MVUA YAUA,300 HAWANA MAKAZI HAI!!

Mkuu wa Wilaya ya Hai, Novatius Makunga.
 
Mtu mmoja amefariki na wengine zaidi ya 300 hawana mahali pa kuishi katika Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro baada ya mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali kubomoa nyumba zao.
Mbali na hasara hiyo, mvua hizo iliyonyesha kwa takribani siku nne sasa, pia zimeharibu vibaya zaidi ya ekari 60 za mazao ya chakula.

Familia hizo kwa sasa zinaishi kwa kutegemea hisani kutoka kwa wasamaria wema.

Habari zilizopatikana jana na baadaye kuthibitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Hai, Novatius Makunga, zilileza kuwa tayari serikali kupitia Ofisi
ya Waziri Mkuu Kitengo cha Maafa, kimetoa msaada wa chakula tani 1.5 kwa ajili ya kuhudumia waathirika wa tukio hilo.

Aidha, aliyefariki dunia kutokana na adha hiyo ametajwa kuwa ni John Mboya (45), dereva wa pikipiki mkazi wa kijiji cha Kwatito.

Dereva huyo wa bodaboda anadaiwa alifariki dunia juzi baada ya kuzidiwa nguvu na kusombwa na maji.

“Kutokana na hali yenyewe ilivyo,tayari tumeanza kupokea misaada ya kijamii kwa ajili ya kusaidia waathirika wa mvua hizo ambazo zimeathiri
sana wananchi wa kata ya Machame Kusini na Machame-Weruweru na maeneo mengine ya Hai mjini.

Kaya zote zilizoathiriwa na mvua hizo hivi sasa zinahifadhiwa kwa majirani kutokana na makazi yao kubomolewa na mvua,” alifafanua Makunga.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Wilaya, tathmini ya awali ya uharibifu wa mali za wakazi hao, inaonyesha kuwa kinahitajika kiasi cha zaidi ya Sh. milioni 46.8 kugharimia vifaa vya ujenzi yakiwamo mabati ili wananchi hao warejee katika makazi yao ya asili.

Makunga aliongeza kuwa msikiti wa Mudio ulioko Tarafa ya Masama uliezuliwa.

Makunga alisema kufuatia hali hiyo, Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Regnald Mengi, ameahidi kutoa misaada ya kijamii kwa waathirika hao kupitia kampuni tanzu ya vinywaji baridi ya Bonite Bottlers Limited ya mjini Moshi.

“Bado tunaendelea kupokea misaada na ahadi za kusaidia waathirika wa mvua hizo na Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Kilimanjaro (KNCU)
kimeahidi kutoa magunia 10 ya mahindi, matano ya maharage na mafuta ya chakula huku kampuni ya Usagishaji nafaka ya Mono Ban ya Arusha, ikiahidi kutoa msaada wa tani mbili za unga wa nafaka,” alisema Makunga.

Katika hatua nyingine, serikali imesema itaendelea kutoa msaada wa chakula kwa waathirika hao kwa mwezi mmoja hadi hapo wananchi hao watakaporejea katika makazi yao ya asili.

Alivitaja baadhi ya vijiji vilivyoathirika zaidi na mvua hizo kuwa ni Kwatito, Mijungwani, Shirimgungani, Mijongweni na Ngosero.Vingine ni Kilimambogo, Kikavu Chini na Lerai.

Hata hivyo, habari zilizolifikia NIPASHE baadaye zilidai kuwa umetokea uharibifu wa madarasa matano, ofisi ya mwalimu na nyumba tatu za walimu wa Shule ya Sekondari Kibohehe inayomilikiwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata).

Baadhi ya waathirika hao, Gerald Massawe na Ambros Kihimisho, waliiambia NIPASHE kuwa mvua hizo zimeawaathiri kwa kiasi kikubwa kwa kuwa hivi
sasa wanalazimika kulala nje huku familia zao zikishindia mlo mmoja kwa siku.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment