendekezwa ipatikane.
Kauli
ambayo amekuwa akiirudia mara kwa mara pindi anapokutana na makundi hayo
wakiwemo baadhi ya waandishi wa habari ambao wanaripoti habari za
Bunge hilo.
“Jambo
lolote lililoandikwa na binadamu halikosi kasoro, katika Rasimu hii ya
Katiba tumegundua inayomapungufu kadha wa kadha, kuna baadhi ya maoni
ambayo hayakuzingatiwa ndiyo maana tunayafanyia kazi ili yawemo katika
Katiba Mpya itakayopatikana,”.alisema Mhe. Sitta.
Katika
mchakato wa kusaka Katiba mpya, yatupasa kufahamu kuwa si Watanzania
wote wenye nia nzuri ya kufanikisha suala hili liendelee vema kama
ilivyopangwa, kwani kuna makundi mbalimbali wakiwemo watu binafsi wenye
kujawa na chuki na sababu zisizo na mashiko na wenye lengo la
kuwapotosha wananchi kuhusiana na mchakato huu wa kusaka Katiba mpya.
Na ndiyo
watu hawa tunapaswa tuwaelimisheili wapate kuelimika juu ya umuhimu wa
Katiba hiyo kwani kuipinga, kuisema vibaya, kuidharau ikiwemo kuisusia
pamoja na kudhalilisha wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wala hakuleti
muafaka wowote kwakuwa Katiba hii itamfaa kila aliye Mtanzania hata huyu
anayeipinga sasa kuwa mchakato wake usitishwe ama usiendelee.
Sambamba
na haya, mnamo tarehe 3 Septemba mwaka huu,wawakilishi wa Taasisi za
Dini wa Bunge Maalum la Katiba toka wajumbe 201 walitoa tamko lao dhidi
ya tuhuma mbalimbali zinazoendelea katika kulichafua Bunge hilo, ikiwemo
baadhi ya wajumbe wa kundi hilo wakituhumiwa kudaiwa kupewa rushwa.
Katika
mkutano wao huo, tamko hilo lilitolewa na viongozi wa kiroho akiwemo
Askofu wa Kikristo Amos Joseph Muhagachi pamoja na Sheikh Hamid Masoud
Jongo wakiwa wameongozana na Mwenyekiti wa kundi hilo la 201, Mhe. Dkt.
Francis Michael na wajumbe wengine wa kundi hilo, wakati walipofanya
mkutano na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa Spika uliopo Bungeni
mjini Dodoma.
Akisoma
tamko hilo, Askofu Amos Muhagachi ambaye pia ni Mjumbe wa kundi hilo
alisema kuwa kama ilivyoelezwa hapo awali kabla ya kuanza kwa shughuli
za Bunge hilo, kila mjumbe alikula kiapo cha kuwa mwaminifu na mtiifu
kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa kadiri ya uwezo wake na
ufahamu wake, kufanya kazi zinazomhusu bila upendeleo.
Askofu
Muhagachi alieendelea kusema kuwa wameshangazwa na kusikitishwa kuona
kwamba mchakato wa kutayarisha Katiba itakayopendekezwa na Bunge hilo
kwa wananchi unachafuliwa taswira yake, Bunge Maalum la Katiba
linachafuliwa, shughuli zake kuingiliwa na kupotoshwa na wajumbe wenzao
walioko nje ya Bunge hilo, makundi, taasisi na vyombo mbalimbali vya
habari.
Aliongeza kwamba, uhalali na ukweli wa shughuli za Bunge hilo unapotoshwa na wananchi wanaaminishwa mambo yasiyo na ukweli.
“Upotoshwaji huu umezua mijadala mbalimbali katika jamii ya Watanzania nabado unaendelezwa”, alisema Muhagachi.
Aidha, Askofu Muhagachi alizitaja baadhi ya tuhuma zinazotolewa na wajumbe wenzao dhidi ya Bunge hilo zikiwemo;-
“Bunge
Maalum la Katiba halina uhalali kwa kuwa hao wajumbe wenzetu walioondoka
wameliondolea uhalali wake kwa vile hawapo, kwamba Kanuni za Bunge
Maalum la Katiba zinavunjwa ovyo ovyo, Kwamba kinachojadiliwa sasa
katika Bunge hili ni Waraka mwingine na si Rasimu iliyotayarishwa na
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Inadaiwa na watu pamoja na Taasisi
mbalimbali kwamba viongozi wa dini, wajumbe wa Bunge hilo na wajumbe wa
kundi la 201 kwamba wanapewa rushwa baadhi ya Vyombo vya Habari
vimeandika tuhuma hizi, pia madai mengine ni kwamba wajumbe waliomo
katika Bunge hili ni wachache ikilinganishwa na hao waliopo nje ya Bunge
na tuhuma ya nyingine ni ile ya kwamba Bunge hili lazima lisitishwe au
livunjwe na Mhe. Rais.
“Tunapenda
kuwafahamisha Watanzania wenzetu kwamba mchakato wa Katiba una hatua
tatu kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na mpaka hivi sasa ni
hatua moja iliyokamilika, aidha hatua ya pili ndiyo inayoendelea na
hatua ya tatu bado haijaanza”, alisema Muhagachi.
Alisema idadi ya wajumbe wanaohudhuri Bunge hilo, wako zaidi ya robo tatu kati ya wajumbe wote walioteuliwa.
Akitoa
tamko hilo, Askofu Muhagachi alisema kuwa wao kama wawakilishi wa
Taasisi za Dini, ambao kuuhubiri, kuutangaza na kuusimamia ukweli ni
moja ya majukumu yao katika jamii, hivyo wameskitishwa na taarifa potofu
zinazosambazwa kwa makusudi na makundi, taasisi na baadhi ya vyombo vya
habari.
“Tukiwa
kama wajumbe wa Bunge hili ambao tunafahamu kwa kina na tunaridhika na
kila hatua ya mchakato huu, tuna wajibu wa kusahihisha upotofu huu
unaoendeshwa kwa makusudi na hivi kuwaeleza Watanzania ukweli na hali
halisi inayojiri hapa Bungeni, Watanzania msifadhaishwe na wala
msibabaishwe, hali ni shwari, mchakato unaendelea kwa amani na
utulivu”, alisisitiza Muhagachi.
Katika
mkutano wao huo naye Sheikh Hamid Masoud Jongo aliviasa vyombo vya
habari kutilia mkazo katika kutoa taarifa zilizosahihi ili mchakato wa
Katiba uendelee kwa amani kwani nao ni moja ya kundi la watu
inayowahusu.
“Vyombo
vya habari vina nguvu ya kuhabarisha umma juu ya mambo mengi
yanayoendelea nchini, ni vema tukishirikiana sote kwa pamoja ili
kuhakikisha kuwa tunapata Katiba yetu kwani hata nyie Katiba hii
inawahusu hasa katika kudai haki na uhuru wa vyombo vya habari”, alisema Sheikh Jongo.
Pia
Mwenyekiti wa wajumbe wa Kundi hilo la 201, Mhe. Dkt. Francis Michael
aliongezea kwa kukanusha suala la rushwa kwa wajumbe wake huku
akisisitiza kuwa wajumbe wake katika kundi hilo ni watu wenye heshima
zao hivyo madai hayo hayakuwa na ukweli wowote.
Watanzania
hatunabudi kulibariki na kuliheshimu Bunge Maalum la Katiba pamoja na
kazi zake na viongozi wake, na pia ni vema sasa kila mmoja kutokana na
imani ya dini yake kwa wakati wake kuiombea kwa Mwenyezi Mungu ili aweze
kuepusha ubaya wowote ambao unaweza kuikosesha haki ya Watanzania wote
ya kupata Katiba Mpya iliyo bora, pia yatupasa kuwa makini dhidi ya watu
wasiolitakia mema Bunge hili huku wakisahau kuwa wao pia ni miongoni
mwa watu watakaonufaika na Katiba hiyo na hata vizazi vyao vya baadaye.
Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania.
0 comments:
Post a Comment