LAAC waitupia lawama TAMISEMI.

Naibu waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Aggrey Mwanri (kulia) akiwa na Naibu waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Lucy Nkya (katikati),kwenye Vikao vya Bunge mjini DODOMA. Picha na Maktaba.

 KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), imeitupia lawama Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) kwa kushindwa kusimamia vizuri Halmashauri mbalimbali ikiwemo ya Kasulu, mkoani Kigoma.

Uongozi wa halmashauri hiyo ulikutana na LAAC Dar es Salaam jana ili kukaguliwa hesabu zao za mwaka 2012/13, kupitia utekelezaji wa maagizo waliyopewa na Serikali ambayo iliitaka halmashauri hiyo itoe asilimia 10 za mapato yao ya ndani ambayo ni asilimia tano kwa wanawake, tano za vijana na asilimia 20 kwa maendeleo ya vijiji.

Utekelezwaji wa maagizo hayo ulizua maswali mengi kutoka kwa wabunge na kuitupia lawama TAMISEMI.

Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Bw. Mbarouk Mohammed, ilibaini sh.milioni 239 hazikutumika kwa malengo yaliyokusudiwa na Serikali hivyo kamati ilihoji zilipo fedha hizo na halmashauri kushindwa kutoa majibu ya kuridhisha.

Bw. Mohammed alisema mwaka 2012/13, Serikali imekuwa ikitoa fedha katika halmashauri ili zipelekwe vijijini kwa ajili ya mikopo kwa wanawake asilimia tano na vijana asilimia tano ili waweze kutekeleza miradi mbalimbali ya kuwaingizia kipato jambo ambalo halmashauri hiyo imefanya kinyume.

Kwa upande wake, mjumbe wa kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Mwibala, Bw. Kangi Lugola, alisema halmashauri nyingi zimekuwa zikifanya makosa ya aina hiyo kwa kushindwa kutekeleza maagizo ya Serikali na kudai wa kulaumiwa ni TAMISEMI ambayo inaonekana kushindwa kusimamia ipasavyo halmashauri hizo.

"Inawezekanaje Serikali itoe fedha za kusaidia wanawake na vijana vijijini lakini halmashauri hazitekelezi, jambo hili inabidi TAMISEMI ilaumiwe kwani wao ndiyo wameshindwa kusimamia vizuri halmashauri zao.

"Halmashauri zote matatizo yao yanafanana, kutotekelezwa kwa maagizo ya Serikali, hali hiyo inachangia wanawake wengi kufanya biashara haramu ya kuuza miili yao na vijana kuunda makundi ya kihalifu," alisema.

Kamati ilikataa kujadili hesabu za halmashauri hiyo na kudai watalipeleka suala hilo bungeni liweze kujadiliwa kwa kina ili kupatiwa ufumbuzi.

Pia kamati hiyo ilitoa miezi mitatu kwa halmashauri hiyo ipitie vizuri vitabu vyao, kufanya marekebisho na wakimaliza wakabidhi hesabu hizo kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ili ziweze kuwasilishwa kwenye kamati.

Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment