Mfanyakazi wa kampuni ya Mwananchi Communication Limited Patrick Pera, akionyesha mkono uliopigwa risasi akiwa katika hospital ya Amana jijini Dar es Salaam |
Watu wasiojulikana wamempiga risasi moja ya mkono na kumpora
fedha kiasi cha Sh2milioni mfanyakazi wa Kampuni ya Mwananchi
Communication Limited, Patrick Pera mara baada ya kutoka kuzichukua
katika benki ya NMB tawi la Mandela jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo limetokea leo mchana katika kituo cha
mafuta cha Oil Com kilichopo katika eneo la Tabata Relini wakati Pera
alipokuwa amepakia kwenye pikipiki huku akiwa na idadi hiyo ya fedha
kutoka benki
Akizungumza na tovuti hii akiwa katika hospital ya
Amana jijini Dar es Salaam kabla ya kuhamishiwa katika hospital ya
Taifa ya Muhimbili, Pera ambaye ni Mhariri msaidizi wa habari za kwenye
mtandao amesema alifika katika benki hiyo majira ya saa nane ili
kuchukua kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya matumizi muhimu.
Amesema baada ya kuandikisha fomu na kupatiwa
fedha hizo alitoka nje ya benki hiyo na moja kwa moja alielekea kwa
waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda ili kukodi kwa lengo la kuletwa
ofisini kabla ya kwenda kukabidhi fedha hizo kwa kaka yake.
Amesema waendesha bodaboda walianza kutupiana
mpira huku kila mmoja akitaka mwenzake ampeleke ndipo kijana mmoja
alipoamua kumpakia.
Amesema kabla ya kufika ofisi za MCL wakiwa kwenye
kituo cha mafuta cha OIL Com walitokea vijana wengine wawili waliokuwa
na pikipiki na kumuamrisha atoe fedha alizokuwa nazo.
Amesema aliwauliza kuwa wao ni wakina nani, ndipo
walipomuonyesha bastola na akaamua kuwapatia fedha hizo, lakini kama
hiyo haitoshi wakaamua kumpiga risasi moja mkononi.
Baadhi ya mashuhuda waliyokuwepo katika hospitali
ya amana waliambiwa kuwa risasi iliyopigwa mkononi mwa Pera imesaga mfupa
hivyo anahamishiwa kwenye Hospital ya Muhimbili kwa ajili ya kufanyiwa
upasuaji kwa kuwa hospital hiyo haina uwezo wa kufanya hivyo.
Aidha Jeshi la Polisi limethibitisha kutokea kwa
tukio hilo na kwamba uchunguzi umeanza mara moja kwa kumshikilia na
kumuhoji kijana wa Bodaboda aliyekuwa anamuendesha Pera alipokuwa
akitokea benki.
0 comments:
Post a Comment