BARAZA LA MADAKTARI LATWISHWA MZIGO KUHAKIKISHA WALIOTUPA VIUNGO VYA BINADAMU WANACHUKULIWA HATUA KALI!!


Tukio la utupaji wa viungo vya binadamu jalalani, linalodaiwa kufanywa na  Chuo cha Kimataifa cha Matibabu na Teknolojia (IMTU) cha Dar es Salaam,  linadaiwa kuandika historia mbaya nchini.

Wakati serikali ikiendelea kuchunguza tukio hilo, ikiwemo kuunda tume nyingine chini ya Wizara ya Afya na Ustawi, kujiridhisha kabla ya hatua kuchukuliwa,  Baraza la Madaktari limetwishwa mzigo wa kuhakikisha linachukua hatua kali kwa watakaobainika kuhusika na kitendo hicho. 
Imeeleza kwamba katika miaka  yote, tangu mafunzo ya udaktari yaanze kutolewa nchini, halijawahi kutokea tukio kama hilo.
Serikali imetumia nafasi hiyo kuonya vyuo vingine, kwa kusema  jambo hili ni la kusikitisha, la aina yake katika historia ya mafunzo ya udaktari tangu yaanze nchini takribani miaka 40 sasa. 
"Pia tunatoa onyo kwa vyuo vingine, mafunzo haya tumeanza miaka 40 iliyopita lakini haijawahi kutokea kitu cha aina hii, ni mara ya kwanza ni jambo la kusikitisha sana," alisema Naibu Waziri wa Wizara ya Afya na Ustawi, Dk Steven Kebwe.
Naibu Waziri aliwaambia waandishi wa habari kuwa kitendo hicho cha kutupa viungo vya binadamu  hadharani,  si jambo la kawaida, ni la uvunjifu wa haki za kibinadamu.
Alisema tangu Tanzania ipate uhuru wake,  haijawahi kutokea tukio kama hilo, ambalo linatia hofu miongoni mwa wanajamii.
Katika kile kinachodhihirisha chuo hicho kung’ang’aniwa, kabla ya kuamua hatua za kuchukua dhidi yake, Wizara hiyo yenye dhamana ya afya, pia imeunda kamati ya watu 15 kwa ajili ya kuchunguza tukio hilo. 
Kamati hiyo ya wizara iliyopewa siku saba kukamilisha kazi, imeundwa kukiwa na tume nyingine iliyoundwa na Polisi Kanda ya Dar es Salaam, kuchunguza sakata hilo la kutupwa viungo katika maeneo ya Bonde la Mbweni Mpiji, Bunju jijini Dar es Salaam. 
Dk Kebwe aliwaambia waandishi wa habari kwamba kamati hiyo ya wizara itafanya kazi yake kwa siku saba kuanzia juzi. Inajumuisha wataalamu mbalimbali kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu, Polisi na Wizara ya Afya na Ustawi.
Aidha, alisema zipo sheria zinazoelekeza namna ya kuteketeza miili hiyo baada ya kumalizika kwa kazi yake. 
“Lakini inasikitisha kuona miili hiyo ilitelekezwa na watu wanaojua maadili ya kazi ya udaktari,” alisema.
Alisema kwa kuwa madaktari huwa wanakula viapo baada ya kumaliza mafunzo yao, Baraza la Madaktari nchini linatakiwa kuhakikisha linachukua hatua kali kwa watakaobainika kuhusika na kitendo hicho.
Timu iliyoundwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,  imejielekeza kuja na majibu kadhaa,  ikiwa ni pamoja na kufahamu idadi kamili ya watu wenye viungo hivyo. 
Ikiwa na watu saba akiwemo  Mkemia Mkuu wa Serikali, itakuja na majibu yanayofafanua viungo hivyo ni vya muda gani na zilitumika kemikali gani kuvikausha.
Pia, jopo hilo litabaini kama ipo sheria na ni ipi  inavunjwa. Wataalamu hao wanalenga kubaini, pia kama upo uzembe katika kulinda viungo vya binadamu na vinapatikanaje kwa ajili ya mazoezi.
Katika sakata hilo, lililovuta hisia za watu na kuzua mjadala mitaani na kwenye mitandao ya kijamii, watu wanane wakiwemo madaktari wa IMTU, walikamatwa  na Polisi kwa mahojiano, wakituhumiwa kuhusika  katika  utupaji viungo vya binadamu jalalani.
Kwa mujibu wa Polisi, mifuko ipatayo 85 yenye vichwa, miguu, mikono, moyo, mapafu, vifua na mifupa ya aina mbalimbali ya binadamu, ilikutwa maeneo ya bonde la Mbweni Mpiji  eneo la Bunju jijini Dar es Salaam.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment