MGOGORO WA KIKATIBA:RAIS WA TFF JAMAL MALINZI AVUNJA KAMATI ZOTE!!

 Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi
 Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amefanya mabadiliko kwenye kamati zote, ikiwa ni miezi isiyopungua kumi baada ya kuundwa kwa kamati hizo.
Hadi sasa ni kamati mbili tu za TFF zilizofanya kazi tangu uongozi huo uingie madarakani Oktoba mwaka 2013 ambazo ni Kamati ya Uchaguzi na Kamati ya Nidhamu.
Katibu mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa alisema kuna mabadiliko katika kamati za TFF na kueleza kwamba wiki ijayo wanatarajia kutangaza wajumbe wapya wa kamati hizo.
“Ni kweli kuna mabadiliko makubwa katika Kamati za TFF, wapo wajumbe waliondolewa na tayari wajumbe wapya wameshateuliwa, kuna utaratibu maalumu tunaandaa na tutawatangazia,” alisema Mwesigwa.
Kuhusu hoja ya kuvunjwa kwa katiba ya shirikisho hilo, Mwesigwa alilikwepa  akisema hilo halimhusu.
Hata hivyo, Mwesigwa alisema kuwa Jumamosi, kamati ya utendaji ya shirikisho hilo itakaa kujadili masuala mbalimbali, ikiwamo la mkutano mkuu wa TFF uliopangwa kufanyika Machi 14 hadi 16 mkoani  Singida.
Katika siku za karibuni, TFF imekuwa kwenye mzozo na Kamati ya Rufaa za Nidhamu ambayo ilipelekewa rufaa ya Wakili Damas Ndumbaro ya kupinga uamuzi wa Kamati ya Nidhamu ya kumfungia miaka saba madai kuwa aliwakilisha klabu ya Yanga wakati akiwa mwanachama wa Simba na kwamba aliwakilisha klabu za Ligi Kuu bila ya ridhaa zao, kupinga makato kwa ajili ya kuisaidia TFF.
Makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, Hamidu Mbwezeleni amekuwa akieleza kuwa TFF haijawajulisha wanakamati kuhusu rufaa hiyo, lakini Mwesiga amekuwa akieleza kuwa suala la kujadili shauri la Ndumbaro ni la kamati.
Jana Mwesiga alinukuliwa akisema kuwa Mbwezeleni hastahili kuzungumzia kamati hiyo kwa sababu si mjumbe, kauli ambayo makamu mwenyekiti huyo aliijibu kwa kuitaka TFF itangaze rasmi ili kumpunguzia mzigo wa kufuatwa na waandishi wa habari.
Kikatiba, Kamati ya Mbwezeleni inatakiwa ivunjwe kwa ridhaa ya Mkutano Mkuu, jambo ambalo kama limevunjika uongozi wa TFF utakuwa umevunja Katiba ya shirikisho hilo.
 Kamati ya Nidhamu inaongozwa na Tarimba Abbas, na ya Rufaa ya Nidhamu inaongozwa na Profesa Mgongo Fimbo.
Pia, Kamati ya Maadili inaongozwa na Wakili William Erio, ya Rufaa ya Maadili inaongozwa na Jaji Mstaafu Stephen Ihema, Kamati ya Uchaguzi inaongozwa na Wakili Melkizedeck Lutema na ile ya Rufaa ya Uchaguzi inaongozwa na Wakili Julius Lugaziya 
Kwa mujibu wa katiba hiyo, mwenye mamlaka ya kutengua uamuzi ya Kamati ya Utendaji ya TFF ni Mkutano Mkuu wa TFF pekee, hakuna chombo kingine cha chini chenye mamlaka hayo.
Hatahivyo tayari kamati hizo zimeshavunjwa kwa sababu mbalimbali,  ikiwamo rufaa Ndumbaro aliyefungiwa miaka saba kwakujihusisha na masuala ya soka ndani na nje ya nchi.
Mmoja wa wanasheria wa shirikisho hilo alisema:  “Kwa mujibu wa kanuni na Katiba ya TFF, kamati zilizoundwa na kupitishwa na mkutano mkuu zinatakiwa zifanye kazi kwa miaka miwili ndipo zifanyiwe mabadiliko au kuvunjwa na kuteuliwa nyingine ambazo zitapitishwa tena na mkutano mkuu.
“Hakuna kiongozi au Sekretarieti ya TFF mwenye mamlaka ya kuvunja kamati za kisheria za shirikisho. Kamati ya utendaji inapitisha na mkutano mkuu unabariki, hali kadhalika uvunjaji wake ni baada ya miaka miwili,” alieleza mjumbe huyo.
TFF imepanga kufanya Mkutano Mkuu mjini Singida mwezi Aprili, ikiwa ni mwaka mmoja na zaidi tangu uongozi huo uingie madarakani, kinyume na Katiba ya TFF inayotaka mkutano huo ufanyike mara moja kwa mwaka.
Akitoa maoni yake kuhusu kuvunjwa kamati ndogo za TFF au kufanya mabadiliko kama alivyosema Mwesiga, Wakili Alex Mgongolwa alisema: “Kamati zote za TFF zinafanya kazi kwa niaba  ya Kamati ya Utendaji.
“Kamati ya Utendaji ya TFF ndiyo yenye mamlaka ya kuteua na kufukuza wajumbe wa kamati ndogo pale inapoona inafaa, ingawa kiutendaji rais ndiye anapendekeza majina yanapitishwa na Kamati ya Utendaji.
Alisema katiba inatamka  wazi kuwa kamati ya utendaji ndiyo inayoteua, hivyo mwenye  mamlaka ya kuteua wajumbe wa kamati na kuvunja ni chombo hicho.
Kamati ya Utendaji ya TFF haijakutana kubadilisha wala kuteua wajumbe wapya kama Mwesiga alivyoeleza jana na hivyo hata kuvunja uamuzi wa kamati hizo ndogo, ni kukiuka katiba ya TFF.


Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment