UKAWA IKISHINDA UCHAGUZI MKUU MCHAKATO WA KATIBA UTARUDIWA!!

Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Halima Mdee.{Picha na Maktaba}

 Siku moja baada ya viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutangaza mpango wa kusaini makubaliano ya kusimamisha mgombea mmoja katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, imeelezwa kuwa endapo utachukua dola, utarejea upya mchakato wa kuandika Katiba.

Hayo yalisemwa kwa nyakati tofauti na viongozi wa mabaraza ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Furahisha jijini Mwanza juzi.
Walisema mchakato huo utarudiwa kwa kutumia Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katibailiyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.

 Pia, viongozi hao waliwataka Watanzania waliofikisha umri wa kupiga kura, kujiandikisha katika Daftari la Wapigakura mara baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuanza uandikishaji huo.
Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Halima Mdee akihutubia mamia ya wananchi waliofurika kwenye viwanja hivyo, alisema maoni ya wananchi waliyoyatoa mbele ya Tume ya Warioba yamewekwa kando kwa masilahi ya wachache.
“Ni kwamba, Ukawa tukishinda uchaguzi ujao mwakani, mwaka 2016, mchakato wa Katiba utaanza upya kwa kutumia Rasimu ya Jaji Warioba... Warioba na wenzake walitengeneza Rasimu yenye manufaa kwa Taifa zima si genge la watu wachache,” alisema Mdee.
“Sasa (mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi, Andrew) Chenge na wenzake kwa kuona itawabana katika maeneo ya uwazi na maadili wameichakachua.
“Hatuwezi kukubali kuiona asilimia 80 ya maoni yenu mliyoyatoa kwa Jaji Warioba ikiwekwa kando na kuingizwa yao... ikija ikataeni, ikataeni, tupeni kule. 
Kama theluthi mbili wamechakachua katika kura ya maoni, watakiona,” alisisitiza.
Nae Katibu mwenezi wa Bavicha, Edward Simbeye alisema wanachokitaka katika Katiba Inayopendekezwa ni huduma bora za afya na si mabomu ya machozi, maji safi na chaki shuleni si virungu vya polisi.
“Polisi wanatumika vibaya. Ili kuhakikisha tunajikomboa kutoka utumwa wa Serikali ya CCM, tujitokeze kujiandikisha katika Daftari la Wapigakura ili tuanze kuiondoa CCM kuanzia uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwakani, ndiyo tuseme kwaheri CCM,” alisema Simbeye.
Naibu katibu mkuu wa Bawacha (Bara), Kunti Yusuph alisema Katiba Inayopendekezwa iliyokabidhiwa kwa Rais Jakaya Kikwete, imeshindwa kuziba mianya ya rushwa na maadili kwa viongozi wa umma na badala yake kujiwekea mazingira ya kuendelea kuwanyonya Watanzania.
“Tukicheza na Katiba hii waliyoipendekeza ma-CCM, ikipita tutakuwa tumejichimbia kaburi wenyewe... hatutaki na tutaipinga kona zote. Tumeanza hapa tutazunguka nchi nzima,” alisema Yusuph.
Mbunge wa viti maalumu (CUF), Mkiwa Kimwanga alisema kazi inayofanywa na Ukawa itaendelea kuanzia chaguzi za Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu ili kuhakikisha CCM haiendelei kuwanyanyasa wananchi.

 “Katika sherehe za Uhuru wa Tanganyika mwaka huu, vijana wa halaiki walitumia Sh775 milioni, weka mbali polisi, ndege za kivita na mengineyo, halafu leo mnaambiwa mchangie ujenzi wa maabara, hamuoni kama huu ni wizi,” alihoji Mkiwa.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment