JESHI
la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, jana liliimarisha ulinzi ndani
na nje kwenye majengo ya Makao Makuu ya Jeshi hilo na kusababisha
taharuki kubwa kwa wapita njia baada ya Mwenyekiti wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Freeman Mbowe, kuwasili katika
ofisi hizo.
Bw. Mbowe alifika
katika ofisi hizo saa tano asubuhi kwa ajili ya mahojiano akidaiwa kutoa
kauli ya kuitisha maandamano yasiyo na kikomo nchi nzima ili
kushinikiza Bunge Maalumu la Katiba lisitishe vikao vyake kabla ya
Oktoba 4 mwaka huu.
Nje ya ofisi hizo,
kulikuwa na askari wenye mbwa, gari la maji ya kuwasha, askari waliokuwa
na sare za jeshi wakiwa na silaha za moto na waliovaa kiraia ambao
walionekana wakiranda maeneo yote ya Posta Mpya.
Gari ya Bw. Mbowe
ilipofika lango kuu la kuingilia katika ofisi hizo, lilizuiliwa na
polisi ambao walimtaka ashuke na kuingia ndani peke yake bila gari
lakini wafuasi wake waliokuwa nje, walianza kupiga kelele wakitaka
aruhusiwe kuingia na gari.
Wafuasi hao walisikika
wakiimba "People's Power...People's Power" na wengine wakisema "Rais
ajaye, Rais ajaye...amewasili Makao Makuu ya Polisi".
Mzozo huo ulidumu kwa
dakika 10 ndipo akaruhusiwa kuingia nagari lake ambapo muda mchache
baadaye, aliwasili Mwanasheria wa CHADEMA, Bw. Tundu Lissu akiwa kwa
miguu akazuiliwa kuingia ambapo mzozo huo ulidumu kwa robo saa
akaruhusiwa.
Wengine waliozuiliwa
kuingia katika ofisi za Makao Makuu ya jeshi hilo ni Mbunge wa Kawe, Bi.
Halima Mdee, Mbunge wa Nyamagana, mkoani Mwanza, Bw. Ezekiah Wenje na
Bw. Joseph Mbilinyi mbunge wa Mbeya Mjini baada ya kufika katika ofisi
hizo kwa kuchelewa.
Wafuasi wa chama hicho
walionekana wakiranda katika maeneo mbalimbali ya Posta Mpya baada ya
kutimuliwa nje ya geti la Makao Makuu ya Polisi.
Baadhi ya wananchi
waliofika Posta Mpya kwa shughuli mbalimbali, waliingiwa na hofu ya
kupigwa mabomu ya machozi kama zitatokea vurugu kati ya polisi na
wafuasi wa CHADEMA ambapo baadhi ya watu waliofika Makao Mkuu ya jeshi
hilo kwa mahitaji ya kiofisi, walilazimika kuondoka.
Kauli ya John Mnyika
Ilipofika saa saba
mchana, Mbunge wa Ubungo, Bw. John Mnyika, alitoka nje ya ofisi za jeshi
hilo ili kuzungumza na wafuasi wa chama hicho akiwataka wawe watulivu
wakati Mbowe akiendelea kuhojiwa.
"Baada ya kuingia
ndani, Mbowe alioneshwa mkanda wa video waliodai alitoa kauli za
uchochezi zenye kuhamasisha vurugu katika mikutano...muda wote alikuwa
hajaanza kuhojiwa kwa sababu kulikuwa na ubishani baada ya kuoneshwa
mkanda.
"Mbowe alitakiwa kutoa
maelezo kwa kuandika barua ya kukiri yeye ni mchochezi lakini alikataa,
badala yake alikubali kuandika barua yenye maelezo kuwa kwanini
amekataa," alisema.
Baada ya masaa mawili,
Bw. Lissu, alitoka nje ya ofisi hizo baada ya mahojiano kumalizika na
kusema kuwa, Bw. Mbowe amepewa dhamana ambayo ilikuwa ikishughulikiwa na
Bi. Mdee na kiongozi mwingine wa CHADEMA hivyo aliwataka wafuasi wa
chama hicho watawanyike kwani wakikaidi, polisi watatumia nguvu.
"Kilichoafikiwa ni
kwamba, Mbowe atasindikizwa na moja ya magari ya polisi hivyo nawaomba
muondoke eneo hili muende katika ofisi za chama au nyumbani bila kufanya
maandamano yoyote hadi mtakapotangaziwa," alisema Bw. Lissu.
This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
0 comments:
Post a Comment