MCHUANO
wa kumtafuta mrithi wa Rais Jakaya Kikwete, katika nafasi ya urais
ndani ya chama kikongwe CCM umefikia hatua ngumu kutokana na kubadilika
kwa upepo huku baadhi ya makada wake wakijipanga kuhamia upinzani endapo
watakosa nafasi hiyo.
Hali hiyo imebadilika ikiwa imebaki siku
moja kabla ya waziri mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, kutangaza nia
kugombea nafasi hiyo ya urais katika mkutano wake utakaofanyika mkoani
Arusha, Jumamosi wiki hii.
Kwa sasa kuna taarifa kuwa ndani ya chama hicho hali imebadilika na kukifanya chama hicho kuwa katika nafasi ngumu.
Taarifa
ambazo zimetufikia jana, zimeeleza kwamba
makada hao wamefikia msimamo huo kutokana na kile wanachodai kuna dalili
za chama hicho kufanya makosa katika uteuzi jina la mgombea, hali
itakayowapa nafasi wapinzani kushinda kwa kishindo kwenye uchaguzi huo.
Mapema
wiki hii baadhi ya vyombo vya habari vilinukuu makada wa CCM wakidokeza
kwamba wana wasiwasi mkubwa kwa baadhi ya makada wake maarufu kuchukua
hatua za kukihama chama hicho kama hawataridhishwa na mchakato mzima wa
kupata jina la mgombea wa chama hicho.
Makada waliozungumza kwa
sharti la kuhifadhiwa majina yao walitaja jina la mawaziri wawili mmoja
akiwa waziri mstaafu na mwingine ni waziri katika Serikali ya Rais
Kikwete na jina la mbunge mmoja ambaye aliwahi kuwa waziri katika
serikali hiyo kwamba wanahofiwa kuchukua uamuzi huo mzito endapo
hawataridhishwa na uteuzi wa jina la mgombea wa CCM.
Hata hivyo,
inadaiwa kuwa baadhi ya makada wenye msimamo mkali wanatishwa na upepo
unaovuma na kuonesha nguvu kubwa ya Lowassa ambaye anaonekana kuwa na
nguvu kubwa miongoni mwa wagombea wa CCM, hali inayotishia kushinda
uteuzi huo.
Pamoja na hali hiyo, baadhi ya makada ndani ya CCM
wanaamini kwamba kiongozi huyo hatoshi kwenye nafasi hiyo hali inayoweza
kutoa nafasi ya wazi wapinzani wanaounda kundi la UKAWA kushinda nafasi
hiyo.
Chanzo chetu cha habari kilieleza kwamba makada hao wa CCM
wanaohofiwa kujipanga wanaweza kukimbilia Ukawa kwa lengo moja tu la
kusaka kuteuliwa kugombea nafasi hiyo ili wapambane na Lowassa kama
atapitishwa na CCM kwa imani kwamba watakuwa na nafasi kubwa ya ushindi.
Mtoa
habari wetu huyo alisema; "Makada wanaosaka urais CCM wanahofu kwamba
Lowassa anaweza kuteuliwa kusimama kugombea urais kupitia CCM kutokana
na mazingira na kauli za viongozi wa CCM zinazotolewa sasa.
Hali
hiyo imefanya baadhi ya makada wanaoamini kwamba Lowassa hatoshi kwenye
viatu vya urais kujipanga kwenda Ukawa ili kukabiliana naye endapo
atapitishwa na CCM.”
Chanzo hicho kimesisitiza kwamba wanachama
wengi ndani ya CCM wanaamini kwamba Lowassa anaweza kuibuka na ushindi
mkubwa ndani ya vikao vya chama, lakini atakapokwenda kwa wananchi na
kukutana na hoja za upinzani mbele ya umma zilizochangia kumng’oa
uwaziri mkuu, atapoteza nafasi hiyo.
Kauli ya Mwenyekiti wa
Chadema Freeman Mbowe aliyoitoa kwenye gazeti moja akidai
kwamba Lowassa ni dhaifu na ‘bubu’ kutokana na kwamba hana ubavu wa
kukemea rushwa, ufisadi na ubadhirifu inawapa nguvu makada wa CCM
wanaotaka kukimbilia Ukawa ili kukabiliana naye endapo atapitishwa na
CCM.
Alisema makada wanaowania urais wanamjua vizuri sana hivyo
wanaamini kwamba wakiachwa watakimbilia Ukawa na huko watakuwa na hoja
za kutosha kupambana naye na nafasi yao ya ushindi itakuwa kubwa.
Wakati
huo huo, huko mkoani Mbeya macho na masikio ya Watanzania yanatarajiwa kuelekezwa mkoani
Mbeya Juni Mosi, mwaka huu wakati Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi
Maalum) Profesa Mark Mwandosya, atakapotangaza rasmi kuwania urais
kurithi nafasi inayoachwa na Rais Jakaya Kikwete, ambaye anamaliza muda
wake kwa mujibu wa Katiba.
Akizungumza kwa njia ya simu akiwa
nchini Vietnam jana alikokwenda kumwakilisha rais, Prof. Mwandosya
alisema kuwa siku hiyo (Jumamosi) atatangaza rasmi kuwania tena nafasi
hiyo ambayo mwaka 2005 aliwania na kufanikiwa kushika nafasi ya tatu.
Hatua
hiyo bado inatafsiriwa kwamba wana-CCM wana imani kubwa na yeye, hivyo
katika mchuano wa mwaka huu ana nafasi ya kufanya vizuri zaidi. Alisema
kuwa baada ya kuwa mbunge na waziri kwa kipindi cha miaka 15 akiwa
anachaguliwa na wananchi wa Busokelo mara zote bila kupingwa hali
ambayo imempa nguvu wakati wote na kuona kuwa ni wakati wa kuachia
nafasi hiyo na kumwachia mwingine na kisha yeye kurudi ulingoni kwa
ajili ya kuomba ridhaa na kuwaongoza Watanzania wote.
Prof.
Mwandosya alisema kuwa yeye anajivunia kuwa mzalendo aliyesomeshwa kwa
kodi za Watanzania na hivyo anaona deni la kuwatumikia Watanzania kwa
uaminifu mkubwa kama ambavyo ameonesha wakati wote alioaminiwa na Rais
Dkt.Jakaya Kikwete pamoja na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa.
Alisema
rekodi yake haina shaka inamsukumu awatumikie Watanzania. Waziri huyo
alisema ameamua kutoa heshima kubwa kwa wazazi wake wa Mkoa wa Mbeya kwa
kuamua kurudi nyumbani kutangaza azima hiyo ambapo pia kwa kutambua
kuwa yeye amekuwa akitumikia CCM wakati wote ameona vyema kwenda makao
makuu ya chama hicho mkoani Mbeya kwa ajili ya kutangaza nia.
Wananachi
wa Mkoa wa Mbeya na mikoa jirani wakizungumzia hali hiyo wamesema
wamejipanga kwa ajili ya kumpokea kiongozi huyo. Walisema atapata
mapokezi ya kishindo kikubwa.
Mzee Daimon Mwasampeta, ambaye ni
kiongozi mstaafu wa chama cha NCCR-Mageuzi alisema Profesa Mwandosya ni
mtu wa watu wote pasipo kujali itikadi na hivyo kinachotakiwa ni
kuhakikisha anatumia uwanja wa Sokoine ili azungumze na Watanzania wengi
bila kujali itikadi zao kama rais mtarajiwa.
Mwenyekiti mstaafu
wa CCM Mbeya Mjini, Allan Mwaigaga, alisema Watanzania wanapaswa waache
woga katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi kwa kuhakikisha wanasema
wazi kuwa umefika wakati wa rais kutoka katika mikoa ya Mbeya, Iringa
na Njombe kutokana na ukweli kuwa haijawahi
kutoa rais wala waziri mkuu.
Mwaigaga ambaye ni mfanyabiashara mmiliki wa mabasi ya Ndenjela, alisema
kuwa
Watanzania hususani wanaotoka katika mikoa hiyo iliyosahaulika
wanapaswa kuweka msimamo mkali kwa kuwaunga mkono wagombea wao ili
kuonesha usawa katika nchi ya Tanzania.
Alisema Mkoa wa Mara
umetoa Rais, Arusha Waziri Mkuu, Pwani Rais, Katavi Waziri Mkuu, Dodoma
Waziri Mkuu, Mtwara Rais na hivyo kuonesha wazi kuwa sasa ni wakati
wa mikoa ya Mbeya, Iringa na Njombe kutoa rais.
This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
0 comments:
Post a Comment