UJENZI STENDI YA MABASI MBEZI LUIS NI NDOTO?


Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi
Uhamishaji wa Stendi ya Mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani ya Ubungo (UBT) unaonekana kuwa ni ndoto kutokana na kutokuwapo dalili.
Hali hiyo inatokana na kutokuwapo kwa dalili zozote za ujenzi katika eneo la Mbezi Luis huku yakijengwa majengo mapya ya kisasa katika kituo hicho karibu na ofisi za Shirika la Viwango Tanzania (BTS).

Wakati hali ikiwa hivyo, Jiji la Dar es Salaam lilishatoa tamko kwamba ujenzi huo ungeanza wakati wowote bila kujali hukumu ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kitengo cha Ardhi kuwapa ushindi wakazi wa Mbezi Luis ambao walifungua kesi wakidai kuwa kiwanja cha ujenzi wa stendi hiyo ni eneo lao halali, hivyo kabla ya utekelezaji wa mradi huo wanapaswa kulipwa fidia.

Machi mwaka huu, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi, aliliambia NIPASHE kuwa walikuwa wanaendelea na mchakato wa kuandaa michoro kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho kipya ambacho  kinakadiriwa kugharimu Sh. bilioni sita katika hatua za awali.

Licha ya wakazi hao kudai kuwa ni eneo lao na kwamba hawatapisha ujenzi wa stendi hiyo hadi walipwe fidia kutokana na hukumu ya mahakama, Dk. Masaburi alisema Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ndiyo mmiliki halali wa maeneo hayo na hivyo wanaendelea na mchakato wa kuandaa michoro kwa ajili ya ujenzi.

Hata hivyo, Dk. Masaburi alipotafutwa ili kueleza maandalizi ya ujenzi huo, alisema yupo safarini na kuelekeza atafutwe Mkurugenzi wa jiji hilo,  Willison Kabwe.

Hata hivyo, tangu wiki iliyopita, Kabwe hakupatikana kutokana na kuelezwa kwamba alikuwa katika vikao.

UBT ambacho kimekuwa Ubungo toka miaka ya katikati ya tisini kinatakiwa kuhamishiwa Mbezi Luis kutokana na sehemu kubwa ya eneo lake kumegwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya mradi wa mabasi yaendayo kasi (Dart) hivyo  kubakiwa na eneo dogo lisilokidhi mahitaji.

Mwaka jana wakazi hao walishinda kesi namba 80 ya mwaka 2005 iliyofunguliwa na Proches Eleza Tarimo na wenzake 72, dhidi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mahakama ilitambua kuwa wanamiliki maeneo yao kihalali na kuzitaka  mamlaka zote za serikali zinazotaka kuchukua maeneo hayo kuwalipa kwanza fidia wamiliki wake halali kulingana na sheria ya vijiji ya mwaka 1999.

Masaburi alisema ujenzi wa kituo hicho hautazuiliwa na mtu yeyote, kwa sababu eneo panapojengwa kituo hicho ni mali ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na kuwa lina hati ya Jiji, hivyo mwingiliano na eneo la makazi ya wananchi kwa kuwa  eneo hilo ni kubwa.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment