Mafanikio na mikakati iliyofikiwa na Mahakama Kuu ya Tanzania 2013.

Pix 01 
Naibu Msajili Mwandamizi toka Mahakama Kuu ya Tanzania Mh. John Kahyoza akizungumza na waandishi wa habari (Hawapo pichani) leo jijini Dar es Salaam kuhusu mafanikio yaliyofikiwa na mahakama hiyo ikiwemo kuanzishwa kwa mfuko wa mahakama, kulia ni Afisa Habari wa Mahakama ya Tanzania Bi. Mary Gwera. Pix 02 
Naibu Msajili Mwandamizi toka Mahakama Kuu ya Tanzania Mh. John Kahyoza akielezea mikakati ya Mahakama hiyo kutumia mfumo wa TEHAMA ili kuongeza kasi ya uendeshaji wa mashauri, katikati ni Afisa Habari wa Mahakama ya Tanzania Bi. Mary Gwera na kulia ni Afisa Habari wa Idara ya mahakama.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.
Mahakama ya Tanzania ni moja kati ya Mihimili mitatu ya Dola, na majukumu yake makubwa kwa mujibu wa Katiba ni Kutafsiri sheria na kutolea maamuzi kesi mbalimbali zinazoletwa Mahakamani.
107A:- (1) Sura ya tano ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasomeka kuwa:
‘Mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa ni Mahakama.’
Kufuatia jukumu hili muhimu Mahakama imejiwekea dira ambayo ni; ‘Kutoa haki sawa kwa wote na kwa wakati.’
Hata hivyo; Mahakama ya Tanzania imekuwa ikikabiliwa na changamoto kadhaa likiwemo suala zima la uendeshaji wa shughuli zake za kila siku.
Hata hivyo Mahakama ya Tanzania,imefanikiwa kwa kiasi kikubwa, kufuatia hatua na michakato mbalimbali ambayo tayari imekwishafanyika na mingine ikiwa kwenye hatua nzuri yote yakiwa yanalenga katika kuboresha huduma ya utoaji haki nchini.
MAFANIKIO YALIYOFIKIWA NA MAHAKAMA YA TANZANIA.
i.            Kurejewa kwa Muundo wa Mahakama na kuandaa Muundo
mpya wa Utawala wa Mahakama uliopitishwa katika Sheria mpya ya Uendeshaji wa Mahakama (The Judicial Administration Act, No.4/2011). Kwa mujibu wa muundo huu Shughuli za Kiutawala na za Kimahakama zimetenganishwa, Mhe. Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania atasimamia shughuli za Mahakama tu, wakati Mtendaji Mkuu (Chief Court Administrator) atashughulikia masuala ya Kiutawala.  Muundo huu mpya tayari umeanza kutekelezwa rasmi katika mwaka wa fedha uliopita, 2012/2013. Hatua hii itaboresha na kuongeza ufanisi katika shughuli za utoaji haki nchini. 
Mchakato wa mabadiliko ya Muundo wa Mahakama ulianza miaka 16 iliyopita kufuatia ripoti ya Kikosi kazi kilichoongozwa na Mhe. Jaji Mark Bomani ambayo ilipendekeza kufanyika kwa mabadiliko ya Muundo wa Mahakama ili kuboresha ufanisi katika utendaji kazi wa Mhimili huu muhimu. 
ii.          Uanzishwaji wa Mfuko wa Mahakama chini ya Sheria ya
Uendeshaji wa Mahakama Na.4 ya mwaka 2011. Lengo la mfuko huu ni kuwezesha uendeshaji wa mashauri katika Mahakama za ngazi zote kwa kuboresha mfumo wa usikilizaji wa Mashauri katika Mahakama za ngazi zote kwa kuboresha mfumo wa usikilizaji Mashauri na ununuzi wa vitendea kazi. 
Kuanzishwa kwa Mfuko wa Mahakama kumesaidia kuongezeka kwa bajeti ya Mahakama kutoka bilioni 20 kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2011/12 kuwa bilioni 30 kwa bajeti ya 2012/13 na kuwa bilioni 140 kwa bajeti ya mwaka 2013/14. 
Aidha, Mfuko umesaidia kuharakisha kasi ya usikilizaji wa mashauri na idadi ya vikao vya Mahakama. Vikao vya Mahakama ya Rufani vimeongezeka kutoka 22 kwa mwaka wa fedha 2012/13 hadi 30 kwa mwaka huu wa fedha. Huku rufaa zilizomalizika zikiongezeka kutoka 585 hadi 634 hadi kufikia mwezi wa Septemba 2013. Mahakama ya Rufani inakusudia kumaliza rufaa 1200 kwa mwaka 2014. Mahakama Kuu yenye kanda 13 na inatarajia kumaliza mashuri 11000 wakati kwa mwaka jana illimaliza mashauri 5600 na kutolea maamuzi mashauri. Mahakama Kuu hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu mahakama tayari ilikuwa imepokea mashauri mapya 1402 na kumaliza mashauri 1781 kati ya hayo 936 akiwa ya jinai na 489. yakiwa ya madai na yaliyobakia yakiwa ni mashauri ya jinai yaliko katika masjala za kawaida. 
Utaratibu huu pia umesaidia kuharakisha upatikanaji wa nakala za mwenendo wa Mashauri na hukumu pamoja na kuwarahisishia kazi Majaji na mahakimu wanaosikiliza kesi katika Mahakama hii. Mfuko huu pia utasaidia katika kuboresha miundombinu ya Mahakama hususani Majengo, Vitendea kazi, maslahi ya Watumishi n.k.
Mfuko umewezesha kufufuliwa kwa vikao vya kusukuma kesi na mashauri. Vikao hivi ni muhimu kwani hukusanya wadau na kujadili mbinu za kupunguza mashauri yenye muda mrefu mahakamani. Bajeti ya kuendesha vikao hivyo kwa ngazi mbali mbali za mahakama imetengwa na tayari vikao hivyo vimeanza kufanyika. 
iii.        Upatikanaji wa fedha za O.C kadri ya Bajeti ilivyopangwa. 
iv.         Uanzishwaji wa zoezi la nchi nzima la utunzaji bora wa kumbukumbu, ukusanyaji wa Takwimu na matumizi yake na kuingiza mpango kamili wa matumizi ya TEHAMA kwenye shughuli.
v.           Kufanyika kwa vikao vya Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu (Court sessions kwa asilimia 100).
vi.         Kuanzisha programu maalum ya uondoshaji wa mashauri ya muda mrefu Mahakamani.
vii.       Kukamilishwa kwa ujenzi wa jengo la Mahakama Kuu Bukoba na kuzinduliwa rasmi na Mhe. Rais Jakaya M. Kikwete mnamo tarehe. 25, Julai, 2013.
viii.     Uboreshwaji wa posho za Wazee wa Baraza kutoka 1,500 hadi kufikia Shilingi 5000 kwa kila shauri linalohitimishwa.
ix.         Kuajiri jumla ya Mahakimu 300 wahitimu wa Shahada ya kwanza ya Sheria na kuwasambaza kwenye vituo vya Mahakama za Mwanzo katika wilaya 102. Hatua hii imesaidia tatizo lililokuwepo la upungufu wa Mahakimu wa  Mahakama za Mwanzo.
x.           Miradi ya ujenzi.
Aidha, Mahakama ya Tanzania inaendelea na mchakato wa kuanza kwa ujenzi wa majengo ya Mahakama katika ngazi mbalimbali.
·        Ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.
·        Ujenzi wa Mahakama Kuu katika Mikoa tisa; ambayo ni Mtwara, Kigoma, Mara, Lindi, Morogoro, Manyara, Singida, Shinyanga na Dodoma.
·        Kuanza kwa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Bunda, Bariadi, Nkasi, Bukombe, Bagamoyo na Kilindi.
·        Kuanza kwa ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Buguruni, Kawe, Kigamboni, Makuyuni, Maili Moja, Songea, Mpanda, Terrati, Mtowisa, Sangabuye, Ilolankulu, Mwanga, Mangaka, Makongolosi, Itigi, Machame, Mkomazi, Gairo, Kiagata, Lukuledi na Longido; pamoja na ujenzi wa Mahakama za Mwanzo Ngorongoro, Kolekero, Magoma na Bomang’ombe. 
MIKAKATI YA MAHAKAMA
·        Dhamira ya Mahakama ni kuondoa mashauri/kesi zote zenye umri zaidi ya miaka miwili (2).
·        Kuboresha takwimu za mashauri/ kesi zilizopo Mahakamani.
·        Kuboresha na kusimamia masjala.
·        Kudhibiti kalenda za vikao ‘Court Sessions’.
·        Kuweka “Benchmarks” kwa maofisa wa Mahakama katika kumaliza mashauri kwa wakati.
·        Kuboresha kanuni za kuendesha mashauri.
·        Kuimarisha utawala na usimamizi wa mashauri.
Pamoja na Mafanikio tajwa; jitihada za dhati bado zinaendelea kufanyika katika kuhakikisha kuwa Mahakama inajengewa mazingira bora ya kufanyika kazi, kufanikisha jukumu la Utoaji Haki kwa wakati nchini.
Asanteni kwa kunisikiliza.
Contact; Mary Gwera. (0756 866533/marygwerac@yahoo.com)
                Afisa Habari
               Mahakama ya Tanzania
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment