ZENGWE LINGINE DODOMA WABUNGE WA UKAWA WAIKALIA KOONI IKULU!!

Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (kushoto) akichangia bungeni mjadala wa kupitisha bajeti ya Ofisi ya Rais , Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Utawara Bora na Uhusianao na Uratibu kwa mwaka wa fedha 2015/2016, mjini Dodoma jana
Mjadala wa bajeti mwaka 2015/16 umegeuka mwiba mchungu kwa Ofisi ya Rais baada ya mawaziri watatu waliopo katika ofisi hiyo kubanwa na wabunge wa upinzani hasa wale wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wakisema “njaa imeanzia Ikulu na Ofisi ya Rais inayosimamia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) haina utashi wa kupambana na rushwa.”

Mawaziri hao jana walitakiwa kueleza sababu za ofisi hiyo kushindwa kutokomeza rushwa, mikakati ya Serikali kuiwezesha Takukuru na kuipa meno ya kuwashtaki moja kwa moja watuhumiwa wa rushwa.
Kambi hiyo imeilipua Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (Wama) inayoongozwa na mke wa Rais, mama Salma Kikwete wakitaka ifutwe kwa maelezo kuwa imekiuka sheria za nchi.
Katika mjadala huo, Mbunge wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali aliibua malumbano makali kati yake na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika na Mwenyekiti wa Bunge, Lediana Mng’ong’o, baada ya kudai kuwa Ikulu na Serikali ya Awamu ya Nne imeshindwa kupambana na rushwa licha ya kuwa chini ya Rais.
Katika mjadala huo, Mkosamali alihoji; “kama Takukuru, Mkurabita na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (Tasaf) ziko chini ya Ofisi ya Rais na bado zinalia njaa, kwa nini watumishi wa umma kama wauguzi na walimu wawe chini ya ofisi hii badala ya kuwa katika Ofisi ya Waziri Mkuu au Tamisemi?
“Yaani njaa imeanzia Ikulu. Tumeiweka Takukuru Ikulu tukidhani kuwa Rais ataweza kupambana na rushwa, sasa ukiona taasisi hiyo imefeli tambua kuwa Rais hana utashi wa kisiasa wa kupambana na rushwa.
“Watu wanajua Takukuru ikiwatuhumu katika kesi kubwa zitafutwa. Taasisi hii kufeli kufanya kazi maana yake ni kuwa Serikali imefeli katika miaka yote minane, hata Rais hakuwa na nia ya kupambana na rushwa,” alisema na kusisitiza jinsi Bunge la Katiba lilivyoshindwa kuipa meno Takukuru kupitia Katiba Inayopendekezwa.
Alihoji, “Tasaf wameomba Sh18 bilioni mwaka jana na mpaka sasa wamepewa Sh3 bilioni na sasa hivi mnaomba tena mabilioni ya shilingi. Hivi mnataka wakurugenzi wa Tasaf na wafanyakazi wawachukuliaje?”
Alihoji taasisi zilizopo chini ya Ofisi ya Rais kutopewa fedha za bajeti kama ilivyoidhinishwa mwaka jana na kusema kitendo cha mwaka huu wizara tatu za Ofisi ya Rais kuja na bajeti nyingine wakiomba mabilioni ya fedha ni fedheha.
“Kama taasisi zilizopo Ikulu zina njaa, hivi nyinyi huko katika halmashauri si ndiyo mtakufa! Rais ambaye taasisi hizi zipo ofisini kwake anashindwa kuzihudumia atawakumbuka watu wa Kibondo? Hii Serikali imechoka kabisa na imechakaa,” alisema.
Kauli hiyo ilimnyanyua Mkuchika na kuomba kutoa taarifa, jambo ambalo lilipingwa na Mkosamali akidai kuwa awali aliomba kutoa taarifa kwa mwenyekiti na kunyimwa.


“Mwenyekiti usiendeshe Bunge namna hii, nieleze umetumia kanuni gani ya kunizuia nisitoe taarifa na kumruhusu Mkuchika. Umetumia kifungu kipi, kwani huyu (Mkuchika) si mbunge kama mimi,” alihoji Mkosamali na kujibiwa na Mng’ong’o kuwa Mkuchika ni waziri.
 
Huku akiwa amesimama, Mkosamali aliendelea kuzungumza licha ya kuzimiwa kipaza sauti.
Katika taarifa yake Mkuchika alisoma Kanuni ya ya Bunge 64 (d) inayosema; Hatatumia jina la Rais kwa dhihaka katika mjadala au kwa madhumuni ya kutaka kulishawishi Bunge kuamua jambo lolote kwa namna fulani.
“Mkosamali wakati anachangia ameeleza Rais hana nia ya kupambana na rushwa. Namtaka afute kauli hiyo kwa sababu amekwenda kinyume na kanuni za majadiliano. Ila mchana nikimjibu nitamweleza alichokifanya Rais katika kupambana na rushwa,” alisema Mkuchika.
Taarifa hiyo ilikataliwa na Mkosamali akisema: “Nitafutaje wakati ndiyo hali halisi. Juzi, Katibu Mkuu Kiongozi (Balozi Ombeni) Sefue kawasafisha wala rushwa. Kesi kubwa zote mmezifuta na suala la kuiongezea meno Takukuru lililokuwa katika rasimu ya (Jaji Joseph) Warioba mmeshindwa kuliweka katika Katiba Inayopendekezwa.”
Licha ya kutakiwa na Mng’ong’o kufuta kauli ya ‘Rais kashindwa kupambana na rushwa’, Mkosamali alisisitiza, “Nimesema Takukuru wakituhumu kesi 4,000 wanashinda kesi 40 hadi 50, sasa huo ni uongo, kweli wana nia ya kupambana na rushwa?”
Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Karagwe (CCM), Gosbert Blandes alisema Sheria ya Kupambana na Rushwa inatakiwa kubadilishwa ili kuiwezesha Takukuru kumshtaki moja kwa moja mtuhumiwa wa rushwa, badala ya kumchunguza tu na kupeleka faili kwa DPP.
Mbunge wa Tarime (CCM), Nyambari Nyangwine alisema: “Takukuru inatakiwa ipewe fedha kwa wakati na watumishi wa kutosha ili iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Tunatakiwa tuwe na sheria kali ili watakaokamatwa kwa rushwa wanyongwe au kupigwa risasi kabisa.”
Aliongeza, “Viongozi wote wanatakiwa kuchunguzwa kwa sababu wanapata maendeleo ndani ya muda mfupi tangu kuwa viongozi, iweje ndani ya mwaka tu mtu awe na nyumba ya ghorofa na magari?”
Mbunge wa Manyoni Mashariki (CCM), John Chiligati alisema: “Rushwa imekithiri kwa kiasi kikubwa ninaitaka Serikali ieleze kwa nini haichunguzi mali za viongozi. Wapo viongozi wanaotumia ofisi za umma kwa masilahi yao binafsi kwani ndani ya muda mfupi wanakuwa matajiri wa kutupwa.”
 
 Akiwasilisha hotuba ya Kambi ya Upinzani kuhusu matumizi ya Ofisi ya Rais na Uratibu, msemaji wa kambi hiyo wa Ofisi ya Rais, Ester Matiko alisema, Wama inatakiwa ifutwe kwa sababu imekiuka sheria za nchi.

“Iweje Waziri (Simba) awe mjumbe wa Bodi ya Wama wakati ni wizara yake ndiyo inasimamia taasisi zisizokuwa za Serikali? Ikiwa Serikali imeamua kuyasafisha mashirika yasiyo ya kiserikali isisahau kuifutia Wama usajili,” alisema.
Katika hotuba yake, Matiko pia alisema Usalama wa Taifa umeshindwa kazi kutokana na nchi kuwa na matukio mengi ya ufisadi, mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi na rushwa...
 “Ni jambo la kushangaza kuwa na Usalama wa Taifa unaoshindwa kutoa taarifa za kiintelejensia kuhusu ukatili kwa watu wenye ulemavu wa ngozi wasiozidi hata 200,000. Hii ni aibu kubwa kwa utawala wa CCM na Rais Kikwete.”
Awali, akiwasilisha bajeti ya Ofisi ya Rais, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani alisema Takukuru imefanikiwa kurejesha zaidi ya Sh623 milioni baada ya kuchukua hatua mbalimbali za kupambana na rushwa.
“Kutokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa katika jitihada za kupambana na rushwa, wahusika waliopatikana na hatia walirejesha Sh623,941,408,” alisema Kombani.
Alisema katika kipindi cha kati ya Julai mwaka jana hadi Machi, majalada 50 yaliyohusu tuhuma za rushwa kubwa yalifikishwa kwa DPP, kati ya hayo 27 yamepata kibali na watuhumiwa wamefikishwa mahakamani.
Kombani alisema kesi  856 za rushwa ziliendeshwa mahakamani zikiwamo mpya 192. Alisema kati ya kesi hizo, 664 zilitolewa uamuzi na watuhumiwa 73 walipatikana na hatia na kuadhibiwa.
“Kesi 24 ziliondolewa mahakamani kutokana na sababu mbalimbali na kesi 123 watuhumiwa wake waliachiwa huru,” alisema.
Katika mwaka wa fedha 2015/ 2016, Kombani alisema Takukuru itaendelea kuchunguza tuhuma 2,776 zilizopo na mpya zitakazojitokeza.
Akizungumzia mishahara, Kombani alisema katika mwaka wa fedha 2014/2015, Serikali imeongeza kima cha chini cha mshahara kutoka Sh240,000 hadi Sh265,000 kwa mwezi.

“Vibali vya ajira mpya 58,483 kati ya 68,138 vilivyoidhinishwa katika bajeti ya 2014/2015 vilitolewa,” alisema.
Alisema mwaka 2015/2016 Serikali inatarajia kuajiri watumishi wapya 71,496 na kipaumbele kitakuwa katika sekta za elimu, afya, kilimo na mifugo.

Akijibu hoja za wabunge hao, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya alimshutumu mmoja wa kiongozi wa upinzani kwa kushindwa kuwa mzalendo.
Alisema kiongozi huyo akiwa Marekani, alieleza kuwa Tanzania imekuwa ikikiuka haki za binadamu kwa kuwapiga wapinzani.
Alisema kiongozi huyo alipigiwa makofi bila kufahamu waliokuwa wakifanya hivyo walikuwa wakimshangaa kwa kitendo chake cha kutokuwa mzalendo kwa nchi yake.
Alisema kiongozi huyo alifika mbali na kusema kuwa wataleta wanasheria na kuipeleka Serikali katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai ya The Hague.
“Huwezi kumkuta Mmarekani akiisemea vibaya nchi yake na hii ni kwa nchi yoyote duniani. Mimi niliposikia nilishangaa kwelikweli,” alisema.
Aliwaomba wabunge wa upinzani kumpa heshima yake Rais na kuacha kumzungumza kama wanavyomzungumzia mbunge mwingine.
“Huwezi kumzungumzia Rais kama unavyomzungumzia Mbunge wa Rungwe. Mimi mnaweza kuzungumza hata mkitaka kunitukana sawa, lakini mnapomzunguzia Rais lazima tuseme,” alisema.
Profesa Mwandosya alitumia fursa hiyo kuaga akisema hatagombea tena ubunge katika Uchaguzi Mkuu... “Miaka 15 niliyopita bila kupingwa inatosha labda unaweza kuwa ndiyo mwanzo wa kulitumikia Taifa katika ngazi nyingine,” alisema.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba alisema ni shirika lisilo la kiserikali moja tu la Sisi kwa Sisi lililofutiwa usajili kutokana na kujihusisha na ushoga.

Kuhusu Wama alisema imesajiliwa na Brela na inaendeshwa kwa kufuata taratibu za kisheria.
Katika majibu yake, Mkuchika alisema hakuna mkutano wowote ulioitwa na Ikulu kwa ajili ya kuwasafisha mawaziri na viongozi waliohusika na sakata la Tegeta Escrow wala Operesheni Tokomeza.
Juu ya Rais Kikwete kutokuwa na dhamira ya kupambana na rushwa, alisema Rais, Serikali na chama kupitia ilani yake ya uchaguzi wana dhamira ya dhati ya kupambana na tatizo hilo.
Alitaja mambo yanayoonyesha kuwa Serikali ina dhamira ya dhati kuwa ni pamoja na kujenga makao makuu ya Takukuru, kujenga ofisi saba za chombo hicho na kuongeza raslimali watu.


Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment