HATUA ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini,
Zitto Kabwe kutaja hadharani mshahara wa Rais na Waziri Mkuu, imechukua
sura mpya baada ya Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE)
kulaani hatua hiyo na kuomba Spika Anne Makinda kuchukua hatua kwa vile
ni ukiukaji wa sheria.
Chama hicho kimeeleza kusikitishwa na kitendo hicho kufanywa na Mbunge
aliyehusika na upitishaji wa sheria hiyo huku wabunge wenyewe wakiwa
wakali pale wananchi na wadau mbalimbali wanapohoji mapato yao.
Katibu Mkuu wa Tughe Taifa, Ally Kiwenge alisema Dar es Salaam jana
kwamba pamoja na hatua hiyo kukiuka sheria ya kazi na uhusiano kazini
inayosema mshahara ni siri ya mwajiri na mwajiriwa, pia kitendo hicho si
ajenda ya wafanyakazi hivi sasa.
Alisema ajenda ya wafanyakazi kwa sasa ni kuona wabunge wanapigana kufa
kupona katika kuhakikisha kuwa mshahara wa mfanyakazi unaongezeka
kukidhi mahitaji ya mwezi mzima na kuwaondolea mzigo wa mikopo
inayowaandama.
“Huu si wakati wa wafanyakazi kutaka kujua mishahara ya Rais au
Waziri Mkuu, ajenda yetu kwa sasa ni kuona wabunge wanapigana ili
kuboresha mishahara ya wafanyakazi ili ukidhi mahitaji muhimu tofauti na
sasa,” alisema Kiwenge.
Alisema pamoja na hilo ni mkakati wa wafanyakazi sasa kuona wabunge
wanatumia muda wao uliosalia kabla ya Bunge kuvunjwa kuhakikisha mambo
makubwa mawili yanaingizwa katika Katiba mpya, moja ikiwa ni nafasi ya
mfanyakazi kikatiba ikoje na pia kuona Katiba mpya inasema nini juu ya
hatima ya maslahi ya wafanyakazi.
“Tunataka Katiba mpya itamke wazi juu ya mishahara ya wafanyakazi ili iwe ni ile inayokidhi haja,” alisema.
Aeleza kuwa ni jambo la kusikitisha kuona wabunge wanaanza kutaja
mishahara ya viongozi wa taifa hadharani kwa kudhani kuwa ndio njia
sahihi ya kuwasaidia Watanzania bila kujua kuwa hatua hiyo itasababisha
mgawanyiko wa matabaka na kuligawa Taifa, jambo ambalo ni la hatari.
“Sisi mishahara ya viongozi wote tunaifahamu na hata ya wabunge, lakini
sheria inasemaje juu ya kutangaza mshahara wa mtu hadharani? Wafanyakazi
wanaweza kuitaja lakini kwa vile wameandaliwa hawafanyi hivyo,
wanazingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi.
“Naamini kama wafanyakazi wangekuwa ni watu wa kukusanyana na
wangekuwa hawana maadili wangeweza kusema mengi ambayo yangeshangaza
jamii lakini hawafanyi mambo kwa kukurupuka au kuutafuta umaarufu usio
na msingi,” alisema.
Katibu Mkuu huyo wa Tughe alisema kwa kufuata mfano wa wafanyakazi,
viongozi wakiwemo wabunge watoe kauli za kujenga nchi na si zenye
kuashiria matabaka na ubaguzi, jambo linaloweza kusababisha migogoro
mikubwa na kuliingiza taifa katika machafuko yasiyo na tija,” alisema.
Alisema wabunge wafahamu pia kwamba suala la mishahara litaendelea
kubakia kuwa ni la mwajiri na mwajiriwa na ndio maana katika fomu au
nyaraka nyingine zinazoelezea majukumu ya wabunge suala la mishahara na
marupurupu yao haliwekwi wazi kwa vile ni siri kati yao na taasisi ya
Bunge kisheria.
POSTED BY:www.info@dirayetu.blogspot.com
Home / Uncategories / CHAMA CHA WAFANYAKAZI WA SERIKALI KUU(TUGHE) WAMJIA JUUMBUNGE WAKIGOMA KASKAZINI ZITTO KABWE!!
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment