Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad akihutubia wanachama wake mara baada ya kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa na chama hicho kugombea urais wa Zanzibar. |
Alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari visiwani
hapa baada ya kuchukua fomu hiyo katika ofisi za CUF Bububu wilaya ya
Magharibi jana kwa ajili ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25,
mwaka huu.
“Ingekuwa afya yangu siyo nzuri nisingegombea nafasi hii, lakini
kwa kuwa nipo imara kimwili na kiakili na siugui wala siyo mgonjwa
nitagombea,” alisema Maalim Seif.
Alisema hakuna atakaemzuia kuwa Rais wa Zanzibar na kuwataka
wafuasi wa chama hicho kuwa na umoja na mshikamano ili kuibuka na
ushindi katika uchaguzi huo.
VIPAUMBELE VYAKE
Alieleza vipambele vyake endapo atashinda katika uchaguzi mkuu na
kuwa Rais wa Zanzibar kuwa ni pamoja na kuwafanyia mambo mema
Wazanzibari ambayo yameshindwa kutekelezwa na CCM.
Pia alisema atahakikisha amani na mshikamano na haki sawa kwa watu wote kwa sababu haki hiyo haipo na inatolewa kwa upendeleo.
Alitolea mfano haki ya kupata vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi,
akidai haki hiyo inatolewa kwa dhuluma na wenye haki hiyo wananyimwa na
kupewa watu wengine ambao hawana haki na wala hawastahili kupewa.
Alisema pia atahakikisha anaboresha maisha ya wananchi wa Zanzibar kwani hali zao za kimaisha kwa sasa haziridhishi.
“Rasilimali Zanzibar tunazo lakini hazijatumiwa vizuri, lakini
ninaahidi mkinichagua nitazitumia rasilimali zilizopo na vijana mtapata
ajira sawa sawa,” alisema Maalim Seif huku akishangiliwa na wafuasi
wake. Alipoulizwa kuhusu endapo atashindwa katika uchaguzi mkuu ujao
ataendeela tena kugombea nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka
2020, alisema wakati ukifika ataamua kama alivyoamuwa mwaka huu kuwa
atagombea au hatagombea.
Kuhusu wanachama wa chama hicho kutogombea nafasi hiyo ya urais na
badala yake kuwa mgombea pekee kila mara, Maalim Seif ambaye pia ni
Makamu wa Kwanza wa Rais, alisema hajamzuia mtu kugombea nafasi hiyo na
kuwataka wafuasi wake kujitokeza kugombea.
“Chama hiki hakina ubaguzi kila mtu ana haki ya kugombea nafasi
hii na wala hakuna anayeniogopa labda niseme kuwa tu wameridhika na mimi
nigombee nafasi hii,” alisema.
Alisema muda bado upo wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kugombea urais na imani yake kuwa watu watajitokeza.
WAFUASI CUF WAZUNGUMZA
Wafuasi wa chama hicho ambao walijitokeza kwa wingi kutoka maeneo
mbalimbali ya visiwa vya Zanzibar kumsindikiza kiongozi wao kuchukua
fomu hiyo, walionekana kuwa na furaha na kusherehekea uamuzi wa kiongozi
wao na kusema uamuzi huo wa Maalim Seif ni matarajio yao kuona
anashinda na watampa kila ushirikiano kuhakikisha anaongoza nchi.
Khadija Salum Ali (53), mkazi wa Michezani ambaye alifika katika
maeneo hayo, alisema kitendo cha kiongozi huyo kuchukuwa fomu
kimemfurahisha kwa sababu amewakubalia maombi yao kwani ndiye
wanayemtaka kwani wana imani ataikomboa nchi .
“Maalim Seif anania njema na Wazanzibari na ndio maana wafuasi
wake tunamkubali na kumuamini na yale ambayo tunayahitaji. Wazanzibari
ndiyo wanaopata tabu katika mfumo wa Mungano,” alisema Khadija.
Alisema ni matumaini yake Maalim Seif akiwa Rais wa Zanzibar
watapata serikali yenye mamlaka kamili na kuwa na Muungano wa mkataba.
Shihabu Ahmmed, mkazi wa Hurumzi, alisema alisema kwa wakati huu
hakuna kiongozi mwingine katika chama hicho atakayeweza kukiletea
ushindi chama hicho kwa nafasi ya urais wa Zanzibar zaidi ya Maalim
Seif.
Alisema tokea chama hicho kilipotangaza utoaji wa fomu za kugombea
nafasi hiyo hakuna mtu aliyejitokeza kugombea nafasi hiyo zaidi ya
katibu mkuu huyo kwa sababu hakuna atakayeweza kukiletea ushindi chama
hicho.
“Maalim Seif ni mtu wa watu, kwanza ana mvuto, haiba na anakubalika
kila kona kwa hivyo watu wanaona kushindana naye ni kujihangaisha tu,”
na kuongeza:
“Kama yupo mtu anaweza kushindana na mkwaju huu na kuiletea
ushindi Zanzibar kwa tiketi ya CUF basi ajitokeze lakini mimi kura yangu
ni kwa Maalim Seif.”
0 comments:
Post a Comment