Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti
mjini hapa katika vituo vya uandikishaji, wananchi hao walisema kuna
mabadiliko ukilinganisha na siku zilizopita, hivi sasa kazi zinafanywa
haraka.
Mmoja wa waliojiandikisha katika daftari hilo,
Nico Ndembe alisema idadi ya watu wanaokwenda katika vituo ni kubwa,
hivyo wanatakiwa kuongeza mashine au muda wa kujiandikisha.
“Natoa ushauri kwa wataalamu wa tume kama wanaweza
kutambua uwezo wa mashine zinaandikisha idadi ya watu kiasi gani kwa
siku, jambo muhimu kwao ni kuandika namba za watu wanaopaswa
kuandikishwa, kisha wanaozidi wanarudi nyumbani,” alisema Ndembe.
Alisema hiyo itasaidia wale wanaosubiri muda muda mrefu bila kupata huduma, waendelee kufanya shughuli zao nyingine.
Naye, Aldol Mchapa alisema awali kazi hiyo ilikuwa ikichukua muda mrefu, lakini hivi sasa inachukua muda mfupi.
Katibu wa Chadema, Jimbo la Njombe, David Tweve
alisema mabadiliko yapo katika vituo mbalimbali, lakini muda uliopangwa
hautoshi.
Tweve alitoa mfano katika Kituo cha Lupila kwamba
watu waliojiorodhesha kwenye kituo hicho ili wapate vitambulisho
walikuwa 200, lakini waliofanikiwa kuandikishwa ni 127.
“Hali ilivyo sasa ni tofauti na jana (juzi) kwani
mtu mmoja kujiandikisha inachukua kati ya dakika sita hadi 10, wakati
ilikuwa zaidi ya hapo, hii inatokana na ukweli kuwa watendaji wake
wanaonekana wameshazizoea mashine,” alisema Tweve na kuongeza kuwa:
“Watu wanaokwenda kwenye vituo kujiandikisha idadi
yao ni kubwa kuliko hata makadirio ya tume, kama hawataongeza muda au
vifaa, siku saba walizopanga, hazitatosha na wengi wataachwa bila ya
kujiandikisha,” alisema.
Baadhi ya waandikishaji na wasimamizi wa mashine
wameiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kuongeza muda ili kazi hiyo
ifanyike kwa ufanisi zaidi.
Hatua hiyo inatokana na kuharibika mara kwa mara
kwa mashine hizo, wananchi kupigwa picha ambazo hazionekani kwenye
kitambulisho, kukosewa tarehe na jina pamoja na alama za vidole
kutokamilika kutokana na vidole kuwa na sugu .
Akizungumza katika kituo cha Mwembetogwa, opereta wa mashine ya
kuchukua alama ya vidole na picha, Typhone Lumato alisema kazi
inaendelea vizuri, licha ya mashine na kichapishi kuharibika mara kwa
mara.
Alisema hali hiyo inasababisha usumbufu kwa wananchi ambao wapo kwenye foleni kwa muda mrefu kusubiri huduma hiyo.
0 comments:
Post a Comment