Hii ni njia ambayo mwanamke anaweza
kutumia kupanga uzazi bila kutumia dawa au kitu cha aina yoyote. Njia hii inategemea kuchagua kwa makini siku
za kufanya mapenzi kutegemeana na ufahamu wa kipindi chote cha hedhi cha
mwanamke.
Njia hii ina faida yake, lakini
yeyote anayeitumia lazima awe makini sana, kwa sababu lazima ajue lini
anategemea kupata damu ya hedhi tena. Ni
rahisi sana kufanya makosa kwa kutumia njia hii, kwa hiyo pamoja na kutoa
maelezo ya jinsi ya kutumia, sisi hatumshauri mtu kutumia njia hiyo.
Nani anaweza kutumia njia ya kalenda
Moja, Wanawake walioko tayari
kuchukua miezi 3 hadi 6 kupima vipindi vyao vya hedhi kabla ya kutumia njia
hiyo.
Pili, Wanawake walio na mzunguko wa hedhi ambayo
urefu wake haubadiliki.
Tatu, Wanawake wanaojua
hisabati vizuri sana.
Kwa
hiyo, kabla ya kutumia njia
hiyo, ni vyema kwa mwanamke kuandaa kalenda inayoonesha siku yake ya
kwanza
kutoa damu ya hedhi kila mwezi kwa kipindi cha miezi 3 hadi 6. Hii
itamsaidia kujua lini mayai yake yalipevuka. Njia hii inamsaidia zaidi
mwanamke aliye na
mzunguko wa hedhi wa siku 28, na hutegemea kufahamu kuwa yai la mwanamke
hupevuka siku 14 kabla hajaingina kwenye hedhi.
Kwa mfano;
1. Kama unaanza kuingia katika hedhi
tarehe 1 Juni (na una mzunguko wa hedhi wa siku 28), basi kuna uwezekano mkubwa
utaingia kwenye kipindi kipya cha hedhi tarehe 29 Juni. Kwa hiyo yai lako litapevuka siku 14 kabla
kwenye tarehe 15 Juni. Kwa hiyo, kuna
uwezekano mkubwa wa kwako wewe kupata mimba kama unafanya mapenzi karibu na
tarehe hii, kuanzia tarehe 14 Juni hadi 16 Juni. Kwa hiyo kuepukana na kupata mimba, usifanye
mapenzi kati ya tarehe hizo. Lakini
lazima ukumbuke kuwa mbegu za kiume zinaweza kuishi ndani ya mwili wa mwanamke
kwa siku 7, kwa hiyo ili kuwa na uhakika Zaidi ya kuepukana na kupata mimba,
una takiwa kutokufanya mapenzi kuanzia tarehe 8 hadi 16 Juni.
2. Katika mfano mwingine, kama
unaanza kuingia katika hedhi tarehe 13 Juni (na una mzunguko wa hedhi wa siku
28), basi kuna uwezekano mkubwa utaingia kwenye kipindi kipya cha hedhi tarehe
11 Julai. Kwa hiyo yai lako litapevuka
siku 14 kabla kwenye tarehe 28 Juni. Kwa
hiyo, kuna uwezekano mkubwa wa kwako wewe kupata mimba kama unafanya mapenzi
kati ya tarehe 27 Juni na 29 Juni. Ili
kuepukana na kupata mimba, usifanye mapenzi kati ya tarehe hizo. Kwa usalama zaidi, usifanye mapenzi kuanzia
21 hadi 29 Juni.
3. Katika mfano mwingine, kama baada
ya kuandaa kalenda kuonesha mzunguko wako wa hedhi wa miezi 3 hadi 6 iliyopita,
unagundua kuwa mzunguko wako ni wa siku 33 badala ya siku 28, basi kifuatacho
ni kweli: kama unaanza kuingia katika
hedhi tarehe 1 Juni basi kuna uwezekano mkubwa utaingia kwenye kipindi kipya
cha hedhi tarehe 4 Julai. Kwa hiyo yai
lako litapevuka kwenye tarehe 20 Juni (Siku 14 kabla ya tarehe 4 Julai). Kwa hiyo, kuna uwezekano mkubwa wa kwako wewe
kupata mimba kama unafanya mapenzi kati ya tarehe 19 na 21 Juni. Ili kuepukana
na kupata mimba, usifanye mapenzi kati ya tarehe hizo. Kwa usalama zaidi, usifanye mapenzi kuanzia 13
hadi 21 Juni.
4. Katika mfano mwingine, kama baada
ya kuandaa kalenda kuonesha mzunguko wako wa hedhi wa miezi 3 hadi 6 iliyopita,
unagundua kuwa mzunguko wako ni wa siku 26 badala ya siku 28, basi kifuatacho
ni kweli: kama unaanza kuingia katika
hedhi tarehe 1 Juni basi kuna uwezekano mkubwa utaingia kwenye kipindi kipya
cha hedhi tarehe 27 Juni. Kwa hiyo yai
lako kitapevuka kwenye tarehe 13 Juni (Siku 14 kabla ya tarehe 27 Juni). Kwa hiyo, kuna uwezekano mkubwa wa kwako wewe
kupata mimba kama unafanya mapenzi kati ya tarehe 12 na 14 Juni. Ili kuepukana na kupata mimba, usifanye
mapenzi kati ya tarehe hizo. Kwa usalama
zaidi, usifanye mapenzi kuanzia 6 hadi 14 Juni.
Faida ya kutumia njia hiyo
MOJA, Haina madhara yeyote ya
kimwili.
Matatizo yanayoweza kujitokeza
MOJA, Njia ya kalenda si kinga dhidi
ya virusi vya UKIMWI na magonjwa mengine ya zinaa.
PILI, Njia hii ni ngumu na inahitaji
wanawake kuwa wastadi katika hisabati, na kuwa waangalifu sana kuandika au
kukumbuka tarehe ya kuanza kipindi chao cha hedhi cha mwisho.
TATU, Huchukua muda mrefu (miezi 3
hadi 6) kufahamu urefu wa mzunguko cha hedhi.
TATU, Mzunguko wa hedhi huweza
kubadilika wakati wowote kufuatana na mabadiliko katika mwili. Hii huweza kusababisha tarehe ya yai kupevuka
kuwahi au kuchelewa, kwa hiyo mwanamke huweza kujiweka katika hatari ya kupata
mimba bila kufahamu.
NNE, Ili njia hii iwe na uhakika,
mwanamke hawezi kufanya mapenzi katika siku zake 9 kila mwezi ambapo kuna
uwezekano wa yeye kupata mimba. Kwa hiyo
njia hii inahitaji uwezo mkubwa wa kujidhibiti na hufanya kazi vizuri iwapo mwanaume
namwanamke wamekubaliana kufanya hivyo kwa pamoja, na mwanaume anamsaidia
mwanamke kuhesabu au kuandika urefu wa mzunguko wake wa hedhi.
0 comments:
Post a Comment