KILA MJUMBE BUNGE LA KATIBA KUONDOKA NA SHILINGI 300,000/- KWA SIKU...

Ukumbi utakaotumika kwa Bunge la Katiba ukiwa tayari umekamilika.

Bunge Maalumu la Katiba litafunguliwa rasmi Jumatano ijayo ya Februari 26, mwaka huu likiwa na wajumbe 629 na imethibitishwa kuwa kila mjumbe atalipwa Sh 300,000 kwa siku.

Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Thomas Kashillilah, aliwaambia waandishi wa habari hayo jana ndani ya ukumbi mpya wa Bunge, walipoingia kwa mara ya kwanza ndani ya ukumbi huo kuangalia mfumo wa kisasa wa sauti na mambo mengine.

Dk Kashillilah akiwa amefuatana na Katibu Msaidizi wa Baraza la Wawakilishi na maofisa wengine wa Bunge la Jamhuri, alisema ratiba ya mkutano wa Bunge Maalumu la Katiba inaonesha kuwa litazinduliwa rasmi Februari 26, ingawa kesho litaanza kwa mkutano wa maelekezo ya ukaaji na jiografia ya ukumbi.

Alisema ratiba imeanza jana kwa kusajili wajumbe hao, kazi ambayo inaendelea leo na kesho asubuhi kutafanyika mkutano huo wa maelekezo na saa 8 mchana, kutasomwa tangazo la kuitisha Bunge Maalumu, uchaguzi wa Mwenyekiti wa Muda na kuandaa na kupitisha Kanuni za Bunge hilo.

"Mwenyekiti wa muda atachaguliwa kwa utaratibu maalumu uliowekwa na Katibu wa Bunge la Muungano na wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, ambao utaratibu tutatoa kesho (leo). Mwenyekiti wa Muda atasimamia kuchaguliwa kwa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba," alisema Dk Kashillilah.


Alisema Mwenyekiti wa Muda pia atasimamia kuandaliwa kwa Kanuni, na baada ya kupatikana kwa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti, ndipo atateuliwa Katibu na Naibu Katibu wa Bunge hilo kwa mujibu wa sheria kwani yeye na mwenzake wa Zanzibar, kwa sasa wanasimamia tu mchakato huo.

Alisema kabla ya Mwenyekiti na Makamu wa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba kuanza kazi zao, kwanza watasubiri Rais kuwaapisha Katibu na Naibu Katibu, na ndipo Katibu wa Bunge hilo, atakuja kumwapisha Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti; na Mwenyekiti kuwaapisha wajumbe wake.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Jumatano na Alhamisi zitatumika kwa kikao cha kazi cha kuandaa Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalumu, wakati Ijumaa itakuwa siku ya kupitisha Azimio la kuridhia Kanuni za Bunge Maalumu, uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti na kiapo cha Katibu na Naibu Katibu wa Bunge Maalumu (ingawa hiyo siyo shughuli ya Bunge Maalumu).

Dk Kashillilah alisema Jumamosi, itakuwa ni kiapo cha Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu na kufuatiwa na kiapo cha wajumbe wa Bunge Maalumu ambacho kitaendelea hadi Jumapili.

Aidha, Jumatatu pia kutakuwa na kiapo cha wajumbe saa 4 asubuhi na kuunda Kamati za Bunge Maalumu, kabla ya ufunguzi rasmi wa Bunge utakaofanywa na Rais Jakaya Kikwete, saa 10 jioni.
Katibu huyo wa Bunge la Muungano alisema uwasilishwaji wa Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalumu itakuwa ni Jumanne na Jumatano ya Februari 26, mjadala wa kupitisha Rasimu ya Katiba utaanza hadi Aprili 30, mwaka huu.

Kwa mujibu wa kifungu cha 25 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Bunge Maalumu litakuwa na mamlaka ya kujadili na kupitisha masharti ya Katiba inayopendekezwa na kutunga masharti ya Mpito na masharti yatokanayo kama Bunge Maalumu litakavyoona inafaa.

Ili Katiba inayopendekezwa ipitishwe katika Bunge Maalumu la Katiba, itahitajika kuungwa mkono kwa wingi wa theluthi mbili ya idadi ya wajumbe wote wa Bunge Maalumu kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Zanzibar.

Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, muda ambao Bunge Maalumu litajadili Rasimu ya Katiba hautazidi siku 70 kuanzia tarehe ambayo Bunge Maalumu lilipoitishwa, hivyo uhai wa Bunge hili unatarajiwa kukoma Aprili 30, mwaka huu, lakini unaweza kuongezwa kwa mashauriano kati ya Mwenyekiti wa Bunge Maalumu na Makamu wake kwa ridhaa ya Rais kwa kushauriana na Rais wa Zanzibar.

Akizungumzia gharama za ukarabati wa jengo na miundombinu mingine, Dk Kashillilah alisema ni Sh bilioni 8.2, ambazo zote zimetoka katika Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2013/14 ambayo ilishapitishwa na Bunge ikiwamo posho za wajumbe ambazo ni Sh 300,000 kwa siku kwa mjumbe.
"Fedha zote hizo zilikuwapo katika Bajeti ya Serikali iliyopitishwa Juni mwaka jana, kwa hiyo siyo suala geni. Na zimetumika katika ukarabati wa jengo la ukumbi, vifaa vikiwamo viti 678 ambavyo gharama yake ni dola za Marekani milioni moja," alifafanua Katibu wa Bunge.

Alisema katika posho, wajumbe watalipwa posho ya kawaida ya Serikali ya siku (haikutaja), lakini alisema kutawakuwa na kodi maalumu ambayo itahusisha posho ya kikao, usafiri, malipo kwa madereva na mengineyo, ambayo itakuwa ni Sh 220,000. Hivyo posho ya kawaida itakuwa Sh 80,000 ukijumuisha na Sh 220,000 unapata Sh 300,000 watakazolipwa kwa siku.

Alisema Bunge Maalumu litajumuisha wajumbe 629 ambao ni wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 357, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi (BLW) 82 na wajumbe wa kuteuliwa kwa uwakilishi 201.

Aliongeza katika idadi hiyo, unapunguza wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ambao pia ni wajumbe wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sita, Mjumbe wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa uteuzi wa Rais wa Zanzibar, wabunge wawili waliofariki na nafasi mbili za uteuzi wa Rais zilizo wazi, unapata wajumbe 629, ambao zaidi ya 120 walikwisha jisajili hadi kufikia jana mchana.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment