MAALIM SEIF ALAUMU TUME YA UCHAGUZI ZANZIBAR KUANDIKISHA WAPIGA KURA HEWA!!

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam jana. 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ametoa tuhuma nzito dhidi ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) akidai kuwa iliandikisha na kuruhusu wapigakura wasiostahili zaidi ya 10,000 kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa 2010, wakiwamo marehemu 8,507.
 
Maalim Seif aliyewania urais wa Zanzibar katika uchaguzi huo na kushindwa ikiwa ni mara ya tano na wagombea wa CCM, alitoa tuhuma hizo jana alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam akisema wapigakura hao wasiostahili, bado wapo kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura la Zanzibar.
Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, alikuwa akizungumzia utafiti wa Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa Zanzibar uliofanywa kati ya Agosti 2014 hadi Machi 2015. Alieleza pia kwa nini hakulalamika wakati huo na badala yake akakubali matokeo.
Kwa nini alikubali matokeo?
“Ni ukweli usiopingika kwamba uchaguzi huo ulikuwa na mapungufu lukuki lakini mawakala wetu hawakuwa na vithibitisho, hatukuweza kupinga matokeo yale kwa sababu hatukuwa na uthibitisho wowote.”
Aliongeza, “Hivi unaweza kusema matokeo siyo ya haki wakati huna uthibitisho? Lakini utafiti huu umeweka wazi mambo yote yaliyofanywa nyuma ya pazia kwenye uchaguzi uliopita, kwa hiyo sasa tuna uthibitisho wa kutosha.”
Kiongozi huyo alisema endapo kasoro hizo zikifanyiwa kazi, Rais wa sasa, Dk Ali Mohamed Shein ajiandae kisaikolojia kuwa makamu wa rais wakati yeye akiwa Rais baada ya uchaguzi ujao.
Kasoro za uandikishaji
Kwa mujibu utafiti huo, ZEC iliandikisha katika daftari hilo wapigakura wenye umri chini ya miaka 18, ambao si wakazi katika maeneo waliojiandikisha na waliotumia majina na picha ambazo siyo zao.
Alisema licha ya baadhi ya watu hao kuwa marehemu na wengine wasiokuwa na sifa, bado hawajafutwa kwenye daftari hilo tangu 2010 na majina yao yatatumika kupiga kura mwaka huu.
Akizungumza kwa kujiamini huku akitabasamu, Maalim Seif alisema utafiti huo unaonyesha kuwa kuna zaidi ya watu 10,000 ambao waliandikishwa kinyume na sheria na kwamba walipiga kura katika uchaguzi wa mwaka 2010.
Akitoa mfano huku akirejea utafiti huo, Maalim Seif alidai kwamba katika Jimbo la Donge, ZEC iliandikisha watoto 463 ambao hawajafikisha umri wa miaka 18 na kwamba walipiga kura.

Katika matokeo ya Uchaguzi Mkuu 2010, Zanzibar mgombea urais wa CCM, Dk Ali Mohamed Shein alipata kura 179,809 sawa na asilimia 50.1 wakati Maalim Seif wa CUF alipata kura 176,338 sawa na asilimia 49.1.
Maalim Seif aliwataja na kuonyesha picha za watu aliodai waliandikishwa kinyume na sheria na maeneo wanayotoka.
“Hii ni sehemu ya rafu zilizofanywa na ZEC ambazo tumezibaini kwenye utafiti, tuna ushahidi wa kila aina, tunajua majina yao, wanapoishi, vitambulisho vyao na picha zao,” alisema.
Utafiti wenyewe
Mkuu wa Kitengo cha Sera, Utafiti na Mafunzo wa CUF, Hassan Jani Masoud alisema makosa yaliyoonekana katika uandikishaji wa daftari hilo yanarudisha nyuma demokrasia.
Alisema ukiangalia sura za watoto walioandikishwa kwenye daftari unagundua kwamba ZEC ilidhamiria kuisaidia CCM kwa gharama zozote.
“Ni watoto wadogo lakini walivyoandikishwa wameonyesha kwamba wamefikisha umri wa miaka 18, hii ni hatari,” alisema na kuongeza:
  “Kuna wale walioandikishwa kwa zaidi ya mara moja, unakuta picha ya mtu mmoja lakini imepigwa kwa nyakati tofauti na majina yanatofautiana.”
Kinachofanyika sasa
Maalim Seif alisema shughuli ya uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura itaanza Mei 16 hadi Juni 28, mwaka huu na imebainika kwamba yaliyojitokeza katika uchaguzi uliopita yatarudiwa.
“Hivi tunavyozungumza kunaendelea zoezi kubwa la kuandaa wapigakura haramu ili waweze kuja kuandikishwa,” alidai na kuongeza kuwa maandalizi hayo yanahusisha Idara ya Usajili wa Wazanzibari ambao ndiyo hutoa vitambulisho vya Mzanzibari, wakuu wa mikoa na wilaya, masheha na sekretarieti ya ZEC na vikosi vya ulinzi na usalama.
Alisema kambi moja ya jeshi Zanzibar inatumika kuandikisha mamia ya vijana ambao wanapewa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi ili waje waandikishwe kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura.
“Vijana hao wamekuwa wakipelekwa kwenye kambi hiyo kwa magari maalumu katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita na wiki iliyopita wameitwa na kupewa vitambulisho vya wakaazi,” alidai.

Alidai kuwa katika majimbo mbalimbali ya Unguja na Pemba, vijana wanaofikia 20,000 wameandikishwa na kupewa vitambulisho na miongoni mwao wapo watoto walio chini ya umri wa miaka 18.
Upande wa ZEC
Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha hakupatikana jana kuzungumzia madai hayo licha ya kupigiwa simu zaidi ya mara tatu na gazeti hili.
Hata aliyetajwa kuwa Mkurugenzi wa ZEC alipopigiwa simu yake ya mkononi, alipokea na kujibu kwamba yeye si mkurugenzi wa tume hiyo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohammed Aboud Mohammed alipopigiwa simu alisema: “Nipo kwenye kikao” na kukata simu.
Alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno kwenye simu yake na kuulizwa kuhusu hali hiyo, Aboud alijibu: “Nipo kwenye BLW (Baraza la Wawakilishi) kwenye kamati ya uongozi.”
Maagizo ya CUF
Maalim Seif  alisema ili Uchaguzi Mkuu ujao uwe huru na amani na ili kuiepusha nchi na vurugu, chama hicho kimetoa maagizo tisa ambayo SMZ na ZEC wanatakiwa kuyachukua.
Maagizo hayo ni pamoja na “Wapigakura haramu wote waliopatiwa vitambulisho vya Mzanzibari mkazi kinyume na sheria watakiwe kuvisalimisha na wasiandikishwe katika Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Agizo jingine ni watu wote wenye haki ya kupatiwa vitambulisho wapewe kabla ya uandikishaji wapigakura ili waweze kutumia haki yao ya kupiga kura.
Vilevile, vikosi vya jeshi na Idara Maalumu ya SMZ ziache kutumiwa kisiasa na kwenda kinyume na sheria zinazoongoza kazi zao.
Ofisi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Idara Maalumu za SMZ) iache kuwatumia wakuu wa mikoa, wilaya na masheha katika kusajili wapigakura haramu kwa kuwapatia vitambulisho.

CUF pia imeitaka pia Idara ya Usajili wa Mzanzibari iache kutumika kisiasa kwa kusajili watu wasio Wazanzibari, watoto wadogo na watu wanaotoka nje ya majimbo yao kwa lengo la kuisaidia CCM.
Chama hicho kimelitaka Jeshi la Polisi lisikubali kutumiwa kinyume na sheria kuwalinda wapigakura haramu wanapopelekwa kwenda kujiandikisha
Chama hicho pia kimetaka Daftari la Wapigakura lifanyiwe uhakiki kwa mfumo wa kielektroniki unaotumia alama za mwili (BVR) ili kuwafuta waliosajiliwa zaidi ya mara moja na kuwaondoa waliofariki na watoto chini ya umri wa miaka 18.
Agizo jingine ni kuwa sekretarieti ya ZEC ifanyiwe marekebisho ili iwe huru isiyojiegemeza kwa CCM.
Pia, CUF imetaka ZEC ikatae kutumiwa na CCM katika suala la ukataji wa mipaka ya majimbo ya uchaguzi.
Maridhiano
“Pamoja na matatizo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 tuliweza kuvuka salama kupitia misingi madhubuti ya maridhiano ambayo tuliyaasisi mimi na Rais mstaafu, Aman Karume,” alisema na kuongeza: “Sisi tulitekeleza wajibu wetu ni imani yangu kwamba Rais Jakaya Kikwete na Rais Ali Mohamed Shein nao watafanya wajibu wao ili kuepuka kuturudisha kule tulikotoka.
“Naomba niwakumbushe wenzangu kwamba wimbi la mabadiliko linapofikia wakati wake huwa halizuiliki tena, CCM isitarajie kuendelea kubakia madarakani kwa kutumia njia za hadaa, hujuma, udanganyifu, nguvu na vitisho.
Kwa nini asiwaache wengine?
Maalim Seif alipoulizwa kama yuko tayari kuwaachia wengine kuwania nafasi ya urais katika SMZ kupitia chama hicho na yeye kupumzika, alisema: “Sijawahi kuwakataza wanachama wa CUF kuwania nafasi ya urais, mimi nimekuwa nikijitokeza kuwania na wengine wajitokeze kuwania na hii ndiyo demokrasia.”
Alisema wanachama wa chama hicho wana haki sawa ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi ikiwamo urais... “Sasa kama hawajitokezi hilo si tatizo langu, mimi nimekuwa nikijitokeza.”
Uhakiki wa ZEC
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF, Ismail Jussa Ladhu alisema chama hicho kinaendelea na msimamo wake wa kutaka uhakiki ZEC ufanywe na kampuni za kimataifa.
“Tunaamini kampuni kutoka nje itakuwa huru na itatenda haki katika jambo hili tofauti na kampuni ya hapa ndani,” alisema.
Alisema kasoro hizo zikiondolewa, Dk Shein ajiandae kisaikolojia kuwa makamu wa kwanza wa Rais wa SMZ
“Kasoro zilizopo zikirekebishwa tunachukua nchi katika Uchaguzi Mkuu ujao, Dk Shein ajiandae kutupisha,” alisema.
Kwa nini utafiti Zanzibar tu?
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema ulifanywa Zanzibar pekee yake ili kupata matokeo kabla ya Uchaguzi Mkuu.
 “Tumefanya upande wa Zanzibar kwa sababu kama tungefanya Tanzania nzima gharama zingekuwa kubwa na utafiti ungechukua muda mrefu,” alisema.
Alisema lengo lilikuwa kukiwezesha chama kuchukua hatua zinazostahili.
Kauli ya CCM
Akizungumzia madai ya Maalim Seif, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema tuhuma hizo ni za uzushi na wala hazina ukweli wowote.“(CUF)  wanafahamu tupo kwenye maandalizi ya Uchaguzi Mkuu kwa hiyo wanaanza kujenga hofu za makusudi kwa watu na kuipaka matope CCM kwa tuhuma za uongo ili watakaposhindwa waseme tumewaonea,” alisema Vuai na kuongeza:
“ZEC ina wawakilishi saba, wawili wanatoka CUF ambao waliwapendekeza wenyewe kwa ajili ya kuhakikisha kunakuwa na uchaguzi huru na haki, sasa wanacholalamikia ni nini! Wanataka kusema wawakilishi wao wanawageuka?”Alisema chama hicho hakitakiwi kuilalamikia CCM badala yake wailalamikie tume hiyo kwani ndiyo iliyopewa dhamana ya kusimamia uchaguzi.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment