PCT walalamikia kukosa uwakilishi Bunge la Katiba!!

Mwenyekiti wa Makanisa ya Kipentekoste Tanzania, Askofu David Butenzi, akizungumza na waandishi wa habari (hawako pichani), wakati Baraza la Maaskofu wa kanisa hilo lilipotoa tamko lao kuhusu kutopata mwakilishi wao katika Bunge la Katiba pamoja na kupeleka orodha ya majina katika Ofisi ya Rais. Wengine kutoka kushoto ni Askofu Zakaria Kakobe, Katibu Mkuu wa makanisa hayo, Askofu David Mwasota na Askofu Sebastian Mcheri.
Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania (PCT), limesema limefedheheshwa na kusikitishwa kwa kunyimwa uwakilishi wa  kushiriki katika Bunge maalum la Katiba licha ya kuwasilisha  majina ya wajumbe wake.
Limesema kitendo cha kushindwa  kupewa fursa ya kushiriki katika Bunge hilo,  ni kuwanyima haki za msingi Watanzania wengi wanaowakilishwa na Baraza hilo, kama ilivyo kwa Watanzania wengine.

Akisoma tamko la baraza hilo mbele ya waandishi wa habari jana, baada ya kufikiwa katika mkutano ulioshirikisha Maaskofu wakuu wa Madhehebu ya Kipentekoste jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa PCT,  David Mwasota,  alisema wameamua kutoa tamko hilo ili kuonyesha namna ambavyo wamesikitishwa na kitendo hicho.

“Tumewaita leo (jana) ili mtusaidie kufikisha masikitiko yetu kwa viongozi, Watanzania  na waamini wa Kipentekoste kutokana na kitendo cha serikali yetu tunayoiheshimu, kuipenda na kuiombea, kwa kutubagua na kututenga katika bunge maalum la Katiba, huku  tukiwa ni  miongoni mwa taasisi kubwa za kidini na makundi mengine ya kijamii,” alisema na kuongeza:

“Ikumbukwe kuwa hivi karibuni Rais aliagiza makundi mbalimbali ya kijamii na taasisi za kidini kupendekeza majina ya watu wanaoona wanafaa kuchaguliwa kushiriki katika bunge maalum la Katiba na kwa kuzingatia wingi wa wanachama wetu tulipendekeza majina  tisa ya watu tulioona wanafaa kutuwakilisha, lakini cha kushangaza hakuna hata mmoja aliyeteuliwa.”

Aidha, aliongeza kuwa ikiwa serikali itaendelea kunga`ng`ania msimamo wake wa kutaka wajumbe wa baraza la PCT wasihusike katika Bunge hilo, Baraza litaitisha mkutano mkuu wa dharura wa kitaifa utakaojumuisha maaskofu wote wa kitaifa, Kanda na jimbo, mitume na manabii na  wachungaji zaidi ya 30,000 ili kutafakari kwa pamoja na kuamua hatua za kuchukua.

Mjumbe wa TCP ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Kanisa la  Full Gospel  Bible Fellowship,  Zacharia Kakobe,  alisema Katiba ni haki ya Watanzania wote hivyo haoni sababu ya wengine kubaguliwa.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment