Akiwa kwenye mkutano wa hadhara wa Chadema mjini
Moshi, hivi karibuni, Lissu alikaririwa akieleza kuwa Dk Slaa, ndiye
atakayepitishwa na Ukawa kugombea nafasi hiyo.
Lakini Mkuu wa Idara ya Kampeni na Uchaguzi wa
NCCR-Mageuzi, Faustine Sungura alisema mwishoni mwa juma
kuwa ni makosa kudhani kwamba Chadema ndicho Chama chenye nafasi ya
kusimamisha mgombea urais kupitia Ukawa, wakati bado mchakato wa kumpata
mgombea haujafanyika.
Sungura ambaye pia ni miongoni mwa waasisi na
mwanzilishi wa mageuzi nchini, alisema kati ya vyama vinne vilivyounda
Ukawa, tayari Chadema imepewa majimbo mengi ya ubunge. “Fursa hiyo pekee
imeshawapa uwezekano wa kutoa waziri mkuu kama upinzani utashinda”,
alisema.
“Kwa kawaida chama chenye wabunge wengi ndicho
kinachotoa waziri mkuu, sasa kwa namna yoyote Chadema ndiyo itakayotoa
waziri mkuu, hivyo haiwezekani watoe na mgombea urais. Nawashauri
wachague nafasi mojawapo,” alisema Sungura.
Sungura alisema kauli hiyo ya Lissu siyo sahihi na
hailengi kujenga Ukawa, bali kuubomoa kwa kuwa haiwezekani chama kimoja
kitoe rais, makamu wake na waziri mkuu. “Ni vizuri ikaeleweka mapema
kwamba, haiwezekani chama kimoja kati ya vyama vinne washirika wa Ukawa,
kikatoa mgombea urais, makamu na waziri mkuu,” alisema Sungura na
kuongeza:
“Kwa kuwa CUF kina nafasi kubwa ya kumtoa mgombea
urais wa Zanzibar, vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema na NLD, kimoja kati
ya vyama hivyo kitamtoa ama rais au waziri mkuu au spika wa Bunge,
kinyume chake ni tamaa inayoweza kuua Ukawa.”
Kwa mujibu wa Sungura, mageuzi chanya hayawezi kuletwa kwa ubinafsi, bali nia ya dhati ya Ukawa katika kuyatafuta.
0 comments:
Post a Comment