MADIWANI MOSHI WAMJIA JUU MKURUGENZI ATUHUMIWA KUPORA ENEO LA UWANJA!!

Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi Bw. Shaaban Ntarambe.


SAKATA la kiwanja kilichopo Kata ya Mawenzi Manispaa ya Moshi, chenye L.O.Na. 9850, limechukua sura mpya, baada ya kikao cha Baraza la Madiwani la Manispaa hiyo kuvunjika, wakimtuhumu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Shaaban Ntarambe, kuhusika na uporaji wa eneo hilo.

Kikao hicho cha Baraza kilichoanza saa 4:30 asubuhi,kilifunguliwa kwa sala; na Mkurugenzi kumkaribisha Mstahiki Meya kufungua kikao, ndipo diwani wa Kata ya Rau, Peter Kimaro, aliposimama na kuomba kutoa hoja.

Akitoa hoja, Kimaro alisema moja ya majukumu ya madiwani ni kulinda na kutetea mali za wananchi ikiwemo viwanja; na taarifa walizonazo, ni kwamba Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, ameshiriki uporaji wa kiwanja cha kata ya Mawenzi na kwamba ameondoa kwa siri zuio lililowekwa na baraza hilo bila madiwani kushirikishwa.

“Mkurugenzi amedharau agizo la baraza na kuagiza wataalamu wake kutengeneza kwa siri,hati ya kiwanja hicho kwa watu binafsi," alisema.

Kimaro aliongeza kuwa ni muhimu kukaundwa timu itakayohusisha watendaji wa Halmashauri na madiwani, ili kuchunguza sakata hilo na kulipatia ufumbuzi, ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua wale wote ambao walihusika katika kukihujumu kiwanja hicho.

Baada ya kauli hiyo ya Kimaro baadhi ya madiwani walisimama na kuanza kupiga kelele, huku wakitamka kuwa; "Tutoke hatumtaki mkurugenzi huyu... anahujumu mali za umma."

Wakati madiwani hao wakitoa maneno hayo walikuwa wakitoka nje na kuwaacha Watendaji, baadhi ya madiwani wa CCM pamoja na Meya ambaye ni mwenyekiti wa Kikao na Mkurugenzi ambaye ni katibu.

Hali hiyo ilisababisha kikao hicho cha bajeti kuvunjika, huku mkurugenzi wa Halmashauri akilalamikia kuvunjwa kwa kanuni na sheria za uendeshaji wa vikao vya baraza la madiwani, jambo ambalo lilipingwa vikali na mwenyekiti wa kikao hicho, Jaffari Michael, kwa madai kuwa kikao hicho kilikuwa hakijafunguliwa.

Akizungumza mara baada ya kuvunjika kwa kikao hicho Mstahiki Meya wa halmashauri hiyo, Michael, alisema kuna hoja ya msingi iliyosababisha madiwani kuvunja kikao hicho,kutokana na kwamba wapo kwa masilahi ya wananchi.

Meya alisema anaungana na madiwani wenzake kuamua kususia kikao hicho kutokana na kuwepo kwa tatizo la kupuuzwa maazimio mengi ambayo yamekuwa yakipitishwa na baraza la madiwani na ofisi ya Mkurugenzi, jambo ambalo wanaona ni dharau.

“Kuna hujuma dhidi ya kiwanja hicho, kwani haiwezekani hatimiliki ya eneo hilo ikamilike ndani ya wiki moja, huku Mkurugenzi akienda kwa siri kwenda kuondoa zuio lililowekwa na baraza la madiwani bila kurudi kutushirikisha, hali hii inatufanya tuamini kuwa, kuna mazingira ya rushwa katika sakata hili,” alisema Meya.

Mstahiki Meya alisema, amefanya jitihada mbalimbali kushughulikia sakata hilo bila mafanikio, hivyo kuviomba vyombo husika kuingilia suala hilo na kufanya uchunguzi ili kuweza kulipatia ufumbuzi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji katika Halmashauri hiyo,Raymond Mboya, alikiri kamati hiyo kutoshirikishwa, katika mchakato wa utoaji hati ya kiwanja hicho, jambo ambalo ni kinyume cha sheria za mipango miji.

Alisema kiwanja hicho kiliwahi kuvamiwa na kujengwa, lakini baraza la madiwani liliagiza pavunjwe, agizo ambalo lilitekelezwa na mkurugenzi,hivyo hawako tayari kuona tena eneo hilo likivamiwa.

Hata hivyo, mkurugenzi wa Manispaa hiyo alipofuatwa na waandishi wa habari ofisini kwake ili kutoa ufafanuzi kuhusiana na sakata hilo, aligoma na kuomba wanahabari kuonana naye leo kwa kuwa ameitwa kwenye kikao na mkuu wa mkoa huo.

Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment