Kipindupindu ni ugonjwa wa kuharisha na kutapika unaosababishwa na vimelea vya bacteria
vinavyoitwa kwa lugha ya kitaalam “Vibrio cholera”.
CHANZO CHA UGONJWA
•
Vimelea vilivyomo kwenye kinyesi na matapishi ya mgonjwa wa kipindupindu.
•
Vimelea vilivyomo kwenye kinyesi cha mtu bila yeye binafsi
kuonyesha dalili zozote za ugonjwa.
DALILI ZA UGONJWA WA KIPINDUPINDU.
Mgonjwa wa Kipindupindu huwa na dalili
zifuatazo:
•
Kuharisha mfululizo au mara kwa mara bila tumbo kuuma ambako
kunaweza kuambatana na kutapika.
•
Kinyesi au matapishi huwa ya maji maji yasiyo na harufu, yanayofanana
na maji yaliyooshewa mchele.
•
Kusikia kiu sana, macho kudidimia na ngozi kusinyaa ambavyo
hutokana na upungufu wa maji mwilini.
•
Kuishiwa nguvu, kuhema haraka haraka na kulegea. Hali hii
hutokana na upungufu wa maji na madini mwilini.
KIPINDUPINDU KINAVYOENEA.
•
Kula chakula au kunywa kinywaji chochote kilicho na vimelea vya ugonjwa
wa kipindupindu kwa mfano:-
-
Kunywa maji yasiyochemshwa.
-
Kula chakula kilichoandaliwa katika mazingira ambayo siyo safi.
-
Kula matunda yasiyooshwa kwa maji safi na salama.
-
Kunywa pombe za kienyeji zilizoandaliwa katika mazingira machafu
au kunywea katika vyombo vichafu.
-
Kula mboga za majani, kachumbari na saladi bila kupikwa au kuziosha
kwa maji safi na salama.
•
Kula chakula au kumlisha mtoto bila kunawa mikono kwa sabuni na
maji safi na salama yanayo tiririka.
•
Kuosha au kuhudumia mwili wa mtu aliyekufa kwa ugonjwa wa kipindupindu bila
kujikinga.
•
Kunawa mikono kwenye chombo kimoja kwa mfano ndani ya bakuli au beseni
kabla ya kula chakula.
•
Kutotumia choo au utupaji ovyo wa kinyesi.
•
Kutonawa mikono baada ya kutoka chooni.
•
Kuweka mazingira katika hali ya uchafu mfano kutupa taka ovyo
bila kuzingatia kanuni za afya..
•
Kula vyakula vilivyopoa na visivyofunikwa.
•
Kutiririsha maji ya chooni ardhini na hivyo kusababisha uchafuzi
wa vyanzo vya maji na chakula.
· Inzi huchangia kueneza
ugonjwa wa kipindupindu kwa tabia zake za kutua chooni kwenye kinyesi, uchafu
na hata vyakula na vinywaji.
MADHARA YA KIPINDUPINDU
•
Hofu miongoni mwa jamii katika sehemu yenye mlipuko wa ugonjwa
wa kipindupindu.
•
Kifo kutokana na ukosefu wa maji na madini mwilini baada ya
kuharisha na kutapika sana.
•
Kushuka kwa uchumi kutokana na familia/jamii kuacha shughuli za
uzalishaji mali ili kumuhudumia mgonjwa na kushiriki katika misiba.
•
Serikali hutumia fedha nyingi kwa ajili ya dawa, posho kwa
watumishi katika kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu.
JINSI YA KUJIKINGA NA KIPINDUPINDU
•
Kujenga choo bora na kukitumia Ipasavyo
•
Kufunika tundu la choo na kufunga mlango baada ya matumizi yake.
•
Kunawa mikono kwa maji safi na salama kwa kutumia sabuni baada
ya:.
-
kutumia choo.
-
kumtawaza mtoto na kabla ya kula au kumlisha motto.
•
Kula chakula kikiwa bado moto na kufunika chakula kilichoandaliwa
tayari kwa kuliwa.
•
Kunywa maji yaliyochemshwa na kuhifadhiwa katika chombo kisafi
na salama.
•
Kusafisha vyakula vinavyoliwa vibichi (kama vile matunda na
mboga) kwa kutumia maji safi na salama yanayotiririka.
•
Kuhakikisha usafi wa mazingira ya vilabu/baa, wahudumu na vyombo
vitumikavyo. Pombe za kienyeji ziandaliwe kwa maji yaliyochemshwa.
•
Weka mazingira katika hali ya usafi.
· Kumbuka, kuchuja maji
yaliyochemshwa kunaweza kuchafua maji kwa kuingiza vimelea.Hivyo, chuja maji
kabla ya kuyachemsha.
KUHUDUMIA MGONJWA
Mgonjwa wa kipindupindu hupoteza maji mengi na
madini muhimu mwilini anapoharisha na kutapika. Ili kuokoa maisha ya mgonjwa ni
muhimu kuchukua hatua zifuatazo:
•
Mpe mgonjwa dawa ya mchanganyiko wa sukari na chumvi(ORS), maji,
uji mwepesi, supu nk. mara kwa mara.
•
Mpeleke mgonjwa haraka iwezekanavyo katika kituo cha afya/zahanati/
hospitali au kituo cha kutibu kipindupindu kilicho karibu nawe.
•
Matapishi na kinyesi cha mgonjwa ni hatari kwa afya yako. Kwa
hiyo nguo na vitu vingine vilivyochafuliwa na mgonjwa vilowekwe kwenye kemikali
maalumu (mfano Jik) au vichemshwe ili kuua vimelea vya kipindupindu na kasha visafishwe
kwa sabuni.
•
Ndugu waliokuwa wakiishi na mgonjwa au wale wanaomhudumia
wahakikishe wanapata dawa za kinga dhidi ya kipindupindu.
Angalizo:
Ni lazima wakati wote kuwa msafi ili kuzuia
vimelea vya ugonjwa visiingie kinywani kwako kwa njia zilizotajwa hapo juu.
Tahadhari:
Maiti ya mgonjwa wa kipindupindu ni hatari, usijishughulishe
na kuosha maiti hiyo bali izikwe haraka kwa kufuatwa ushauri wa wataalam wa
afya.
0 comments:
Post a Comment