Waziri Mkuu Mizengo Kayanza Peter Pinda.
Waziri
Mkuu Mizengo Pinda, amesema Serikali imepanga kuajiri walimu zaidi ya 35,000
kwa ajili ya shule za sekondari, ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa walimu
nchini.
Alitoa
kauli hiyo jioni wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa kata ya Kiwere, baada
ya kukagua ujenzi wa maabara na kuzindua nyumba nne za walimu kwenye Shule ya
Sekondari ya Kiwere, tarafa ya Kalenga, wilayani Iringa.
Waziri
Mkuu alisema walimu hao watagawanywa kwenye shule kulingana na mahitaji
yaliyokwishawasilishwa na watakapopata mgawo wao, hawana budi kuangalia kwanza
shule zenye miundombinu iliyokamilika kama ilivyo kwa shule hiyo.
Akifafanua
kuhusu kasi ya ujenzi wa maabara, Waziri Mkuu alisema: “Mkoa mzima wa Iringa
unahitaji maabara 318 na zilizo tayari mpaka sasa ni 108.
“Lakini
kuna nyingine 141 ambazo zimekwishaanza kujengwa na zimefikia hatua nzuri.
Nimeambiwa katika muda mfupi ujao kutakuwa na maabara 249 zilizokamilika,”
alisema.
“RC
inabidi uwasukume watu wako ili hizi 69 ambazo hazijaanza kujengwa zikamilike
kabla ya Juni mwaka huu kama ambavyo Rais Jakaya Kikwete alivyoelekeza. Alisema
hataongeza tena muda wa ujenzi,” aliongeza.
Alisema
elimu ni sekta ya msingi ambayo Serikali imeamua kuipa umuhimu wa kipekee na
kuiweka katika moja ya maeneo sita muhimu ya kipaumbele chini ya Mpango wa
Matokeo Makubwa ya Haraka (BRN).
Waziri
Mkuu aliwataka wanafunzi wa shule hiyo wasome kwa bidii na wawe wasikivu, ili
wafanye vizuri zaidi kwenye masomo yao.
Mapema,
akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Ofisa Elimu wa Wilaya ya Iringa, Leonard
Msigwa, alisema ujenzi wa nyumba hizo nne zenye pande mbili, umegharimu Sh
milioni 323.2.
Alisema
nyumba hizo zenye vyumba vitatu vya kulala, sebule na jiko, zina uwezo wa
kubeba familia nane.
Msigwa
alisema ujenzi wa nyumba hizo ulifanywa na shirika la Deswos la Ujerumani kwa
kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Iringa pamoja na wananchi.
Pia
walisaidiwa kujengewa tangi la maji na mabweni mawili yenye uwezo wa kuchukua
wanafunzi 112 kila moja kwa ajili ya wasichana.
Akifafanua
kuhusu hali ya ujenzi wa maabara, Ofisa Elimu huyo alisema hadi sasa
wamekamilisha ujenzi wa vyumba viwili vya Kemia na Bayoolojia, lakini bado viko
kwenye hatua ya kupaka rangi. Aidha mfumo wa gesi na maji umekwishafungwa ndani
ya vyumba vya maabara.
“Ujenzi
wa maabara hadi sasa umekwisha gharimu Sh milioni 52.8/- na kwa Februari 2015,
tumefanikiwa kutengeneza baadhi ya samani za maabara yaani meza 24 na stuli 96
zenye thamani ya Sh milioni 8.9,” alisema.
|
0 comments:
Post a Comment