Zitto (37), ambaye alikuwa naibu katibu mkuu wa
Chadema, alisema kuwa hata kuvuliwa nyadhifa zake ndani ya chama
kulisababishwa na wapambe hao, lakini akasisitiza kuwa hana kinyongo
tena kwa kuwa alishamwomba Mungu na sasa amesamehe kabisa.
Tofauti za wawili hao hazijawahi kutolewa
hadharani licha ya mitandao mbalimbali kuzungumzia kuharibika kwa
uhusiano wao ikinukuu habari kutoka vikao vya ndani vya Chadema.
Hata hivyo, mapema mwaka huu, Zitto alirushiwa
tuhuma nzito na Chadema kutokana na uhusiano wake na baadhi ya makada wa
CCM, lakini mbunge huyo aliyahusisha maneno hayo na mwenyekiti wake na
aliandika maneno makali dhidi ya Mbowe kwenye ukurasa wake wa facebook.
Lakini katika mahojiano na Mwananchi yaliyofanyika
wiki iliyopita nyumbani kwake Masaki jijini Dar es Salaam, Zitto
alionekana kujutia kuharibika huko kwa uhusiano wao na kusema “wapambe
ndiyo wanatugombanisha”.
“Sina shida yoyote na Mbowe, naamini ipo siku
tutagundua wapambe walituathiri na ndiyo waliotufikisha hapa,”
alisisitiza Zitto bila kutaja ni kina nani hasa.
Zitto alisema yeye na Mbowe wametoka mbali tangu
akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na hafurahii uhusiano wao ukiishia
katika hali hiyo.
“Naumia sana, lakini naamini ipo siku ama nikiwa
hai au nimekufa watu wataujua ukweli,” alisema mwanasiasa huyo kijana
aliyepata umaarufu kutokana na uwezo wake wa kujenga hoja.
Alisema, akiwa mwenyekiti wa Serikali ya wanafunzi
wa Chuo Kikuu (Daruso) yeye na mwenyekiti wake ndiyo waliokijenga chama
wakati huo Mbowe akiwa mbunge wa Hai.
Alisema wakati huo Mbowe alikuwa akienda chumbani
kwake kusuka mikakati ya kuiinua Chadema na kwamba walikuwa wakila chips
pamoja na wakati mwingine kwenye klabu ya usiku ya Bilicanas
inayomilikiwa na Mbowe.
“Wakati mwingine naangalia, naumia sana. Wakati
tunafanya hayo yote wengine walikuwa CCM, wengine walikuwa
wafanyabiashara, lakini sasa ndiyo wana sauti katika chama,” alisema
Zitto.
Zitto alisema kuwa wakati huo walikuwa na kampeni
yao waliyoiita ‘Real Madrid’ ambayo ilikuwa na lengo la kuingiza kila
mwanasiasa bora katika chama chao.
0 comments:
Post a Comment