BUNGE LA KATIBA NI HALALI-PINDA!!

 

WAZIRI Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, amesema mchakato wa Bunge la Katiba unaoendelea ni halali na upo kisheria.

Bw. Pinda aliyasema hayo Mjini Sumbawanga, mkoani Rukwa jana wakati akizungumza na mamia ya waumini na viongozi waliohudhuria ibada ya uzinduzi wa Dayosisi Mpya ya Ziwa Tanganyika ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

Ibada hiyo iliambatana na tukio la kuwekwa Wakfu Askofu Ambele Mwaipopo aliyeteuliwa kuongoza dayosisi hiyo ambapo Bw. Pinda, alilazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya Askofu huyo kutaka maoni ya iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba yaheshimiwe na wajumbe wa Bunge la Katiba.

Bw. Pinda alisema, "Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na tume si Katiba bali ni mawazo yaliyokusanywa yanayopaswa kupitiwa na chombo kingine cha kisheria ambacho ni Bunge Maalumu la Katiba hivyo mchakato huo ni halali," alisema.

Alisema muda ambao tume hiyo ilipewa haukuwa mrefu hivyo isingekuwa rahisi kwa wajumbe wake kuzingatia kila eneo ambalo linagusa maisha ya Watanzania.

"Mfano mzuri ni suala la ardhi ambalo halikuelezwa vizuri katika rasimu lakini hivi sasa limefafanuliwa jinsi ardhi inavyoweza kumnufaisha Mtanzania kwenye kilimo, ufugaji, uvuvi na rasilimali misitu," alisema Bw. Pinda.

Aliongeza kuwa, kinachowachanganya Watanzania ni suala la Serikali mbili au tatu lakini katika makabrasha ya tume ambayo wajumbe wote walipewa, suala la Muungano halikupewa kipaumbele na Watanzania wengi waliotoa maoni yao.

"Kulikuwa na masuala makubwa sita, suala la ukiukwaji wa haki za binadamu ndilo lilikuwa namba moja, pia kuna matatizo ya huduma za jamii, suala la Muungano lilichangiwa na kundi dogo," alisema.

Alisema kwa mujibu wa takwimu za tume, watu waliotaka Muungano wa Serikali tatu ni kati ya asilimia 12 na 13 hivyo haiwezekani asilimia hizo ambazo zinataka Serikali tatu, zionekane ni maoni ya Watanzania wote.

Bw. Pinda alisema, ili kukidhi shauku ya wengi, yuko radhi ifanyike kura mahususi ya kuwaomba Watanzania waseme kama wanataka Muungano na uwe wa aina gani.

"Baba Askofu amesema tusitishe Bunge la Katiba, sababu hasa ya kusitisha ni ipi? Je, sote tunajua hoja iliyowafanya wenzetu watoke nje na kususia vikao...katika muda wa kuchangia kulikuwa na dakika 40 za wengi, 20 za wachache lakini wakapewa dakika 30.

"Muda huo ni mwingi mno kama hujaweka mchango wako kwenye maandishi badala yake, sote tulishuhudia kukashifiana na kejeli, nawaomba Maaskofu, wachungaji na viongozi wengine wa dini waliohudhuria uzinduzi huu, muendelee kuuombea mchakato unaoendelea ili uweze kuisha vizuri," alisema.

Alimuomba Askofu Mwaipopo, apokee jukumu hilo kwa mikono miwili akimuahidi kuwa, Serikali itasaidiana naye kuwaongoza Watanzania walioko kwenye dayosisi yake.

Dayosisi hiyo inahusisha Mikoa ya Rukwa na Katavi ambapo Bw.Pinda alisisitiza kuwa, changamoto zinazoikabili dayosisi ni nyingi ikiwemo ya malezi ya vijana na watoto, tabia ya watu kutopenda kufanya kazi hasa vijana, kukosekana injili kwenye maeneo wanayoishi wafugaji na suala la imani za ushirikina.

"Asilimia kubwa ya Watanzania ni vijana ambao ndio Taifa la leo lakini ukiangalia mavazi ya vijana wa kike (vimini) na wakiume (mlegezo), hutamani kuwaangalia mara ya pili.

"Msingi mkubwa wa kuwabadilisha ni malezi ya kiroho hivyo changamoto ni kubwa ya kufikisha neno la Mungu kwa wafugaji ambao ni wengi eneo hili lakini hawana muda wa kuabudu na wengi wao hawalijui neno la Mungu," alisema.

Alisema changamoto kubwa zaidi ni kubadili mtazamo wa jamii kuhusu Mkoa wa Rukwa hasa kwenye suala la ushirikina akimuomba washirikiane kupiga vita imani hizo potofu kwani zinachangia mauaji ya wazee na walemavu wa ngozi.

Akitoa hotuba yake ya kwanza baada ya kusimikwa, Askofu Mwaipopo aliiomba Serikali isifumbie macho viashiria vyote vya upotevu wa amani ambayo ni tunda la upendo na haliwezi kupatikana kwa ncha ya upanga.

Askofu Ambele Mwaipopo alionyesha kupishana kauli na waziri mkuu kwakutaka kusitishwa kwa mchakato wa uundwaji wa Katiba Mpya kwa kuwa Bunge la Katiba limepuuza maoni ya Watanzania yaliyowasilishwa na Tume ya Jaji Joseph Warioba.

“Tusione aibu kujikosoa kama tumekosea...zoezi hilo lisitishwe ili tujipange upya lakini kuendelea kupuuza maoni ya Watanzania itatugharimu,” alisema Askofu Mwaipopo huku akishangiliwa na waumini.
Alisema kanisa hilo litaendelea kuwahamasisha wananchi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ili waweze kusaidia kupatikana kwa viongozi wenye nia ya kuboresha maisha yao na kuondoa wanaosababisha umasikini.
“Nchi hii ni tajiri, ina rasilimali nyingi, umasikini unatokana na kuwa na viongozi wanaojijali wenyewe badala ya kuangalia maisha ya Watanzania wote...sasa tutahakikisha tunahamasisha wananchi kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura ili watuchagulie viongozi safi,” alisema. 

Awali, Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Dk Alex Malasusa alitaka viongozi wa Taifa kubadilika na kuwa na dhamira ya kutenda kile wanachokizungumza kwa kuwa wamekuwa mabingwa wa kuongea kuliko kutenda.
Dk Malasusa alisema viongozi wamekuwa mstari wa mbele kuzungumzia rushwa wakati hawana dhamira ya kupambana nayo, hivyo imefika wakati matendo yao yaendane na kauli zao.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Pinda alisema mchakato wa uundwaji wa Katiba Mpya unaondelea ni halali kwa kuwa Bunge hilo lipo kisheria na haliwezi kusitishwa, kinachofanyika ni kuboresha yaliyomo kwenye Rasimu iliyowasilishwa kwao.
“Walioandaa ile Rasimu ni binadamu kama sisi, kuna mambo mengi waliyasahau, sasa tunayaboresha.
“Hatuwezi kupitisha vilevile ile Rasimu, wananchi wangetushangaa kulikuwa na upungufu mwingi kama kwenye ardhi, haki za binadamu na za walemavu,” alisema Pinda.
Alisema kama tatizo ni muundo wa muungano anafikiri kuna haja ya wananchi kupiga kura ya maoni kama wanataka muungano wa aina gani.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment