Rais Jakaya Mrisho Kikwete (Picha na Maktaba) |
Ajenda hizo kwa mujibu wa wadau wa kada mbalimbali
waliongelea kuhusu vipaumbele vya taifa kwa sasa, ni tatizo
la ajira, changamoto za kuinua kilimo, kutoa elimu bora, kusimamia
makusanyo ya kodi, rasilimali za taifa na kuboresha miundombinu ya
usafiri.
Wagombea hao pia watatakiwa kueleza jinsi
watakavyoondoa migogoro ya wakulima na wafugaji, matumizi sahihi ya
ardhi, mapambano dhidi ya rushwa, uhalifu na matumizi ya dawa za
kulevya, kwa mujibu wa marejeo ya habari mbalimbali yaliyofanywa na wachunguzi wetu.
Kwa kawaida, vyama vya siasa huandaa ilani zake za
uchaguzi ambazo ndiyo mwongozo wa kampeni za kutafuta kura kwa wananchi
kwa ajili ya wagombea wake wa urais, ubunge na udiwani, lakini
watatakiwa kuzingatia hoja hizo muhimu.
Katika mahojiano na wadau mbalimbali, gazeti la
Mwananchi lilitaka kujua ni mambo gani ambayo wananchi “wanataka yawe
ajenda kuu kwenye kampeni za uchaguzi ili kuikwamua nchi” kutoka hapa
ilipo, na majibu yao yalionyesha suala la ajira, kilimo, afya,
rasilimali za taifa, usafiri, maji, rushwa na migogoro ya ardhi kuwa
ndiyo mambo ambayo hayajafanyiwa kazi na hivyo wanataka kusikia wagombea
watakavyokabiliana nayo.
“Kwanza tunahitaji utawala bora unaosimamia haki,
Serikali inayofanya uamuzi sahihi,” alisema mwanasheria wa jijini Dar es
Salaam, Felix Kibodya kabla ya kutaja mambo ambayo anaona yanafaa
kupewa kipaumbele.
Usimamizi wa rasilimali
Kibodya, ambaye amewahi kuwa rais wa Chama cha
Wanasheria wa Tanganyika (TLS), alisema rasilimali zikisimamiwa na
kutumika vizuri, zitalinufaisha Taifa kwa kiasi kikubwa.
“Kuna viongozi katika nchi hii waliwahi kueleza
wazi kwamba rasilimali zikibaki ardhini haziozi. Tukifanya mchezo
rasilimali hizi zitakwisha. Suala hili linaenda sambamba na
ubinafsishaji tulioufanya miaka ya nyuma, sasa ndiyo tunaaza kuona ubaya
wake,” alisema.
Alikuwa akizungumzia rasilimali kama dhahabu,
chuma, shaba, platinum, nickel, almasi, tanzanite, rubi, garnet,
emerald, sapphire na maliasili nyingine kama gesi na mafuta.
Kati ya madini hayo, dhahabu na almasi ndiyo
zimekuwa tegemeo kubwa kwa uchumi wa Tanzania, wakati kugundulika kwa
gesi na uwezekano wa kupatikana kwa mafuta kumeinua matarajio ya maisha
bora kwa wananchi na wakati fulani Rais Jakaya Kikwete aliwahi
kunukuliwa akisema “atakuwa Rais wa mwisho kuiacha nchi maskini”.
Lakini kilio kikubwa cha wadau imekuwa ni
mikataba, ambayo imeelezwa kuwa ni ya siri na hainufaishi Taifa na
badala yake inanufaisha wawekezaji na wajanja wachache.
“Hatuna sababu ya kukopa kwa mataifa tajiri wakati tuna
rasilimali za kutuingizia fedha nyingi. Tukiweza kusimamia vizuri
vivutio vya utalii, gesi, mafuta na madini tutapiga hatua kubwa,”
alisema mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika Idara ya Sayansi
ya Siasa, Richard Mbunda.
Mbunda alitaja mambo matatu yanayotakiwa kusimamiwa kwa umakini kuwa ni matumizi bora ya rasilimali, miundombinu na kilimo.
Claudian Mutayoba mkazi wa Kigoma alisema: “Jambo
la muhimu ninaloliona wazi kuwa linaweza kutusaidia ni rasilimali
tulizonazo. Kama Serikali itaweka mikakati madhubuti ya kuzisimamia
zinaweza kutufikisha mbali. Hilo halifanyiki na ndiyo maana madini
yanaibwa na wanyama kusafirishwa nje ya nchi.”
Ajira
Tatizo la ajira limekuwa likizungumzwa na wengi,
wakiwamo waliotangaza na wanaotajwa kuwania urais, wote wakielezea kuwa
ni bomu linaloweza kuibuka wakati wote. Kwa sasa takriban watu milioni
21 ni nguvu kazi iliyoko sokoni na kati yao, milioni 6.5 tu ndiyo walio
na ajira, wakati watu 800,000 hadi 1,000,000 wanaingia kwenye soko la
ajira kila mwaka.
Idadi hiyo ya watu wanaostahili kuajiriwa ni
kuanzia vijana wa miaka 15 ambao wakati wowote wanaingia sokoni kusaka
ajira na kwa mujibu wa takwimu hizo za Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS)
za mwaka 2012, idadi ya walio tayari kwenye soko la ajira ni takriban
nusu ya idadi ya Watanzania.
“Maendeleo yanatakiwa kusimamiwa. Nchi yetu ina
tatizo kubwa la ardhi na ajira. Tunatakiwa kujiuliza sababu za
wanakijiji na mwekezaji kugombania ardhi. Iweje mwekezaji apewe ardhi na
mwananchi ahamishwe,” alisema Profesa Penina Mlama, ambaye ni
mwenyekiti wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere.
“Tazama ajira. Ni tatizo kubwa ni vyema tukaweka
utaratibu wa kila mwekezaji nchini kuajiri idadi fulani ya Watanzania,
hiyo iwe lazima si ombi.”
Hoja hiyo iliungwa mkono na Tito Kisiya, mkazi wa jijini Dar es Salaam, ambaye alisema ajira ni ajenda namba moja.
“Kipaumbele namba moja ni ajira. Huwezi kukuza
uchumi wa nchi kama rasilimali watu haitumiki inavyotakiwa. Pia,
msisitizo mkubwa uwekwe katika viwanda kwa kujenga vipya, kufufua
vilivyokuwapo ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi,” alisema akiungana
na wengi waliozungumza na Mwananchi.
Desmund Mgongolwa pia alikuwa na maoni kama hayo
aliposema: “Ajira zipewe kipaumbele. Kuna haja ya kuunda mfuko wa
kukopesha vijana wasio na ajira ili waunde vikundi vya kufanya
biashara.”
Kilimo
Suala la kuboresha kilimo ili kiwanufaishe wakulima pia lilikuwa
midomoni mwa wengi na walisema kilimo sasa hakina usimamizi na hivyo
kupoteza umuhimu wake.
Inakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 70 ya
Watanzania wanaishi vijijini ambako kilimo kilikuwa kikielezewa kuwa ni
uti wa mgongo wa uchumi, lakini katika siku za karibuni makundi ya
vijana yamekuwa yakimiminika mijini na kujishughulisha na biashara
ndogondogo kutokana na kilimo kuonekana kutokuwa na manufaa kiuchumi.
Kilimo kinachangia asilimia 27.8 ya Pato la Taifa
kutokana na mazao ya pamba, kahawa, chai, tumbaku, katani na karanga
wakati mazao ya chakula ni mahindi, maharage, viazi na mihogo.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Ruaha,
Profesa Gaudence Mpangala alizungumzia zaidi suala la kilimo akihusisha
na dhana ya soko huria.
“Dhana ya soko huria ndiyo sababu ya kilimo kutowanufaisha wananchi na kutochangia Pato la Taifa kama inavyotakiwa,” alisema.
Akizungumzia mambo yanayotakiwa kuwa ajenda kuu
katika uchaguzi alisema ajenda ya kwanza ni kukuza uchumi ambao ukuaji
wake utatokana na kuboreshwa kwa sekta ya kilimo na viwanda.
“Jambo la pili ni kutokomeza umaskini ambalo
litakwenda sambamba na kumaliza tatizo la ajira. Tatu ni kutokemeza
ufisadi na rushwa na nne kujenga misingi imara ya demokrasia,” alisema.
“Serikali imejiondoa katika kusimamia na kudhibiti
uchumi na hali hii inatokea karibu kila sekta nchini. Mfano, mapato ya
wakulima ni madogo, hawana soko la kueleweka na hata likiwapo bado
wanapangiwa bei za kuuza mazao yao,” alisema.
Alisema barani Afrika Tanzania ni kati ya nchi
ambazo zinategemea jembe la mkono kwa kilimo, jambo ambalo haliwezekani
kulikuta nchi nyingine zinazoendelea.
“Tuna sera ya kilimo kwanza lakini haijasaidia
kuinua kilimo. Kilimo kikifanywa vizuri ni chanzo kizuri cha mapato na
hata kuliletea Taifa letu maendeleo, zipo nchi nyingi duniani
zimeendelea kwa sababu tu ya kilimo,” alisema.
Elimu
Wakati Serikali imezindua Sera ya Elimu bora,
wadau wanaona kuwa bado Serikali ya Awamu ya Tano itatakiwa kufanya kazi
kubwa kuboresha elimu.
CHANZO: Mwananchi
“Mimi naona vipaumbele vikubwa mwaka huu viwe ni ajira, elimu
bora inayozalisha vijana wanaojitegemea na usimamizi mzuri wa
rasilimali,” alisema Dickson Kikoti, mtaalamu wa Sayansi ya Siasa.
Suala hilo pia lilizungumziwa na mhadhiri wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda ambaye alisema elimu ni moja ya
ajenda kuu ambazo anadhani wagombea uongozi kwenye uchaguzi mkuu ujao
wangetakiwa walizungumzie kwa kina.
“Ajenda zinatakiwa kutoka kwa mgombea mwenyewe,
ila binafsi ukinitaka nitaje nitasisitiza zaidi suala la kuwa na msingi
bora wa elimu ikiwa ni pamoja kuimarisha miundombinu yake, kuhakikisha
kuwa kila Mtanzania anapata huduma bora ya afya,” alisema.
Miundombinu ya usafiri
Wakati Serikali ya Awamu ya Tatu imefanya kazi
kubwa ya kuunganisha nchi kwa kutengeneza mtandao wa barabara, bado
tatizo la usafiri wa reli kutorekebishwa linaonekana kuathiri wananchi
wengi na kuathiri barabara zenyewe.
Tanzania ina mtandao wa barabara wa kilomita
86,472, wakati Wizara ya Ujenzi inasimamia barabara za urefu wa kilomita
33,891. Kati ya hizo, barabara za urefu wa kilomita 12,786
zinaunganisha mikoa na nyingine za urefu wa kilomita 21,105 za ndani ya
mikoa.
Kwa mujibu wa tovuti ya Tanroads, kati ya barabara
za urefu wa kilomita 12,786 ambazo hutumiwa na magari makubwa, ni
kilomita 5,130 zilizojengwa.
“Huwezi kujenga barabara na kisha ukaacha kujenga
reli. Ukifanya hivyo barabara unazojenga hazitadumu. Suala la kuwa na
reli za kutosha ni muhimu lakini halipewi uzito wa kutosha,” alisema
Kibodya.
Naye Christopher Bernard, mkazi wa Dar es Salaam
ambaye amehitimu masomo ya shahada ya biashara mwaka jana, alizungumzia
suala la miundombinu akitoa mfano wa bandari.
“Hapa kwetu tuna bandari, mito, maziwa, madini
lakini tumeshindwa kuvitumia. Binafsi nadhani tunashindwa kutokana na
kukosa utawala bora. Ila ukiniambia mambo gani ya msingi tunayotakiwa
kufanya, nitakujibu kuwa ni kilimo, miundombinu na rasilimali,” alisema.
Mbunda aliongeza kuwa usafiri wa reli ndiyo
utawakomboa wananchi kwa kupunguza gharama za usafiri na kuondoa
misongamano ya magari isiyokuwa na sababu.
“Ukiwa na reli utasafirisha mizigo kwa urahisi,
usalama na kwa muda mfupi na kuondoa msongamano usiyo na msingi. Nchi
ikiwa ni miundombinu ya kutosha kila jambo litakwenda vizuri na uchumi
utakuwa.”
Maji
Maji
Kwa mujibu wa marejeo mbalimbali ya habari kuhusu
matatizo ya wananchi, suala la maji, ambalo limeingizwa kwenye Katiba
Inayopendekezwa kama moja ya haki za msingi, bado ni tatizo kubwa na
jitihada za kuanzisha miradi mbalimbali ya majisafi hazijawezesha huduma
hiyo kufika kwa asilimia kubwa ya wananchi.
Kwa mujibu wa takwimu za NBS, ni asilimia 25 tu ya
watu waishio vijijini ndiyo wanaopata maji ya bomba, wakati asilimia
18.4 wanapata maji safi kutoka vyanzo vingine na asilimia 56.7 haipati
majisafi.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, asilimia 57.9 ya watu
waishio mijini wananufaika na maji ya bomba, wakati wengine 25.6
wanapata maji kutoka vyanzo vingine huku asilimia 16.5 ikikosa huduma
hiyo muhimu. Mbali na maji safi, upatikanaji wa maji umekuwa ni tatizo
kutokana na wananchi kulazimika kufuata umbali mrefu.
Kodi
Wananchi walioongea na gazeti hili pia walitaka
ukusanyaji mbovu wa kodi kuwa ni moja ya matatizo na kutaka wagombea
walieleza kwa kina jinsi watakavyolishughulikia.
Mmoja wa watu hao ni Mbunge wa Kibaha, Silvester
Koka ambaye alisema kuwa anatamani kuona rais ajaye anasimamia ipasavyo
kodi na suala zima la rasilimali za nchi.
Alisema uchumi wa Tanzania na maendeleo yake unategemea sana kodi ambayo kila mmoja atafaidi matunda yake.
“Haiwezekani watu wanakwepa kodi halafu wanataka
maendeleo, kodi haikusanywi ipasavyo halafu tunataka maendeleo, hiyo
haipo,” alisema.
Akizungumzia raslimali, alisema raslimali za
Tanzania zinatosheleza Taifa, lakini usimamizi si madhubuti, hivyo, rais
ajaye anatakiwa kuangalia kwa umakini maeneo hayo.
Mahakama ya Kadhi
Suala la Mahakama ya Kadhi limekuwa likizungumzwa
tangu wakati wa kampeni za urais za mwaka 2005 na CCM ililiweka kwenye
ilani yake ikiahidi kuwa ingelishughulikia, lakini hadi leo bado
halijapatiwa ufumbuzi.
Muswada uliolenga kuifanya Mahakama ya Kadhi itambuliwe ambao
ulitakiwa uwasilishwe kwenye mkutano uliopita wa Bunge, ulikwama baada
ya kuwa na kasoro nyingi na Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema muswada
huo umeondolewa ili kutoa nafasi zaidi ya watu kujadili.
Wakizungumzia Mahakama ya Kadhi wananchi hao
walisema kuwa suala hilo ni haki za msingi na hivyo linapaswa
kushughulikiwa ili kuwapa wanaohitaji haki yao ya kikatiba, huku wengine
wakisema suala hilo halitakiwi kuwamo kwenye katiba.
Mijadala kuhusu suala hilo ambayo imekuwapo
inaonyesha bila ya kushughulikiwa, linaweza kuwagawa watu, kama
ilivyokuwa kwenye kashfa ya uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta
Escrow ambalo walisema liliwagawa watu kutokana na kundi moja kuona
jingine linafaidi zaidi.
Dawa za kulevya
Pia, tangu Serikali ya Awamu ya Nne iingie
madarakani imekuwa ikiahidi kushughulikia tatizo la dawa za kulevya,
lakini bado Dar es Salaam na Zanzibar zimeendelea kuwa vituo vikuu vya
kupitishia dawa hizo zilizoharamishwa kimataifa.
Fedha nyingi zitokanazo na dawa hizo zimekuwa
zikihusishwa na kukua kwa vitendo vya ugaidi, wakati matumizi ya dawa
hizo yanaathiri afya, hasa za vijana ambao ni taifa la kesho.
Migogoro ya ardhi
Kati ya maeneo ambayo hayajapata ufumbuzi ni suala la migogoro ya ardhi karibu maeneo mbalimbali ya nchi.
Kukithiri kwa migogoro hiyo, kulimlazimisha Spika
wa Bunge, Anne Makinda kuunda Kamati maalumu ya Bunge chini ya
Mwenyekiti wake, Christopher Ole Sendeka kuchunguza chanzo chake hasa
kwa wakulima, wafugaji, wawekezaji na watumiaji wengine wa ardhi nchini.
Rais ajaye anatakiwa kuangalia maeneo yenye migogoro; Kiteto (Manyara), Morogoro maeneo ya Kilosa, Ifakara na Mahenge.
Maeneo mengine yenye migogoro ni; Mwanza na Mara.
0 comments:
Post a Comment