Kamanda mkuu wa kundi la waasi la
LRA nchini Uganda Dominic Ongwen amewasili mjini Hague ambako
atafunguliwa mashitaka ya uhalifu wa kivita.
Uganda ilikubali kwamba muasi huyo apelekwe katika mahakama ya kimataifa ya ICC, licha ya nchi hiyo kuwa mkosoaji mkubwa wa mahakama hiyo.
Wanajeshi wa Marekani wakishirikiana na wanajeshi wa Afrika, wamekuwa wakifanya msako dhidi ya Ongwen tangu mwaka 2011.
Aidha mahakama ya ICC ilisema kwamba Ongwen atazuiliwa katika kituo kimoja nchini Uholanzi hadi mahakama itakapokuwa tayari kusikiliza kesi yake.
Hatahivyo Ongwen alitarajiwa kufanyiwa uchunguzi wa kiafya alipowasili Hague huku tarehe ya kusikilizwa kwa kesi yake ikisubiriwa.
Aidha Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na katibu mkuu wa umoja huo imepongeza hatua ya kumpeleka Ongwen mjini Hague.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Jen Psaki pia amepongeza hatua ya kukamatwa kwa muasi huyo akisema inatia matumaini makubwa kwa waathiriwa wa uasi wa kundi la LRA.
Tunawataka waasi wengine wa kundi la LRA waliosalia kufuata nyayo za Ongwen na wapiganaji wengine wa kundi hilo waliojisalimisha tangu mwaka 2012, kusalimisha silaha zao na kurejea nyumbani "alisema.
Aidha inasemekana kuwa Marekani sio mwanachama wa mkataba wa Roma uliosaidia kuundwa kwa mahakama ya ICC lakini licha ya hilo, ilisaidia katika kumkabidhi muasi huyo kwa ICC.
Awali Marekani ilitoa ahadi ya zawadi ya dola milioni 5 kwa yeyote ambaye angetoa taarifa kumhusu Ongwen na kupelekea kukamatwa kwake.
Muasi huyo anatuhumiwa kwa madai ya uhalifu wa kivita dhidi ya binadamu ikiwemo kutumia waathiriwa kama watumwa.
Uasi wa LRA ulianza zaidi ya miaka 20 iliyopita kaskazini mwa Uganda na inakisiwa kati ya wapiganaji 200-500 wameteswa na waasi wa kundi hilo nchini DRC, katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati.
Chanzo:BBC
0 comments:
Post a Comment